Korea Kaskazini yakubali kufunga injini zake

Muktasari:
Kuhusu suala lililompeleka la silaha Moon alisema Kaskazini imekubali "kufunga kabisa" injini zake katika tukio ambalo watahudhuria wataalamu wa masuala ya silaha za nyuklia na makombora.
Pyongyang, Korea Kaskazini. Korea Kaskazini imekubali "kufunga kabisa" injini za kufanyia majaribio ya makombora pamoja na eneo la kurushia la Tongchang-ri, "huku wakishuhudia wataalamu kutoka kwa mataifa husika," imefahamika.
Hayo yameelezwa Jumatano na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in baada ya mkutano wa kilele na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un jijini Pyongyang.
Pia Moon alisema Kim atafanya ziara ya kihistoria katika Korea Kusini "siku chache zijazo".
Viongozi hao wametia saini azimio la pamoja mwishoni mwa majadiliano yao katika siku ya pili. Walikubaliana kuwa watafanya kazi kuifanya Rasi ya Korea kuondokana na tishio la nyuklia.
Moon ambaye alikwenda Kaskazini kwa ajili ya kupata mwelekeo mpya kukwamua mazungumzo yaliyokwama katika jitihada za kuondoa kabisa silaha za nyuklia, alisema ziara hiyo inaweza kufanyika mwaka huu labda tu yawepo "mabadiliko maalum".
Kuhusu suala lililompeleka la silaha, Moon alisema Kaskazini imekubali "kufunga kabisa" injini zake katika tukio ambalo watahudhuria wataalamu wa masuala ya silaha za nyuklia na makombora.
Korea Kaskazini imefanya majaribio na kurusha makombora kutoka eneo la Sohae, ambako licha ya programu yake ya makombora kupigwa marufuku na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bado alitumia maeneo kadhaa mengine kurusha maroketi ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Pyongyang.
Picha za setelaiti zilizopigwa Agosti zilionyesha wafanyakazi wakifungua injini za kufanyia majaribio ukiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyompa Rais Donald Trump wa Marekani.
Moon pia alisema Kaskazini inaweza kufunga kituo cha nyuklia cha Yongbyon ikiwa Marekani itachukua “hatua zinazolingana” ikiwa ni tahadhari muhimu.