KONA YA MSTAAFU: Fedha zinapomwagwa nje nje lakini hazimhusu mstaafu!
Mstaafu wetu anajikuta akifanya kile kinachomshangaza hata yeye mwenyewe, cha kujikuta akikishukuru kibubu cha wastaafu kwa kufanya kilichofanywa na maofisa wake wahusika kuona mwezi jana ukipita bila mstaafu kuhakiki na hivyo kukosa laki mbili na nusu zake za pensheni!
Maofisa hao, wengine wakiwa wapenzi wa makala zake tangu enzi hizoo, walimtafuta mstaafu wetu hadi kumpata huko Chongoleani alikokuwa anatibiwa na kumhakiki ili asikose tena shilingi laki mbili na nusu zake anazozihitaji kutokana na maradhi yanayomsibu. Anawashukuru wahusika wa kibubu chake.
Mstaafu wetu anajikuta akitamani kuwe na wema wengi wenye huruma kama maofisa wale, hasa wale wasemekanao kuwa wanawakilisha wananchi na wanaopokea shilingi milioni... mama wee!... 14 na marupurupu yake kwa mwezi, akamuonea huruma mstaafu wetu kama kibubu kilivyomuonea huruma, na akatoa shilingi milioni moja yake kama pole yake kwa mstaafu, wazo ambalo aliliondoa fasta akilini mwake kwa neno la... maawe!
Anawazaga pia, na hata huwapaga pole wanamuziki wetu wastaafu kwa "miziki" yao iliyotuburudisha baada ya kazi ngumu za kuijenga nchi enzi hizoo, kuwa angalau kuna watu huingiwa na huruma na kuwapa pole wastaafu hao wanamuziki wetu ya shilingi milioni kumi! Ninaamini wastaafu wasomaji, kuna siku nami watanikumbuka! Tuombe...
Ndiyo, mstaafu wetu bado yuko "mitaa" ya huko Chongoleani akitibiwa maradhi haya ya kizee ambayo hushika kasi fasta mtu anapostaafu, na hakuna matibabu ya dezo kama ilivyokuwa wakati ameajiriwa, na kuyafanya kutoka maradhi ya wazee, ambao wamejizoea Panadol, mpaka kuwa maradhi ya "wastaafu", ambayo matibabu yake ya bure yameishia kuwa "maneno ya kanga".
Ni maradhi ya "wastaafu" yanayowasumbua mno wastaafu, lakini mstaafu wetu anajikuta akizidiwa na kuiona Kinondoni ikimhusu anaposikiliza au kusoma mitandao kuhusu nchi ilivyo na fedha, lakini zinaishia kumwagwa mwagwa nje ili baadhi ya wenzetu walegeze mikanda ya suruali zao kutokana na kupanuka kwa viuno vyao, huku wastaafu wakiendelea kukaza mikanda ya suruali zao kiasi cha kuongeza matundu mawili matatu ya ziada ili mikanda yao ibane kisawasawa kama walivyoambiwa enzi hizoo wakati wakilijenga Taifa hili!
Yaani wao walioijenga nchi bado wakaze mikanda, na waliokuja jana tu walegeze mikanda. Mwe...!
Ndiyo, mstaafu wetu ana maradhi ya "wastaafu", lakini anaposikiliza ama kusoma habari jinsi hela zetu zinavyomwagwa mwagwa, chekwa nje, anaishia kuiona Kinondoni ilee ikimhusu.
Anasoma kuhusu hasara ya shilingi bilioni kadhaa kutokana na safari zisizoeleweka za shirika letu la ndege. Anasoma kuhusu hasara ya bilioni kadhaa kwenye bwawa la umeme lenye jina kubwa lisilostahili kule mji kasoro bahari, inavyolitia Taifa hasara. Anaishia kuomba Panadol!
Anasoma kuhusu trilioni kadhaa zilizotengwa kwa ajili ya safari kadhaa wa kadhaa za waheshimiwa wetu. Pia anasikia kuhusu mabilioni kadhaa yanayotengwa na ofisi kadhaa kwa ajili ya vinywaji na vitafunwa kwa ajili ya wageni wa ofisi hizo. Maumivu yanapozidi, anatamani akamuone daktari. Na nini, wakati pensheni yake hajaihakiki na matibabu ya bure kwa wazee yameishia kuwa maneno ya kanga tu!
Mstaafu anaposikia mabilioni kadhaa yakioteshwa mbawa kwa hasara inayopatikana kwa hili treni la kisasa tunaloaminishwa kuwa, pamoja na kuharibika kwake mara kadhaa kutokana na kunguru na nyani, kama tunavyoelezwa, ni bora zaidi kuliko la Uingereza, huishia kuhisi shinikizo la juu la damu kumpanda, na anaiona Kinondoni ilee!
Halafu anaposikia adhabu tunayopaswa kuwapa watu hawa wanaolitia hasara Taifa, na kutaka kuitafuna wenyewe keki ya Taifa, ambayo mstaafu "aliwasha mkaa" kuchangia "upishi" wa keki hiyo, kuwa ni kuwazomea tu badala ya kuwatia ndani na kuwashikisha adhabu kwa kutaka kutafuna peke yao keki ya Taifa aliyosaidia "kuipika" kwa jasho, anachoka kabisa!
Inasikitisha sana kwamba, pamoja na upotevu wa matrilioni na mabilioni haya, hakuna hata bilioni moja ama mamilioni kadhaa "yanayopotezwa" njia ili yaingie kwenye mifuko ya suruali za wastaafu waweze kupata japo pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi! Hilo tu watu wameuchuna, kama siyo kuvaa uso wa mbuzi!
Tumkumbuke hata yule nabii mwema aliyevunja vunja meza na viti vya wahuni aliowakuta wakifanya biashara ndani ya nyumba ya baba yake. Ni wakati sasa wa sisi "Nguchiro", milioni 65, kuvunja vunja meza na viti vya wahuni hawa wanaofanya biashara na hela zetu. Tuamke...
0754 340606 / 0784 340606