Kizungumkuti mabasi 70 ya ‘mwendokasi’ mabovu

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki mbili kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuhakikisha mabasi 70 mabovu yanafanyiwa marekebisho na yanarudi kuendelea na kazi ili kuondoa adha ya usafiri huo kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Chalamila ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Oktoba 12, 2023 alipotembelea kituo cha mabasi hayo Kimara ikiwa imepita siku moja tangu Mwananchi Digital iripoti adha ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi katika kituo hicho.

Mradi huo ulioanza mwaka 2016 mpaka sasa una mabasi 210 kwa mujibu wa Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Willium Gatambi huku Chalamila akisema mabasi 70 ni mabovu, hivyo mazima na yanayofanya kazi kusalia 140.

Chalamila amesema mtoa huduma analipwa fedha katika mradi huo hivyo anashangaa kwanini idadi kubwa ya mabasi ni mabovu huku mahitaji ya wananchi yakiwa makubwa.

"Baada ya wiki mbili nitataka kuona magari hayo yote yanarudi barabarani ili kuwapinguzia adha ya usafiri wananchi.

"Kwani sitakuwa tayari kuona Rais Samia Suluhu Hassan aliye na nia njema na huu mradi anatukanwa kwasababu tu ya uzembe wa watu fulani kushindwa kutimiza majukumu yao,”amesema Chalamila.

Mbali na maagizo hayo kwa Dart, pia Mkuu huyo wa mkoa wenye idadi ya watu takribani milioni 5.4 kutokana na takwimu za Sensa bya watu na makazi yam waka 2022 amesema kwa muda wa wiki nzima atakuwa akifanya ziara za asubuhi katika vituo vya mabasi hayo ili kukagua hali ya usafiri.

Kuhusu ujio wa mabasi mengine, Chalamila amewataka wananchi kuwa na subra kwa kuwa mchakato wa kuyaleta bado unaendelea.

Hata hivyo, wakati Chalamila akifanya ziara alipokea baadhi ya mapendekezo kutoka kwa abiria kuhusu njia mbadala ya kupunguza ama kumaliza kabisa adha hiyo inayotesa wakazi wa Dar es Salaam.

Joram John, mmoja kati ya wasafiri ameshauri ili kuwe na ufanisi wa mradi huo ni vyema Dart atafutiwe mshindani katika kutoa huduma hiyo.

“Mradi huu ili uwe na ufanisi nashauri apatikane mshindani kwa kuwa aliyeopo ni kama ameshindwa kazi,”ameshauri.

Naye, Sarah John amemueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa adha hiyo ya usafiri huwa zaidi kuanzia saa 11 hadi saa mbili asubuhi ambapo watu wengi huelekea kazini na maeneo yao ya biashara huku akiomba Serikali kuongeza mabasi kwani yaliyoko hayatoshi.

Jana Jumatano, Oktoba 11, 2023 Mwananchi Digital ilifanya mahojiano na Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Dart, Willium Gatambi kuhusu kiini cha tatizo hilo ambapo alisema linasababishwa na watu wengi asubuhi kuelekea upande mmoja pia hakuna mfumo rasmi wa kuongozea mabasi hayo.

“Watu wengi kwa mfumo wa jiji la biashara, asubuhi wanaelekea mjini na jioni kuelekea majumban hivyo sio jambo la ajabu kuona abiria wakiwa wengi majira hayo upande mmoja.

“Pia hakuna mfumo rasmi wa kuongezea magari, ndio maana kuna saa abiria wanakuwa wengi na wakati mwingine wanakuwa wachache,”alisema Gatambi