Kituo cha afya Mirerani chaelemewa kuhudumia wagonjwa 23,184

Diwani wa Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia akisoma taarifa ya miezi mitatu ya kata hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kinahudumia wagonjwa kutoka wilaya tatu za Simanjiro, Arumeru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro hivyo kipandishwe hadhi kuwa hospitali.

Simanjiro. Kituo cha afya Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kinazidi kulemewa kwa kuhudumia watu wengi kwani kwa muda wa miezi mitatu wagonjwa 23,184 wa Wilaya tatu wanapata huduma, hivyo kipandishwe hadhi kuwa hospitali.

Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia ameyasema hayo wakati akisoma taarifa ya miezi mitatu ya kata hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Lucas amesema kituo hicho cha afya kinapaswa kupandishwa hadhi kuwa hospitali kwani kwa siku kinahudumia wagonjwa 276 kutoka wilaya tatu.

Amesema kituo hicho cha afya kinahudumia wagonjwa wa kata za Endiamtu, Mirerani, Naisinyai na Shambarai wilayani Simanjiro, Mbuguni wilayani Arumeru mkoani Arusha na Mtakuja wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

"Kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa 23,184 wanaopata huduma kwenye kituo cha afya Mirerani kwa muda wa miezi mitatu, kinapaswa kupandishwa hadi kuwa hospitali," amesema Lucas.

Hata hivyo, ametaja magonjwa 10 yanayoongozwa kutibiwa kwa muda wa miezi mitatu kwenye kituo hicho kuwa ni shinikizo la damu na ajali za barabarani.

Ametaja mengini ni kifua, kuhara, upungufu wa damu, kisukari, mafindofindo, tumbo, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na mimba zinazoharibika.

Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema hawana kituo cha afya wala zahanati hivyo serikali inapaswa kutekeleza sera yake ya kuwa na kituo cha afya kila kata kwa kujenga eneo hilo.

Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema wana changamoto ya ukosefu wa kituo cha afya ila wana zahanati nne, ambapo tatu ni za serikali na moja ya binafsi.

Diwani wa kata ya Terrat Jackson Ole Materi amesema kituo kipya cha afya kinaendelea kujengewa kwenye eneo hilo na kinaendelea vizuri.