Wasichana wanavyotumia ‘ndoa’ kutafuta uhuru na janga la talaka-2

Happyness Reginald.

Muktasari:

  • Kuolewa na kuachika kumeendelea kuwa mwiba mchungu si kwa watoto tu, bali wazazi wa watoto hao hususani kina mama kwani hulazimika kuondoka nao na familia zao kuelemewa na mzigo wa malezi, huku kina baba wakiendelea na maisha mengine ikiwamo kuoa na kuanzisha familia nyingine.

Katika mijadala mingi, wazazi na wataalamu wa malezi wanakubaliana kuwa talaka inaweza kuwa na athari kubwa kwa watoto kwa sababu  wanapitia mabadiliko makubwa katika mazingira yao ya nyumbani yanayoweza kuwasababishia msongo wa mawazo, huzuni na wakati mwingine hata matatizo ya kiakili na kihisia.

Tafiti zinaonyesha watoto wa wazazi waliotalakiana mara nyingi hukumbwa na changamoto kadhaa, ikiwamo ya kupata matokeo duni shuleni ikilinganishwa na wenzao wa familia zisizo na talaka.

Pia, kuna ongezeko la hali ya mmomonyoko wa maadili na talaka zinaweza kuongeza hatari ya watoto kupata matatizo ya afya ya akili.

Endelea kuisoma simulizi hii katika sehemu yake ya pili, uone namna wasichana na wanawake wanavyotaabika na talaka.

Akisimulia mkasa wa kuolewa na kuachika, Naima Khamis Hamad mzaliwa wa Pemba, lakini anaishi na kufanya kazi Unguja, anasema  aliolewa  ndoa ya kwanza akiwa na miaka 20 baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2011 iliyodumu mpaka 2014.

Hata hivyo, anasema walioana ndugu, mtoto wa baba mkubwa na mdogo (visiwani hii ni kawaida) na walikuwa wakiishi Unguja  kwenye nyumba ya familia na yeye kwao ni Pemba.

“Hii ndoa nadhani haikubarikiwa, mama yangu alikuwa haitaki, ila ndugu wengine wote walikuwa wanaitaka, pia sisi wenyewe tulipendana sana, lakini baada ya muda visa vikaanza hapo nyumbani.”

“Mama mkwe na mawifi walikuwa hawanitaki, tulikuwa tunaishi watu wanane kwenye nyumba moja, kuna kipindi nilipokuwa na mimba ya kwanza, wifi yangu alinipiga tumboni hadi mimba ikaharibika, nikarudi nyumbani Pemba, lakini mume wangu alikuja kunichukua kwa masharti tuondoke kwao, kweli akapanga chumba kimoja tukaendelea kuishi,”anasema Naima.

Anasema kuna eneo ambalo mumewe alinunua akawa ameanza kujenga nyumba na ikawa imefikia hatua nzuri, alimshauri walaze mabati wahamie waachane na nyumba ya kupanga wataimalizia taratibu wakiwa ndani.

“Kwa sababu wakati huo alikuwa ananisikiliza, akafanya kama tulivyokubaliana tukahamia,” anasema Naima.

Anasema akabeba mimba akajifungua, wazazi wake walipopata taarifa, wakamkatia tiketi ya ndege aende Pemba.

“Hii ilikuwa baada ya kupita siku tatu tu tangu nijifungue, maana Unguja sikuwa na mtu wa kuniangalia kwa karibu, na kumbuka wakati huo mimi na mume wangu tulikuwa tunaishi kwa furaha na amani,” anasimulia dada huyo.

Hata hivyo, anasema visa vilianza baada ya kubeba ujauzito wa mtoto wake wa pili.

Anasema maneno yalianza tena kutoka kwa familia ya mumewe ambao kimsingi ni ndugu zake na mumewe naye akawa hamsikilizi na wakati mwingine alikuwa analala nje na akiulizwa ugomvi mkubwa unazuka.

 “Tukashindwana nikaenda nyumbani kupumzika, l sikuchukua kitu niliondoka upepo mbaya upite, kwani tulikuwa tukiwasiliana pia.

“Baada ya miezi mitatu nikarudi kwani mume wangu hakunifuata. Nilipofika nilifanya usafi wa chumba, nikatandika kitanda na shuka nyeupe lakini aliporudi usiku, akalala na suruali, nilipomuhitaji akawa hataki, siku ya pili nikamlazimisha tushiriki tendo la ndoa akakubali, lakini hakuwa na mshawasha kama ninavyomjua.

“Asubuhi nilipoamka akawa tayari ameshaenda kazini, lakini nilishtuka baada ya kuona shuka lina matone ya damu, lakini jana usiku nilimona akinywa dawa, ila yeye hakujua kama mimi nimemuona, nikazipiga picha zile dawa nikamtumia ndugu yangu anayefanya kazi maabara ili kujua ni za nini na kama zina uhusiano na zile damu,” anasema Naima.

Anasema kabla hajapata majibu ya zile dawa, alifua shuka, lakini mumewe aliporudi alimuuliza kuhusu yale matone ya damu, akamwambia alipata maambukizi kidogo sehemu za siri, akamwambia amuonyeshe akakataa.

Anasema alimbembeleza sana baadaye alimuonyesha, “sikulala ndugu yangu kwa kile nilichokishuhudia, uume wa mume wangu ulikuwa umechanua kama uaridi, nilishangaa anaumwa ugonjwa gani, nikamuuliza akasema hajui ila alikwenda hospitali akapewa hizo dawa anazotumia.

“Baadaye ndugu yangu akaniuliza maswali kuhusu anayezitumia hizo dawa, akasema basi atakuwa anaumwa kaswende, huo ugonjwa naujua kwa kuusoma tu, sikuwahi kuwaza kama mume wangu anaweza kuumwa.

“Nikajuta kwa nini nilimlazimika kujamiiana naye. Nikamuhurumia sikumuuliza kitu, nilimuomba tu nichukue baadhi ya vitu vyangu ili niondoke zangu, akanikubalia,” anasema.

Anasema alichukua kila kitu chake kasoro kitanda na godoro na baada ya muda aliomba talaka waachane.

Naima anasema baada ya miaka mitatu kupita, aliolewa tena na kiongozi mmoja wa dini aliyekuwa akiishi Pemba, hata hivyo ndoa hiyo haikudumu, mwaka 2022 waliachana kwa kile alichodai ni kukithiri kwa masimango.

“Mwaka 2023 niliolewa ndoa ya tatu, nayo  haikudumu, hivi sasa nafanya kazi zangu naishi na watoto wangu, siwezi kusema sitoolewa, ila kwa sasa napumzika kwanza,” anasema Naima mwenye miaka 31.

Happyness Reginald Fitina ni miongoni mwa wanawake wanaoteseka na watoto baada ya kuzaa na wanaume watatu tofauti ambao wamemtelekezea watoto.

Anasema kadhia ilianza baada ya mama yao mzazi kufariki dunia na baba yao kuwatelekeza wakiwa mkoani Mtwara na yeye akahamia wilayani Masasi.

Baada ya kuishi huku na kule, ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam kwa mama yake mdogo aliyekuwa msaada pekee, lakini kwa bahati mbaya alifariki, alirudi Mtwara.

Mwaka 2007 alikutana na baba wa mtoto wake wa kwanza, “tuliishi vizuri na mwaka 2008 nilibahatika kupata mtoto wa kiume. Hata hivyo, kutokana na tabia zake za uhuni, nikaondoka mwaka 2011 na kurudi kwa dada yangu ambaye ni kama mzazi wangu, sisi tupo wawili tu. Hapo ndipo tulipoachana,” anasimulia mama huyo.

Anasema mumewe huyo tangu wameachana, hana msaada wowote kwa mtoto bali anahangaika mwenyewe kumtunza.

Anasema mwaka juzi alikataa kumlipia mtoto huyo gharama za kukaa kambini kwa madai hana fedha.

Happyness anasema kuna kipindi mwanaume huyo alimchukua mtoto akidai anaenda kuishi naye, lakini baada ya wiki mbili alimrudisha kwa dada yake Happyness akidai anasafiri.

“Lakini huyu bwana hajasafiri na nimempeleka ustawi wa jamii, lakini kila anapoitwa haji. Mtoto ni wa kiume na ana miaka 15 sasa, nalala naye chumba kimoja. Ni mateso na baba yake anafanya kazi lakini hataki kumhudumia,” anasema.

Hata hivyo anasema anaendelea kupambana na maisha kwa kufanya kazi kwenye maghalani wakati wa msimu wa korosho.

“Huku nako hakuna pesa ya maana, ukishindilia gunia unapata Sh500 na sijawahi kujaza zaidi ya magunia 30 kwa siku,” anasema mama huyo wa watoto watatu.

Anasema mwaka 2015 alikutana na mwanaume aliyeishi naye hadi mwaka 2020 wakaachana.

Lakini anasema waliishi vizuri na walipata mtoto mmoja wa kike, lakini changamoto ilikuwa kila alipomwambia aende kujitambulisha kwao au amuoe, alikataa.

“Niliona naishi kihuni sana, nikamwambia aende kwetu walau akajitambulishe ili likitokea tatizo familia ziwe zinatambua uhusiano wetu. Alikataa, nikaamua kuondoka,” anasema.

Anasema baada ya kuachana na baba wa mtoto wa pili, mwaka huohuo alimpata baba wa mtoto wake wa tatu.

Anasema bwana huyo alikuwa na nia ya kumuoa kwa sababu alienda mpaka kwa baba yake Masasi na kutoa barua na mahari, wakachukuana wakaanza maisha.

Historia inaonyesha jamii nyingi mkoani Mtwara, mwanaume akitoa barua ya posa na mahari, anahesabika ameshamuoa huyo aliyemtolea mahari.

Hivyo, Happyness anasema baada ya kuoana walihamia Masasi, ambako ndiyo nyumbani pia kwa baba wa mtoto wake baada ya maisha kumwendea kombo Mtwara.

“Tulikuwa tunaishi vizuri lakini baadaye mama mkwe akaanza visa na kunisingizia nina mwanaume, jambo ambalo hata mwanaye alilikataa. Nilipochoka nikamwambia mume wangu nataka kwenda nyumbani kupumzika.

“Wakati huo dada yangu alikuwa anaishi Dar es Salaam, nikaenda nikakaa miezi mitatu. Lakini kiukweli sikuwa na nia ya kurudi Masasi kwa sababu mama mkwe wangu ananisumbua, nikarudi Mtwara na yeye akaja tukawa tunaishi kwa dada yangu Mkanaledi. Baadaye tukatafuta nyumba hapa tunapoishi sasa.

“Tulikuwa tunaishi naye na watoto wote watatu kwenye hiki chumba kimoja, ila ndugu zake hawakupenda. Kila siku wanamuita arudi Masasi. Januari mwaka jana akapigiwa simu na wazazi wake, ikabidi aende,” anasimulia. Hata hivyo anasema mwanamume huyo alikuwa akimtumia fedha za matumizi, lakini Februari mwaka jana, aliacha kumuhudumia kwa madai ana hali ngumu.

“Ilikuwa akituma Sh5,000 anakaa wiki nzima hatumi, baadaye nikasikia anaishi na mwanamke mwingine ambaye aliwahi kunipigia simu. Huku kusini wanaume hawaoni umuhimu wa kutunza watoto. Wanachojua wao ni kuzaa tu. Ukiwa naye anakushawishi mzae na ndiyo mapenzi yao makubwa kuzaliana. Mkizaa ujue huyo mtoto ni wako,” anasema Happyness.

Akiizungumzia hali hiyo, Abduraufu Mikidadi, mkazi wa Magomeni Mtwara, anasema ugumu wa maisha ni chanzo cha wanaume kutelekeza watoto.

“Mimi pia kuna mwanamke nilikuwa ninaishi naye Lindi, nikazaa naye watoto watatu, lakini kutokana na ugumu wa maisha, nikaja huku Mtwara kujaribu labda niendeshe hata bodaboda. Kuna ndugu yangu fundi seremala aliniambia huku kidogo kuna nafuu, nikajua nikifanikiwa nitakuwa nawatumia matumizi kule nyumbani. Lakini hali haiko hivyo, mimi mwenyewe ninasota, sasa ya kuwatumia itatoka wapi,” anasema Mikidadi.

Anasema mkewe alidhani anakula maisha tu akadai talaka akampatia wameachana.

Lakini anasema hawezi kuwachukua watoto kwa sababu hana pa kuishi nao, “Mimi mwenyewe nimesitiriwa na jamaa.

Akizungumzia uhusiano na mwanamke mwingine, anasema anaye. “Mimi ni binadamu, siwezi kukaa miaka mitatu bila bibi. Lakini hilo siyo shida, tatizo ni huduma kwa familia ndiyo imetutenganisha,” anasema.


Usikose sehemu ya tatu ya simulizi hii kesho.


Makala haya yameandikwa kwa ufadhili wa Bill & Melinda Gates Foundation.