Kuolewa, kuachika kulivyo mzigo wa talaka kwa wanawake – 3
Muktasari:
- Kuolewa na kuachika kumeendelea kuwa mwiba mchungu si kwa watoto tu, bali wazazi wa watoto hao hususani kina mama kwani hulazimika kuondoka nao na familia zao kuelemewa na mzigo wa malezi, huku kina baba wakiendelea na maisha mengine ikiwamo kuoa na kuanzisha familia nyingine.
- Tafiti zinaonyesha watoto wa wazazi waliotalikiana mara nyingi hukumbwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ya kupata matokeo duni shuleni ikilinganishwa na wenzao wa familia zisizo na talaka.
Tatu Abdallah, mkazi wa Mikindani Mtwara, anasema, "Nimegundua wanaume siku hizi wana tabia mbaya, hasa hawa wanaojifanya wanakwenda kutafuta maisha. Wakifika huko wakipata wanawake, hata kama wana kipato, wanafanya makusudi kutokukuhudumia ili udai talaka kwa hiari yako.
Anasema wengi hawahudumii wake na watoto hali aliyosema inachochea wanawake kudai talaka.
“Bora uwe msela udange kwa halali kuliko kuwa kwenye ndoa jina, inayokuzuia kuendelea na maisha mengine,” anasema Tatu.
Akizungumzia kadhia ya talaka, Zaituni Said mkazi wa Mtaa wa Tandika, Mtwara ambaye ni mama wa watoto watano, wakiwemo pacha watatu, anasema hajawahi kuzaa bila kufunga ndoa.
Anasema alishawahi kuishi na kulea watoto peke yake baada ya kuachika.
Zaituni anasema mwaka 2012 aliolewa na akaishi na mumewe kwa miaka sita na kupata mtoto mmoja, lakini baadaye waliachana.
Anasema mwaka 2016 alifunga ndoa tena na mwanaume mwingine na alipata mimba mwaka huohuo. Siku za kujifungua zilipokaribia, alirudishwa kwao kijijini Mtimbwilimbwi, Mtwara vijijini.
“Nilijifungua pacha watatu wakiwa na uzito mdogo, nikahamishiwa Hospitali ya Nanguruwe kwa ajili ya uangalizi zaidi. Ilibidi niwalee kwa kutumia mbinu ya kangaroo, mimi nilijifunga wawili kifuani na mama yangu (Hadija Chande) alijifunga mmoja, mpaka wakaongezeka uzito.
“Sikuwa na pesa na hata kusafirishwa nilipewa na Serikali Sh20,000 za matumizi na walinisafirisha kwa gharama zao hadi Nanguruwe. Mume wangu hakuwahi kufika hata siku moja hospitali wala kunipigia simu kujua hali ya watoto licha ya kupewa taarifa,” anasema Zaituni.
Anasema aliporudi kijijini, maisha yalikuwa magumu kwa sababu alikuwa hana kazi na baba yake mzazi ni mlemavu wa macho, hivyo alizunguka mitaani kufanya vibarua ili apate fedha kidogo za chakula.
“Hali ilinishinda watoto walipofikisha mwaka na miezi minane niliwaaga wazazi wangu kuwa nakuja Mtwara mjini. Waliniuliza kama nitaweza kuwalea watoto, nikawajibu nitapambana. Wakanipa baraka zao nikaja mjini na kufikia kwa dada yangu, nikifanya vibarua vya kulima mashamba ya watu na kufua hadi nikapata pesa ya kupanga huku mabondeni,” anasema Zaituni huku akionyesha eneo analoishi ambalo limejaa maji.
Anasema alipata taarifa kuwa babu yao watatu (baba wa mumewe) amefariki, akaenda kijijini kwa mumewe kuzika na kudai talaka yake, maana hawakuwa na mawasiliano yoyote wala huduma kwa watoto kutoka kwa baba yao. “Nilipofika, nilimkuta ana mwanamke mwingine na mtoto, nikadai talaka akanipa.”
“Niliumiza zaidi kwani rafiki zake anaofanya nao shughuli za ujenzi waliniuliza kama nilipata mchango walionichangia Sh50,000 kwa ajili ya watoto, nikawajibu sikupata, mmoja wao akasema alitumia hiyo pesa kwenda kuolea.”
“Yaani amechangiwa pesa iwasaidie watoto wake ambao hawajawahi hata kuwaona, ameitumia kwenda kuolea, niliumia sana,”anasema Zaituni kwa masikitiko.
Zaituni anasema aliporudi mjini aliendelea kulea watoto wake, na walipofikisha miaka minne akaolewa tena na mwanaume mwingine na kupata mtoto mmoja. Baada ya miezi miwili walitengana.
“Kisa cha kuachana ni kwamba alikuwa anafanya kazi bandari hapa Mtwara, baadaye akahamishiwa Kigoma. Alikaa sana huko na alinitumia nauli kwenda, lakini nilipofika nikamkuta na mwanamke anaishi naye. Nikaona mazingira siyo rafiki nikaachana naye. Mwanzoni alikuwa anatoa msaada lakini sasa hivi hatoi, kwani mkataba wake kule umekwisha na hana hela.”
“Hivi sasa, nafanya vibarua vya kulima na fedha ninayopata ninakwenda feri kununua dagaa, nakaanga na kutembeza mitaani, au nakwenda kukosha wa wenzangu nalipwa ujira kidogo. Hii yote ni kuhakikisha watoto wangu wanakula,” anasema Zaituni.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mtawike (ambako anaishi Zaituni), Raphael Ndila, anasema, “Huyu mama anaishi kwenye nyumba ipo kwenye eneo la maji na inafikia hatua namuonea huruma.”
“Ulaji na kusomesha watoto ni shida, hata wanavyokwenda shuleni ni vichekesho, kuna wakati wanakwenda tumbo wazi. Hali ya maisha ni ngumu sana kwake,”anasema Ndila huku akitokwa na machozi.
Akizungumzia kadhia ya kuolewa na kuachika, Salma Hamad, mkazi wa Koani Unguja, anasema aliolewa akiwa na miaka 18 mkoani Ruvuma na akapata watoto watatu, lakini aliachika na kuachiwa watoto wote.
“Maisha yalipokuwa magumu niliwaacha na mama yangu nikaja Unguja kujitafuta, nako nikampata mume. Niliishi naye kwa miaka mitano tukajenga nyumba maeneo ya Kidimni kwa kuchanga pesa, mimi nilikuwa ninauza nazi na yeye anafanya shughuli zake.”
“Nililala kwenye hiyo nyumba mwaka mmoja tu, akaenda kwao Rufiji (Tanzania Bara) kuchukua mwanamke akaanza kunitimua ndani mwisho akaniacha, ikanibidi nirudi huku Koani nilikozoea,” anasema Salma.
Anasema ni mwaka wa tisa hakuna anayetaka kumuoa, kwa sababuni ana mtoto aliyezaa na huyu mwanaume wa huko na alimchukua mtoto wake mmoja kutoka Ruvuma ili ampunguzie mzigo wa malezi mama yake.
“Hatuna maelewano, alinipa talaka tatu kwa mpigo na hataki kunisikia wala kuniona duniani mpaka mbinguni inanisikitisha sana,” anasimulia mama huyo.
Anasema asingesimama kidete hizo talaka zingempoteza mwanaye, kwa sababu alipokuwa akimuomba fedha ya matumizi, mwanaume alimnyima.
Anasema uamuzi wake ulikuwa amchukue mtoto ampeleke Rufiji akiwa na mwaka mmoja na nusu ili kukata mzizi wa fitina.
“Hakukubali na hata alipoanza shule alikuwa anajaribu kumuiba amuondoe Unguja kila mara. Rafiki yake aliamua kesi hiyo kwa kusema mtoto akae kwake kila anayetaka kumsalimia aende hapo. Aliishi hapo kwa miaka minne, sasa hivi ninaishi naye mwenyewe na sipati msaada wowote kutoka kwake,” anasema.
Kadhia za wanawake kuolewa mara nyingi na kutelekezewa watoto pia imemkuta Saadia Mohamed Bakari, mkazi wa mjini Unguja. Anasema ndoa yake ya kwanza aliolewa akiwa na miaka 16. Mwanaume aliyemuoa alimpa mimba na walipofunga ndoa walizaa watoto wawili, lakini kutokana na tabia yake ya kuwa na wanawake wengi na ulevi, waliachana.
“Niliposhindwa, nilitoroka nyumbani kwa wazazi wake na watoto wangu wawili. Baada ya muda nikaolewa mara ya pili na kupata mimba, lakini mwanaume huyo naye aliniacha ghafla. Mtoto alipokuwa mkubwa kidogo nilimwachia mama yangu na kwenda Muscat, Oman kufanya kazi. Niliporudi nikiwa na pesa nikapata mume mwingine lakini naye aliniacha nikiwa na mimba ya miezi miwili,” anasema Saadia.
Anasema, “baada ya kujifungua, mwanaume huyo alinikataa kwa sababu ya kuungua na moto usoni. Nililazwa hospitalini kwa miezi mitatu na kufanyiwa upasuaji. Alipoona sura yangu ilivyobadilika, alisema hanitaki na kuniandikia talaka kabla sijaruhusiwa kutoka hospitalini,” anasema.
Sasa Saadia ana watoto watano na anajitahidi kuwalea mwenyewe, akifanya biashara ndogondogo. “Nina watoto watano na nimemuacha mmoja alelewe na bibi yake. Nilipitia vipindi vigumu sana, lakini ndugu yangu aliyeko Oman alinisaidia wakati wa ugonjwa wangu. Ingawa najua nimebeba mzigo wa watoto, sitaolewa tena hivi karibuni,” anasema kwa msisitizo.
Anasema hapendi kuzini ndiyo maana hutafuta mume wa kumuoa, “huyu wa mwisho niliporudi Oman nilikuwa na pesa nilimpa pesa apeleke kwetu anioe, kila kitu nilikuwa ninamfanyia kwa sababu nilitaka stara, matokeo yake ndiyo hayo kanipa talaka nipo kitandani na bandeji za moto mwilini.
Makala haya yameandikwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation.
Usikose sehemu ya nne ya simulizi hii kesho.