Kizungumkuti Meya Moshi kudaiwa kupigwa

Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo

Moshi. Baada ya kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii inayodai kuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo alipigwa na diwani wa Mji Mpya, Abuu Shayo baada ya kurushiana maneno katika kikao cha kamati ya mipango miji ya Halmashauri hiyo. Kidumo amekanusha kuwapo kwa tukio hilo.

Taarifa zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii juzi jioni zimedai katika kikao hicho kulijitokeza sintofahamu iliyosababisha meya huyo kupigwa.

Purukushani hiyo inadaiwa imesababisha askari wa halmashauri kuingilia kati na hata diwani Shayo alipotoka nje ya ukumbi alisikika akisema yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake, na hata akigombea kama mgombea binafsi atashinda.

Ingawa kanuni za uendeshaji wa Kamati za Kudumu za Halmashauri ni siri, hivyo kuwa vigumu kufahamu kwa hasa nini kimejitokeza, lakini meya huyo amekanusha kupigwa au kutokea tafrani yoyote, lakini Shayo anathibitisha kuwa imetokea.

Akizungumza na wanahabari jana waliotaka athibitishe au kukanusha kutokea kwa tukio hilo, Meya Kidume amesema taarifa kuwa juzi amepigwa zimemstaajabisha na anashindwa kujua aanzie wapi kutoa majibu kwa jambo ambalo halikutokea.

“Jana (juzi) tulikuwa na kikao cha kamati ya mipango miji na tulimaliza saa saba, baada ya hapo tulipata chakula na nikaondoka kwenda kwenye kikao cha halmashauri kuu ya kata yangu ya Njoro hadi saa 10 alasiri,” amesema.

Kwa mujibu wa meya huyo, ameshangaa jioni kukuta taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikisema amepigwa sana, ameumizwa na amelazwa hospitali, akisema jambo hilo limeleta mtafaruku na amepokea simu nyingi. “Nikashangaa nimepigwa na nani nikawa nashindwa hata kuelewa. Nimepigiwa simu usiku kucha. Hizi habari si za kweli  ni za uongo na aliyetoa hizi taarifa nitalazimika kumtafuta ili anieleze nimepigwa na nani na nimelazwa hospitali gani,” amesema.

Amesisitiza “Ataniambia habari hizi kazipata wapi mpaka akaamua kuzusha jambo kubwa kama hili, dhamira yake mimi siifahamu. Vikao vya kamati ni vya siri, kama kuna diwani alizungumza huyo mngenisaidia kunionesha.

Hata hivyo, Diwani Abuu kwa upande wake amedai juzi walikuwa na kikao cha mipango miji na yeye ni mjumbe halali. “Nilikuwa nikihoji uhalali wa ukuta wa halmashauri kujengwa kwa Sh920 milioni wakati wanajenga jengo la ghorofa kwa Sh1 bilioni.

“Mimi ni Diwani wa Mji mpya nafikisha vipindi vinne sasa. Julai 13, 2023 tulikuwa na kikao cha mipango miji na kama mnavyojua vikao vya kamati ni vya siri lakini ilifikia mahali siri ikawa si siri tena kwa sababu vurugu zilitokea mpaka nje,” amesema.

Amesema kiini cha vurugu ni kuhoji matumizi hayo ya fedha, ambapo amedai hilo halikumfurahisha meya ambapo alishuka kwenye meza kuu na kumfuata mahali alipoketi, ndipo tafrani ya ‘kushikana’ mashati ilipojitokeza.

“Alikuwa kule jukwaa la juu wanapokaa wale mameya na mkurugenzi siye tuko chini, akateremka akanifuata huku chini na mimi nikatoka kwenye kiti changu nikamwambia unataka nini sasa ndiyo hiyo ikatokea kushikana.

“Lakini mimi sijamfuata mbele pale nikaenda nikamshika. Yeye ametoka kule akanifuata huku kwa sababu tu nahoji Sh920 milioni. Hiyo ndiyo ambayo imemuuma,” alidai huku akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan atume timu kuchunguza.

Jitihada za Mwananchi kumpata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa lakini mmoja wa wasaidizi wake amesema itaandaliwa taarifa na kutolewa kwa wanahabari.