Kizimbani kwa tuhuma za ulawiti, ubakaji mtoto wa miaka nane

Mkazi wa eneo la Ilkiding'a wilayani Arumeru, Calvin Abraham (19), akiwa katika Mahakama ya wilaya ya Arusha, ambapo anakabiliwa na makosa mawili ya kulawiti na ubakaji wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka nane. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Mkazi wa eneo la Ilkiding'a wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Calvin Abraham (19) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na makosa mawili ya ulawiti na ubakaji wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka nane.


Arusha. Mkazi wa eneo la Ilkiding'a wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Calvin Abraham (19) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na makosa mawili ya ulawiti na ubakaji wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka nane.

Leo Alhamisi Januari 19, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Bittony Mwakisu mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti hadi Septemba 5, 2022.

Akimsomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Neema Mbwana alidai kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyakazi wa hoteli, ametenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alidai kosa la kwanza ni kulawiti kinyume na kifungu cha 154(1) a na 2, cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo eneo la Ilboru ya Juu, kwa kumwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi mwenye umri wa miaka nane.

Kosa la pili anadaiwa kumbaka kwa nyakati tofauti mwanafunzi huyo kati ya mwezi Agosti hadi Septemba 5, 2022.

Akimsomea maelezo ya awali Wakili huyo alidai kuwa Septemba 5, 2022 mama wa mtoto huyo alisikia mtoto wake akilalamika kwamba sehemu zake za haja kubwa zinamuuma, baada ya taarifa hizo alimuuliza mwathirika wa taarifa hizo nini kimetokea.

Alidai kuwa mwathirika alimweleza mama yake kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anambaka na kumlawiti mara kadhaa na kumpa Sh500, huku akimkanya kuwa iwapo atamweleza mtu atamchoma kisu.

Mama alipoendelea kumhoji mtoto huyo alidai mtuhumiwa huyo amekuwa akimtendea vitendo vya kumuingilia kinyume na maumbile na mara ya mwisho ilikuwa siku hiyo 5/9/2022.

"Baada ya taarifa hizo mama alimkagua mwanaye na wakati akitaka kumshika sehemu zake ya siri alilalamika anasikia maumivu makali na baada ya hapo waliamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na walipewa PF3 na kwenda hospitali kwa ajili ya ukaguzi wa kidaktari," alidai wakili Neema.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa, baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitali utabibu wa kidaktari ulifanyika na matokeo yalionyesha mtoto huyo alikuwa ameingiliwa sehemu zake za siri na kinyume na maumbile na mwingilio huo ulikuwa wa kitu butu na kuonyesha alikuwa amebakwa na kulawitiwa.

Mshtakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo na Hakimu Mwakisu kuahirisha kesi hiyo hadi Februari Mosi, 2023 ambapo upande wa jamhuri  utaanza kutoa ushahidi kutokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika.