KONA YA MSTAAFU: Fedha zinapomwagwa nje nje, lakini hazimhusu mstaafu!
Mstaafu wetu anajikuta akifanya kile kinachomshangaza hata yeye mwenyewe, cha kujikuta akikishukuru sana kibubu cha wastaafu kwa kufanya kilichofanywa na maofisa wake wahusika kuona mwezi jana ukipita bila mstaafu kuhakiki na hivyo kukosa laki mbili na nusu zake za pensheni!
Maofisa hao, wengine wakiwa wapenzi wa makala za Mstaafu Wetu toka enzi za Daily News na Sunday News, walimtafuta mstaafu wetu hadi kumpata huko Chongoleani alikokuwa anatibiwa na kumhakiki ili asikose tena shilingi laki mbili na nusu zake za pensheni. Anawashukuru sana wahusika wa kibubu chake.
Mstaafu wetu anajikuta akitamani kuwe na wema wengi wenye huruma kama maofisa wale, hasa wale wasemekanao kuwa wanawakilisha wananchi na wanaopokea shilingi milioni... mama wee!... 14 na marupurupu na marapurupu yake kwa mwezi, akamuonea huruma mstaafu wetu kama kibubu kilivyomuonea huruma, na akatoa shilingi milioni moja yake kama pole zake kwa mstaafu, wazo ambalo aliliondoa kwa kasi akilini mwake kwa neno la... maawe!
Amemuwazaga pia mama, ambaye ana uhakika kuwa anasomaga kona hii ya wastaafu na hata huwapaga pole wanamuziki wetu wastaafu kwa miziki yao iliyotuburudisha baada ya kazi ngumu za kuijenga nchi enzi hizoo, kuwa anaweza kuingiwa na huruma na kumpa pole mstaafu wetu ya shilingi milioni kumi!... Mama, ninasubiri!
Ndiyo, mstaafu wetu bado yuko huko Chongoleani akitibiwa maradhi haya ya kizee ambayo hushika kasi fasta mtu anapostaafu, na hakuna matibabu ya dezo kama ilivyokuwa wakati ameajiriwa, na kuyafanya kutoka maradhi ya wazee, ambao wamejizoea Panadol, mpaka kuwa maradhi ya wastaafu, ambayo matibabu yake ya bure yameishia kuwa “maneno ya kanga.”
Ni maradhi ya wastaafu yanayomsumbua mno mstaafu, lakini mstaafu wetu anajikuta akizidiwa na kuona Kinondoni inamhusu anaposikiliza au kusoma mitandao kuhusu nchi ilivyo na fedha, lakini zinaishia kumwagwa mwagwa nje, ili baadhi ya wenzetu walegeze mikanda ya suruali zao kutokana na kupanuka viuno vyao, huku wastaafu wakiendelea kukaza mikanda ya suruali zao kiasi cha kuongeza matundu mawili au matatu ya ziada ili mkanda wake ubane sawasawa, kama walivyoambiwa enzi hizoo, wakati wakilijenga Taifa hili!
Yaani, wao walioijenga nchi bado wakaze mikanda, na waliokuja jana tu walegeze mikanda. Mwe...!
Ndiyo, mstaafu wetu ana maradhi ya wastaafu, lakini anaposikiliza ama kusoma habari jinsi hela zetu zinavyomwagwa mwagwa chekwa nje, anaishia kuiona Kinondoni ilee ikimhusu. Anasoma kuhusu hasara ya shilingi bilioni kadhaa kutokana na safari zisizoeleweka za shirika letu la ndege, anasoma kuhusu hasara ya bilioni kadhaa kwenye bwawa la umeme lenye jina kubwa lisilostahili kule mji kasoro bahari inavyolitia Taifa hasara. Anaishia kuomba Panadol!
Anasikia kuhusu trilioni kadhaa ambazo zimetengwa kwa ajili ya safari kadhaa za waheshimiwa wetu na watoto wao. Na pia anasikia kuhusu mabilioni kadhaa yanayotengwa na ofisi kadhaa kwa ajili ya vinywaji na vitafunwa kwa wageni wa ofisi hizo.
Maumivu yanapozidi, anatamani akamuone daktari. Na nini, wakati pensheni yake hajaihakiki na matibabu ya bure kwa wazee yameishia kuwa maneno ya kanga tu!
Mstaafu anaposikia mabilioni kadhaa yakioteshwa mbawa kwa hasara inayopatikana kwa hili treni la kisasa tunaloaminishwa kuwa, pamoja na kuharibiwa kwake mara kadhaa na kunguru na nyani, ni bora zaidi kuliko la Uingereza, huishia kuhisi shinikizo la juu la damu kumpanda na anaiona Kinondoni ilee!
Halafu anaposikia adhabu tunayopaswa kuwapa wahuni hawa wanaotaka kuitafuna wenyewe keki ya Taifa, ambayo mstaafu amechangia upishi wa keki hiyo, kuwa ni kuwazomea tu badala ya kuwatia ndani na kuwashikisha adhabu kwa kutaka kutafuna peke yao keki ya Taifa aliyosaidia kuipika kwa jasho, anachoka kabisa!
Inasikitisha sana kwamba, pamoja na upotevu wa mabilioni na matrilioni haya, hakuna hata bilioni moja ama mamilioni kadhaa “yanayopotezwa” njia kwenda mifukoni mwa wastaafu wapate japo pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi! Hilo tu.
Tumkumbuke hata yule nabii mwema aliyevunja vunja meza na viti vya wahuni aliowakuta wakifanya biashara ndani ya nyumba ya baba yake. Ni wakati sasa wa sisi Nguchiro, milioni 60, kuvunja vunja meza na viti vya wahuni hawa wanaofanya biashara na hela zetu. Tuamke...
0754 340606 / 0784 340606