Kuanika vifaa juani kwamponza Mganga Kivule

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomari Satura, amemvua madaraka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kivule, jijini Dar es Salaam kwa kushindwa kusimamia majukumu yake.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kipande cha video kumuonesha mtumishi wa hospitali hiyo, Deborah Chacha akisafisha vifaa vya kuhudumia wagonjwa vya hospitali hiyo na kuvianika juani.

Hatua hiyo, iliibua sintofahamu huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo, Jomari Satura ametoa taarifa akisema vifaa hivyo vilivyoonekana kupitia video hiyo havikuwa vimetumiwa na wagonjwa na kwamba tukio lililoonekana ni jukumu la kawaida la uchambuzi na usafi wa kawaida wa vifaa hivyo kutoka stoo ya kuhifadhia vifaa.

Hata hivyo, kupitia mtandao wake wa Twitter, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu juzi aliandika,"nimeona clip inayohusu mtumishi wa afya akichambua, kusafisha na kuanika vifaa vya Hospitali katika Hospitali ya Kivule Dar es Salaam.

Kitendo hiki ni kinyume na taratibu na miongozo ya Kanuni za Udhibiti wa Maambukizi (Infection Prevention and Control). Tayari viongozi wa Mkoa wa Dar es salaam wanalifanyia kazi suala hili na watatoa taarifa rasmi,” ameandika.

Wakati taarifa hiyo ya Mkurugenzi ikifafanua, baadaye ilitolewa taarifa nyingine na Msemaji wa jiji hilo, Tabu Shaibu ikieleza kuwa uamuzi wa kumvua umetokana na kushindwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho unazingatia ubora, miongozo, taratibu na sheria za afya.

Taarifa hiyo inaeleza Satura ameelekeza muuguzi kiongozi wa wodi ya wazazi kuondolewa kwenye nafasi yake na kupangiwa majukumu mengine.

Amesema kwa niaba ya uongozi wa jiji, Satura aliomba radhi kwa mamlaka na umma wote wa Watanzania kwa kitendo hicho kilicholeta usumbufu na taharuki.

“Ofisi ya Mkurugenzi inakemea vikali vitendo kama hivi na itahakikisha havijirudii tena na kuwataka watumishi wote wa sekta ya afya na sekta nyingine kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zote,” amesema Shaibu.

Waziri Ummy, katika andiko lake kuhusu video hiyo, alitoa rai kwa wataalamu wa afya kuzingatia mafunzo na miiko ya kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tamisemi zitaendelea kuchukua hatua ili kuimarisha ubora wa huduma za afya.
“Ninamshukuru mwananchi aliyerekodi na kuisambaza clip hii.

Nitoe wito kwa wananchi kutoacha kuibua mambo kama haya yanayotokea katika vituo vyetu vya kutoa huduma za Afya vya umma na binafsi, kuongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya nchini kwa kuwa afya zetu ni wajibu wetu,” ameandika.