Prime
KONA YA MSTAAFU: Pensheni inapomfanya Mstaafu acheke kisha kulizwa!
Mstaafu wetu amejikuta akishtuka sana mwisho wa mwezi uliopita alipoingiziwa kimya kimya Sh450,000 kama pensheni yake ya Septemba.
Sh450,000! Mstaafu wenu hakujua kama acheke au alie, kama sio kulizwa!
Kulikuwa na sababu mbili tatu muhimu sana zilizomfanya ashindwe kujua mara moja kama acheke ama alie.
Kuhusu mshiko huu uliomjia ghafla kufumba na kufumbua bila taarifa yoyote.
Mstaafu wetu alikuwa ameishapanga kuwa pensheni itakapoingia kwenye akaunti, kesho yake ndio atajikongoja kwenda kutoa laki moja yake iliyobaki baada ya benki kufanya vitu vyake vya kukata marejesho yanayopaswa kwa mkopo aliochukua! Tukumbuke kuwa mwana wa mbuzi kamba ni yake!
Lakini ujumbe wa kibubu husika wa kuniambia kimeniingizia pensheni ya Septemba ya Sh450,000 ukanifanya Nijikongoje kwenda kuzitoa huku nikiwa bado sina hakika kama ni zangu kweli!
Híi maana yake ni kwamba, kwa kuchukua kisicho changu nilichokuwa nimefanya pamoja na kuwa kimeingia kwenye akauti yangu na kwa sababu nilikuwa tayari nimekiingiza kwenye matumizi yangu, kwa mpango wa 'Kiendacho kwa mganga hakirudi' pamoja na kwamba kama hazikuwa zangu marejesho yangenihusu!
Lakini ..ngoja kwanza! Je kama hatimaye Siri-kali ilikuwa imeamua kufanya kile wastaafu' tulicholilia Kwa miaka mitano na makala 260 za kona ya wastaafu' kuomba nyongeza ya pensheni ili tuweze kukabiliana kweli na hali ngumu ya maishi tukipokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka ishirini ? Kama ilikuwa hivyo, sasa kimya kimya cha nini?
Siri-kali hii inayopenda ionekane inawajali wastaafu' wake si ingejitokeza kwa mbwembwe zote na kutangaza kuwa inamuongeza mstaafu wake wa kima cha chini pensheni ya Sh450,000 kwa mwezi, ili kuboresha maisha yake, potelea mbali kwamba wastaafu huenda tunaishia kugeuzwa 'kausha damu' kuboresha maisha ya wakopaji badala ya sisi wenyewe!
Kwa nini nyongeza itoke kimya kimya watu wasipate nafasi ya kuisifu Siri-kali kuwa inawajali sana wastaafu' wake wa kima cha chini na imewaongeza Pensheni yao ya mwezi ili wapate Sh450,000 na angalau Kinondoni walisikie redioni tu?
Lakini...ngooja kwanza tena! mstaafu akakumbuka miaka sita au saba nyuma ambapo kibubu au Siri- kali vilipatwa na upungufu wa fedha mahali na wastaafu' tukatakiwa tupokée pensheni yetu ya shilingi laki moja na elfu tano kila baada ya miezi mitatu, yaani shilingi laki tatu na elfu kumi na tano, halafu unakaa miezi mitatu bila pensheni!
Wastaafu' tunakumbuka kilichotokea na maumivu tulioyapata. Yaani penseni yenyewe ya shilingi laki moja na elfu tano haitoshi, halafu uambiwe itaunganishwa ya miezi mitatu na utaipata mara moja kila baada ya miezi mitatu!
Mstaafu wetu hajui kwa nini aliiona Kinondoni kama ilisogea karibu au ni maumivu yake tu!
Ni jambo jema kwamba sera hiyo ya 'lump sum' ilidumu kwa mwaka mmoja au miwili tu na ikaisha na tukarudi kwenye 'laki si pesa' yetu kwa mwezi, lakini tuliipata freshi kwa kupauka!
Mstaafu sasa anasubiri kuona pensheni ya Oktoba ikoje.
Itakuwa laki nne elfu hamsini ili kudhibitisha kuwa hatimaye Siri-kali imeboresha kweli maisha ya mstaafu.
...au kutakuwa hakuna kitu hadi miezi mitatu baadaye hadi Desemba! Wahusika wajitahidi kutafuta njia nyingine ya kutafuta ela na sio kukimbilia kwenye kibubu cha pensheni ya mstaafu. Mnatuumiza!