KUELEKEA MIAKA 2 YA SAMIA: Baada ya vyumba madarasa, zamu ya walimu na vifaa

Uwekezaji kwenye vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwamo vitabu unatajwa kuwa jambo muhimu baada ya ujenzi wa miundombinu shuleni.

Miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeacha alama mojawapo kubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu hususan upande wa miundombinu.

Maendelo haya ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 katika shule za sekondari. Ujenzi huo pia ulihusisha vyumba 3,000 katika shule shikizi 970 katika maeneo mbalimbali nchini.

Ujenzi huo ulitokana na fedha za mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya janga la Uviko-19. Jumla ya Sh1.3 trilioni zilitolewa na shirika hilo ambazo pia zilitumika kujenga vituo vya afya zaidi ya 200.

Akizungumzia ujenzi huo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia sekta ya elimu, Gerald Mweli, alisema ujenzi hasa wa madarasa 3000 katika shule shikizi utaweka historia nchini.

“Tukishajenga madarasa 3000 kwenye hizi vituo shikizi 970 tunaamini tunakwenda kuweka historia tena kubwa kwa shule hizi za msingi mpya 970 pia tutakuwa tumewaondolea adha watoto kutembea umbali mrefu, ” alisema Mweli aluipozungumza na vyombo vya habari.

Kabla ya ujenzi huo, mwaka 2021 Tanzania ilikuwa na vyumba vya madarasa 132,389 katika shule za msingi na 50,538 katika shule za sekondari.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za elimumsingi (Best) za mwaka 2021 zilizotolewa na Tamisemi.


Kidato cha tano na sita mbioni

Ikiwa jithada za kuondoa uhaba wa madarasa kwa shule za sekondari, Katibu Mkuu wa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo aliiagiza Serikali kuelekeza nguvu kwenye ujenzi wa madarasa na shule za sekondari za kidato cha tano na sita ili kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Chongolo alibainisha hayo mjini Singida hivi karibuni, wakati wa mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara yake ya siku sita mkoani humo ambapo alitembelea wilaya zote za Singida kuanzia Manyoni, Ikungi, Iramba, Mkalama na Singida akikagua utekelezaji wa ilani va uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.

Alisema Serikali iliweka nguvu kubwa kuhakikisha kwamba shule za msingi madarasa ya kutosha yanajengwa ambapo ndani ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, zaidi ya madarasa 20,000 yamejengwa nchini kote.

“Sasa ni muda mwafaka kwa Serikali kuongeza nguvu kwenye kujenga madarasa na shule za sekondari za kidato cha tano ili kuongeza idadi ya wanafunzi,’’ alisema.

Bila shaka kauli ya Chongolo ambaye ndiye mtendaji mkuu wa chama kinachoongoza Serikali, inaweza kuwa sawa na agizo kwa mamlaka kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika ngazi hiyo muhimu ya elimu nchini.


Wasifu mkakati

Mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko anasema ujenzi wa madarasa hayo umesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wengi waliokuwa wanasoma darasa moja, jambo linalofanya utoaji elimu kuwa bora.

“Waliokuwa wanachaguliwa awamu ya pili kujiunga kidato cha kwanza sasa hawapo na badala yake wote wanaingia kaa wakati mmoja. Hii inafanya wote kuwa sawa na hakuna anayeachwa nyuma,” anaeleza Nkoronko.

Anaongeza kuwa ufundishaji wa mwalimu darasani, kabla ya ujenzi wa madarasa haya ulikuwa wa shida hususani katika kuwasimamia wanafunzi waliokuwa zaidi ya kiwango cha Serikali yaani wanafunzi 45 kwa chumba kimoja.

“Sasa wanafunzi wamepungua darasani na mwalimu anaweza kwenda huku na kule.Hilo limeongeza pia chachu ya wanafunzi kuhudhuria shuleni, kwani baadhi walikuwa wakiacha kutokana na kukosa sehemu ya kukaa,’’ anasema.

Kwa upande wake, mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Ochola Wayoga, anasema kwa mtazamo wake, ujenzi wa madarasa huo unaweza kuwa umepunguza asilimia 20 ya msongamano wa wanafunzi katika madarasa, huku akieleza kuwa jambo hilo bado lipo katika shule mbalimbali.

“Kuongeza madarasa haya haimaanishi imeboresha miundombinu ya shule zote, tunazo shule nyingine ambazo bado zimechakaa na zinahitaji kutengenezwa,’’ anasema.


Uwekezaji zaidi

Pamoja na ujenzi huo wa vyumba vya madarasa kupokelewa kwa bashasha, wadau bado wanaitaka Serikali kufanya zaidi ya ilichofanya, kwa kuwa elimu haishii kwenye miundombinu pekee.

“Tusiangalie tu idadi ya madarasa, pia tuangalie kuwa ni namna gani tumeweza kumfikia kila mtu kupata elimu, mtoto akifika shule kile anachofundishwa kinagusa uchumi wao kijijini, jamii, tamaduni. Isijekuwa unamfundisha mtoto jiografia ya Indonesia,” anasema Wayoga.

Anasema mfumo wa elimu wa nchi unatakiwa uwe ule unaoendana na maisha yao ya kila siku, na hilo linawezekana kwa kuwa na vitu kadhaa wakiwamo walimu wenye sifa.

Hoja ya walimu inaungwa mkono na mwalimu Richard Mabala, anayesema:

‘’Mara zote nimekuwa nikisema mwalimu bila darasa anaweza kufundisha na wanafunzi wakafanya vizuri, ila darasa bila mwalimu darasa haliwezi kufanya kitu. Tuongeze walimu, tuwape motisha ili waweze kutumia madarasa hayo vizuri.Wakiwepo wa kutosha tutaona faida ya uwekezaji uliofanyika.’’Anashauri pia ongezeko la bajeti na uwepo wa mitalaa inayoendana na wakati wa sasa.

“Pamoja na hayo bado nasubiri kuona mitaala mipya itakuwaje itaendana vipi na uboreshaji wa miundombinu na hali ya walimu shuleni, itafanya nini katika lugha ya kujifunzia kwani haina maana kuwaweka wanafunzi wengi darasani halafu hawajui wanachofundishwa,” anasema Mabala.

Anaongeza kusema kuwa baada ya ujenzi huo, ni muhimu kwa Serikali kupima matokeo yake kwa maana kile kilichozalishwa kutokana na ujenzi huo ili thamani ya gharama iliyotumika ionekane.

Kwa upande wake, Nkoronko anasema baada ya ujenzi wa vyumba, sasa Serikali ijikite katika vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

‘’Ipeleke vifaa vya ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu, upatikanaji wake utaongeza chachu, madarasa, vitabu na vifaa vya kufundishia vyote vikipatikana vitakuwa vinakidhi mahitaji ya utoaji bora wa elimu.

Anaongeza kuwa umefika wakati wa kufanya umaliziaji wa maabara zote katika shule za sekondari za kata, ili kutoa nafasi ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo katika masomo ya sayansi badala ya kuendelea kusoma nadharia pekee.

“Ukizunguka mikoani shule nyingi za kata zilijenga majengo ya maabara ambayo kwa sasa yamebaki kuitwa maabara lakini hayana vifaa. Umefika wakati uwekezaji katika maabara hizi ufanyike ili wanafunzi wajifunze kwa vitendo,” anaeleza.