Kizimbani kwa kugushi nyaraka, kujipatia Sh6.4 milioni

Muktasari:
Watu wawili akiwemo Mchumi mkuu Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Halima Mpita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe kwa kosa la kuhujumu uchumi.
Songwe. Watu wawili akiwemo Mchumi mkuu Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Halima Mpita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe wakituhumiwa kwa Makosa Mawili, likiwemo la Uhujumu uchumi na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajili wao na kujipatia Sh6.4milioni
Imedaiwa mbele ya Hakimu Nemes Chami Leo February 16, 2022 na mwendesha mashitaka wa Takukuru, Simone Mapunda kuwa washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo la Uhujumu Uchumi namba 3 ya mwaka 2022 ambapo kwa makusudi washitakiwa wakiwa ni Mwenyekiti na Katibu wa kamati ya manunuzi ya hospitali ya rufaa ya mkoa Songwe waligushi nyaraka zilizowawezesha kujipatia kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa ni kosa na nikinyume cha sheria.
Amewataja washitakiwa hao ambao ni mshitakiwa namba moja Halima Ajali Mpita ambaye ni Mchumi mkuu katika ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Songwe na mshitakiwa wa pili Ellis Mwaikambo ambaye ni Afisa Ugavi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kwa nyakati tofauti Kati ya Octoba 26 ,2019 na Novemba 25,2019 walitenda makosa mawili ambayo ni kumdanganya mwajiri wao ,kwa kuandaa nyaraka za uongo ambayo ni Muhtasari wa kikao cha kamati ya manunuzi ya ujezi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali teule ya Mkoa na iliyokuwa kamati ya manunuzi ya Hospitali Octoba 26 ,2019, wakiwa na lengo la kuonesha kwamba kamati hiyo imefanya kikao na kukubali kununua kifaa cha kuchanganyia saruji (concrete mixture ) ili kurahisisha shughuli za Ujenzi Hospitalini hapo Jambo ambalo si la kweli.
Mapunda amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya 2007 ,ikisomwa sambamba na aya ya 21 ya Jedwali la 1 na kifungu cha 57 (1) na kifungu 60 (2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi ,sura ya 200 marejeo ya mwaka 2002 .
Ametaja Kosa la pili likiwa ni kuisababishia hasara Serikali kinyume na Aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na kifungu 60 (2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2002 kwa kununua kifaa cha kuchanganyia saruji chenye thamani ya Sh6,370, 000 00 ambapo msimamizi wa mradi huo wa Ujenzi alikikataa kwa sababu ya kutokidhi vigezo na kukosa matumizi .
Washtamiwa kwa pamoja wamekana mashitaka hayo na Hakimu Nemes Chami ameahirisha shauri Hilo mpaka Machi 2, 2022 kwa lengo la kusikiliza hoja za awali.
Pia washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kila mmoja kudhaminiwa na watu wawili kwa Bondi ya Sh5 milioni