Kuhusu EPA bado Tanzania itajadili kuuridhia na kuutekeleza mkataba

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel baada ya kuwasili makao makuu ya baraza hilojijini Brussels, Ubelgiji. Picha ya ikulu

Muktasari:

Wakati mjadala kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ukiendelea, Serikali imesema inafanyia kazi changamoto zilizosababisha isiuridhie mkataba huo.

Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ukiendelea, Serikali imesema inafanyia kazi changamoto zilizosababisha isiuridhie mkataba huo.

Juzi, taarifa ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ilisema itafanya majadiliano na EU kuhakikisha makubaliano hayo yanakuwa na manufaa sio kwa Tanzania pekee bali EAC nzima.

“Serikali inapenda kuwaambia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba Tanzania bado haijaridhia mkataba wa EPA na itatoa taarifa rasmi baada ya majadiliano ya kitaalamu kuhitimishwa,” inasomeka sehemu ya taafa hiyo.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Charles Michael huko Brussels nchini Ubelgiji juzi, alisema Tanzania na EU zimekubaliana kukutana katika robo ya kwanza mwaka huu ili kuafikiana mambo yaliyobaki.

“Niko hapa kukuthibitishia kwamba tuko tayari kuendesha mkutano huo katika jiji letu zuri la Dar es Salaam wiki ya kwanza ya Machi 2022, imani yangu ni kwamba uamuzi wa kuandaa mkutano huu unaakisi umuhimu wa pande zote mbili (Tanzania na EU) kuhakikisha makubaliano yanafikia tamati kwa kuzingatia manufaa ya pande zote,” alisema.


EPA ni nini?

EPA ni mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na mkataba huo unalenga kufungua masoko ya nchi hizo kwa bidhaa zao kuingia Ulaya na zinazotoka Ulaya kuuzwa Afrika Mashariki.

Mchakato wa mkataba huo ulianza mwaka 2010 na ulitakiwa kusainiwa Oktoba 2016 lakini wakuu wa nchi za EAC wakajipa muda zaidi wa kutafakari suala hilo na kukubaliana kukutana Januari 2017 wakiwa na majibu.

Hata hivyo, Januari hiyo ziliendelea kushikilia misimamo tofauti huku kila moja ikiangalia masilahi yake binafsi. Pengine hilo ndilo jambo linalosababisha ugumu wa kuwa na msimamo wa pamoja na kuzifanya Kenya na Rwanda kuwa pekee zilizotia saini mpaka sasa.

Ili mkataba huo uanze kutekelezwa, ni lazima nchi zote wanachama wa EAC zitie saini hata ikibaki mmoja itakayoweka ngumu basi hauwezi kutumika.

Kutokana na kuchelewa kusainiwa kwa EPA, nchi za EAC ambazo zinauza bidhaa zake Ulaya kama vile Kenya ziliathirika hasa mwaka 2019 baada ya Ulaya kuweka vikwazo kwenye bidhaa zake hadi pale itakapozishawishi nchi nyingine kuuridhia mkataba huo.


Kwa nini Tanzania haijasaini

Tanzania iliweka wazi kwamba vipengele vya mkataba wa EPA vitaikwamisha kutimiza malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa sababu kuna kipengele kinachotaka bidhaa zote kutoka Ulaya ziruhusiwe kuingia Afrika Mashariki.

Mei 2017, Hayati John Magufuli alisema suala la EPA ni gumu kwa sababu lina vipengele vinavyozibana nchi za Afrika Mashariki na wanachama wa EU si wamoja ndiyo maana Uingereza ilijitoa.

“Mkataka huu una masharti mengi, tunahitaji muda wa kuyasoma na kufanyia mabadiliko ili yasituumize. Pia, Jumuiya ya Ulaya wameiwekea embargo (vikwazo) Burundi wakati nayo ni mwanachama wa EAC, kuna mambo mengi ya kuangalia hapa,” alisema Rais Magufuli kwenye mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi za EAC.

Burundi pia haijasaini mkataba huo kutokana na vikwazo ilivyowekewa na EU kutokana na mgogoro wa kisiasa uliokuwa unaendelea wakati huo. Burundi inaitaka EU kuondoa vikwazo vyake kwanza ndipo EPA ijadiliwe.

Kenya ipo tayari kwa sababu inanufaika na mkataba huo kwa kuuza bidhaa zake Ulaya, hata hivyo, mataifa mengine ya Afrika Mashariki bado hayazalishi kwa wingi bidhaa za viwandani.

Uganda na Sudan Kusini bado hazijasaini pia lakini zinasubiri kuona manufaa ya mkataba huo kabla ya kufanya uamuzi. Rwanda tayari imesaini mkataba huo lakini inaruhusu majadiliano zaidi.


Wataalamu wazungumza

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Humphrey Moshi alisema Tanzania inatakiwa kubadili mkakati wa kutoka kuwatumia wataalamu wa Serikali pekee kwa kuwaongeza wengine kutoka sekta binafsi.

“Mambo yote kwenye EPA yajadiliwe kwa uwazi, tusikubali kufanya vitu vitakavyokwamisha jitihada za Serikali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,” alisema Profesa Moshi.

Mchumi mwandamizi, Dk Donath Olomi alisema Tanzania inahitaji intelijensia ya uchumi kufanya uchambuzi yakinifu kuhusu ya kuyalinda.

“Tunapswa kuwa makini, uamuzi wowote tutakaoufanya utakuwa na athari katika uchumi wetu,” alisisitiza Dk Olomi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Stephen Chamle alisema sekta binafsi inahitaji ushindani kuboresha shughuli zao.

“Ili tuwe na ushindani Serikali iondoe vikwazo vya kibiashara visivyo vya lazima ili kurahisisha mazingira,” alisema Chamle.