KONA YA MSTAAFU: Haki ya mstaafu kulipwa pensheni ya Sh50,000 kwa mwezi
Mstaafu anamshukuru sana Mungu kwa kumfanya kuwa miongoni mwa waliokuwa wakiitwa 'Matineja' (Teenagers) wa enzi hizo za miaka ya katikati ya sabini waliomaliza Kidato cha Nne ambao, japo akili zao hazikuwahusisha kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano, walipata jambo lililokuwa jema zaidi.
Matineja wakawa ni miongoni mwa wanafunzi waliopewa ajira moja kwa moja kutoka sekondari ili kulijenga Taifa letu hili, likiwa na miaka kumi na tano tu tangu lipate Uhuru, kwa jasho lao, damu zao na peni zao za Bic, kwenye mashirika, viwanda na kampuni kibao zilizokuwapo!
Inashangaza kidogo kwamba nchi yetu ikiwa na raia milioni kumi na sita tu, ajira zilitutafuta kutoka shuleni, lakini sasa hivi tukiwa karibu milioni 65, vijana wetu wanatoka vyuoni na kusaka ajira kwa vibatari. Eti maendeleo...!
Matineja tukachimba mitaro na kutengeneza zege lisilolala ili kujenga ofisi nyingi zilizokuwa zikihitajika mno, huku mikono yetu na kalamu zetu za Bic zikiandika kila kilichopaswa kuandikwa. Kwa kalamu, maana hiki tulichokuja kukiita kompyuta kinachorahisisha kazi kilikuwa bado kiko Sayari ya Pluto!
Haikuwa kuweka zege lisilolala au kuchimba mitaro tu, bali hata mishahara yetu ya Sh380 (mia tatu themanini kwa mwezi, sio elfu tatu mia tatu themanini!) ilikatwa, kwanza kwa kujengea shule na kulipa kile kilichoitwa PAYE (Lipia Upatacho) ili vijana wetu wapate elimu bure bwerere kwenye shule hizo tulizozijenga!
Pamoja na makato hayo, tukakatwa pia kile kilichoitwa NPF, akiba ya wafanyakazi, tulichoaminishwa kuwa tutaiona faida yake tutakapostaafu na kuzeeka miaka 40 ijayo. Sasa hivi!
Kwa makato haya, tukajikuta mwisho wa mwezi tukirudi nyumbani na shilingi mia mbili na tisini ambazo, cha ajabu, ni kuwa kama hukuwa 'tineja macho juu juu', ziliweza kukufikisha mwisho wa mwezi unaofuata! Tupeni heshima zetu, vijana wetu. Wazee wenu tumetoka mbali!
Wahenga wetu ndio waliosema mithali ya "Tenda wema, uchape lapa zako, usingoje shukurani." Miongoni mwa waliofaidika na PAYE zetu zilizokatwa kwenye mishahara yetu ya shilingi mia tatu themanini wakawa vijana wetu ambao sasa ni waheshimiwa wanaoweza kupanga waheshimiwa wenzao wapokee mishahara hata ya shilingi milioni... mama wee!... 14 na marupurupu na marapurapu yake kwa mwezi!
Ndiyo, sasa ni waheshimiwa wanaoweza kupanga hata sisi tuliowasomesha kwa PAYE za mishahara yetu, sasa tulipwe pensheni ya shilingi ngapi, tukianza na pensheni ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi, kisha laki moja na elfu tano kwa mwezi tuliyokaa nayo kwa miaka ishirini na moja kabla ya pensheni kuwa shilingi laki mbili na elfu hamsini tangu Oktoba mwaka jana.
Wapendwa waheshimiwa, mkumbukeni sasa mstaafu wenu wa kima cha chini ambaye mlisoma bure na kula bure, chakula vyote vikitokana na PAYE yake iliyonyofolewa kwenye mshahara wake wa shilingi mia tatu themanini kwa mwezi! Ni kweli kuwa alitenda wema na akachapa lapa bila kungoja shukurani. Ni wakati wenu wa kulipa shukurani za wema wa wastaafu wetu wa kima cha chini.
Mkumbuke kuwa gharama pekee waliyoipata wazazi wenu wakati mkisoma sekondari ilikuwa ni kuwanunulia sare za shule na gharama nyingine ndogondogo, lakini PAYE ya huyu mstaafu iliweza kuwalisha kwa miaka minne yote mliyosoma sekondari.
Kumbukeni hili. Kumkosesha amani mstaafu wetu huyu wa kima cha chini aliyefanya yote haya kwa PAYE yake ni kumlipa pensheni ya shilingi laki mbili na elfu hamsini tu, ni kutomtendea haki. Kumlipa pensheni ya shilingi laki mbili na elfu hamsini, halafu matibabu ya magonjwa yake ya uzee yawe juu yake mwenyewe, ni kutomtaka awe na amani.
Kama mnaweza kupanga anayesemekana kuwa ni mwakilishi wake alipwe shilingi milioni... mama wee!... 14 na marupurupu na marapurapu yake kwa mwezi, na mstaafu wetu aliyewezesha yote haya yawezekane alipwe shilingi... "Eloi, Eloi, lama sabaktani?" ('Kisambaa' kwa msisitizo), laki mbili na elfu hamsini kwa mwezi, hamtendi haki. Hakuna amani pasipo na haki.
Kaeni chini na mtafakari vyema ili wastaafu wetu wa kima cha chini walipwe angalau shilingi laki tano kwa mwezi kwa yote waliyoayatenda. Amani ndiyo itakuwepo.
0754 340606 / 0784 340606.