Kizimbani akidaiwa kuomba rushwa ya Sh400,000 amtibu mgonjwa

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imemfikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza  ofisa tabibu wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Joseph Marwa (45) kwa madai ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh400,000.

Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imemfikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza  ofisa tabibu wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Joseph Marwa (45) kwa madai ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh400,000.

Akizungumza kwa njia ya simu leo Ijumaa Juni 11, 2021 mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Frank Mkilanya amesema Marwa alipokea fedha hiyo kutoka kwa ndugu wa mgonjwa (jina limehifadhiwa) ili amfanyie mgonjwa huyo upasuaji.

"Mtuhumiwa alimuomba ndugu huyo Sh600,000 ili amfanyie upasuaji mgonjwa ila baadaye alipewa Sh400,000 ili kufanikisha jambo hilo," amesema Mkilanya.

Mkilanya amesema baada ya uchunguzi wa tuhuma hizo kukamilika  mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza Juni 8, 2021 na kufunguliwa shauri la rushwa namba 60/2021.

"Baada ya kusomewa na mwendesha mashtaka wa Takukuru Dorothea Kinyonto mbele ya hakimu Lukumay mtuhumiwa alikana mashtaka yanayomkabili, hivyo alipewa dhamana hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa tena Julai 1, 2021," amesema Mkilanya.

Pia amesema Takukuru wilayani Kwimba mkoani humo Juni 4, 2021 ilimfikisha mahakama ya Wilaya ya Kwimba mwenyekiti wa kitongoji cha Mwang'ombe wilayani Kwimba, Leonard Holomol (45) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh24,000 kwa watu 12 ili awasaidie kupata vitambulisho vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

"Aliwaambia watoe  Sh2,000 kila mmoja ili awasaidie kupata kitambulisho cha Nida ili waweze kuwa na sifa ya kuwa wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-Tasaf," amesema Mkilanya.

Ameongeza kwamba mwenyekiti huyo aliwaeleza wananchi hao kwamba ili waweze kupata kitambulisho cha Nida wanatakiwa kutoa fedha kitu ambacho sio utaratibu halali na ni kinyume Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kusomewa mashtaka yake na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Jovin Majura mbele ya hakimu, John Jagadi alikana mashtaka yanayomkabili na kuachiwa kwa dhamana hadi Julai 15,2021 kesi hiyo itakaposikilizwa tena.