RIPOTI MAALUMU: Zaidi ya nusu ya Watanzania hawapo kwenye ndoa

Dar es Salaam. “Nina mchumba wangu nipo naye kwa miaka sita sasa kwenye uhusiano lakini akinigusia kuhusu suala la ndoa, ninaogopa na ninajihisi sipo tayari kuingia huko. Kwa sababu naona kila kukicha ndoa nyingi za watu wangu wa karibu zinavunjika,”

Ni kauli ya kijana Justin Msangi (31) mkazi wa Goba jijini hapa.

Hofu ya Msangi kuhusu kuingia kwenye ndoa, imebainishwa pia na takwimu za Ripoti ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), na kuonyesha kuwa asilimia 57 ya Watanzania hawapo kwenye ndoa.

Takwimu hizo zinamaanisha watu watatu kati ya watano nchini waliofika kwenye umri wa ndoa hawapo kwenye ndoa kwa sababu mbalimbali.

Kutokana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, umri wa mwanamke kuolewa ni miaka 15 huku mwanaume ikiwa ni miaka 18.

Hata hivyo kwa Holines Ulomi licha ya kuwa na umri wa miaka 26, hataki kusikia suala la ndoa kama ilivyo kwa Msangi. Anasema:

‘‘ Kwanza siku hizi mitandao ya kijamii inaua sana imani za watu kuingia kwenye ndoa kutokana na yale tunayoyaona ya wanandoa kuuana na kunyanyasana. Mimi naogopa hilo.’’


Ripoti kwa undani

Ripoti hiyo imeonyesha mgawanyo wa wasio kwenye ndoa kama ifuatavyo: Wanandoa waliotengana ni asilimia tano, waliopeana talaka (asilimia 1.9), wasiowahi kuwa kwenye ndoa (asilimia 38.9), wajane na wagane (asilimia 5.4) na wanaoishi kiuchumba (asilimia 6.1).

Wakati idadi ya watu wasio kwenye ndoa ikiwa kubwa, pia walio kwenye ndoa wameongezeka kidogo kutoka asilimia 34.8 mwaka 2014/2015 hadi asilimia 40.5 mwaka 2020/2021.

Pia, utafiti huo umebaini wakazi wa mijini wengi hawapo kwenye ndoa ikilinganishwa na wa vijijini.

“Idadi ya wasioishi kwenye ndoa vijijini ni asilimia 55.5 ya waliofika umri wa kuoa na kuolewa, huku mijini ni asilimia 61.5 sawa na tofauti ya asilimia sita,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Hali ya Watanzania wengi kutokuwa kwenye ndoa, mbali ya hofu, pia inatajwa kusababishwa na mwenendo wa talaka na ndoa kuvunjika kuongezeka siku hadi siku.

Takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) zinaonyesha mwaka 2019 talaka zilikuwa 442, mwaka 2020 zilifikia 511 na mwaka 2021 kulikuwa na talaka 550.

Kwa mujibu wa Rita mambo yanayochochea ndoa hizo kuvunjika ni pamoja na ukosefu wa uaminifu, ukatili na kutekeleza familia.

Nazo takwimu za migogoro ya ndoa zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum zinaonyesha kulikuwa na migogoro ya ndoa 39,571 kwa kipindi cha Julai 2021 mpaka Aprili 2022 ambapo migogoro 19,262 ilipata suluhu, 15,718 bado ipo katika usuluhishi na 4,576 ikiwa mahakamani.

Hata hivyo, licha ya takwimu za talaka na migogoro ndani ya ndoa kuzidi kuongezeka, bado idadi ya ndoa zinazosajiliwa Rita zinaongezeka mwaka hadi mwaka.

Takwimu za Rita zinaonyesha mwaka 2019, ndoa 43,479 zilisajiliwa huku mwaka 2020 zikiongezeka hadi kufikia 54,071 kabla ya kushuka kidogo mwaka 2021 na kufikia ndoa 49,000 na mwaka 2022 ndoa ziliongezeka hadi kufika 51,011.

Hali ilivyo IJC

Aidha, mashauri ya ndoa na talaka 1,358 yalifunguliwa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke (IJC) jijini Dar es Salaam katika kipindi cha kuanzia Novemba 2021 hadi Julai mwaka jana.

Idadi hiyo ni sawa na mashauri 220 yanayofunguliwa kila mwezi kituoni hapo, hali inayoonyesha kuyumba kwa taasisi nyeti ya ndoa, hasa mkoani Dar es Salaam.

Hata hivyo, kituo hicho kilifanikiwa kunusuru ndoa 29 kati ya 80, ambazo wanandoa walifikishana hapo kwa ajili ya kuzivunja.

Agosti mwaka jana, akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Naibu Msajili wa IJC, Mary Moyo, alisema mashauri yaliyoongoza kufunguliwa katika kituo hicho ni ya mirathi ambayo ni 2,911, sawa na asilimia 62 ya mashauri yote, ikifuatiwa na mashauri 1,358 ya ndoa na talaka sawa na asilimia 38.

Kwa upande wa mashauri ya ndoa yaliyofunguliwa katika kipindi hicho, Moyo alisema mashauri yanayoongoza ni ya talaka, wanandoa kuomba kutengana, mgawanyo wa mali baada ya ndoa kuvunjika, matunzo ya watoto na sehemu wanakotakiwa kuishi watoto baada ya wazazi wao kutengana.


Dar yaongoza

Ofisa usajili mwandamizi wa Rita, Jane Barongo alisema mkoa unaoongoza kwa talaka ni Dar es Salaam.

Anasema matukio ya talaka yamekuwa na vyanzo vingi huku akivitaja vyanzo vikuu vitatu,ambavyo ni kukosa uaminifu, ukatili na kutelekeza familia.

“Vyanzo vya migogoro ya ndoa mpaka kufikia talaka ni pale ndoa imeonekana kwamba haiwezi kurekebishika kwa kukosa uaminifu na mengine ni ukatili pamoja na suala la kutelekeza familia na hii utakuta mmoja wa wanandoa labda kapata nafasi ya kazi mbali, nje ya nchi anamtekeleza mwenza,” anasema .

Barongo anasema kwa Tanzania sheria ya ndoa ni muunganiko wa hiyari unaokusudiwa kuwa kati ya mwanamke na mwanaume ambao utakua wa kudumu.

“Kuna sababu zinazotokea lakini hakuna ndoa ya mkataba ingawaje kuna upungufu unaotokea kutokana na watu kutofahamiana vizuri au shida zilizojitokeza baina ya wanandoa. Kuna kitu kinaitwa talaka hii ni amri au ruhusa inayotolewa na mahakama kwa wanandoa ili kila mtu aendelee na maisha yake mahakama ndiyo inayotenganisha sisi tunasajili tu,” anaongeza.

Septemba 5 mwaka jana, Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ilishtushwa na kasi ya kuvunjika kwa ndoa nchini chanzo kikubwa kikiwa ni kumomonyoka kwa maadili huku Mkoa wa Dar es Salaam pekee ukiwa na ndoa zaidi ya 300 zinazovunjika kila mwezi.

“Tumepata hesabu (ya ndoa kuvunjika) kwa mfano Dar es Salaam pekee yake zaidi ya ndoa 300 kwa mwezi zinavunjika. Hili tunaona ni tatizo kubwa na ni janga. Sisi kama kamati tunaona haja kubwa ya kuishauri Serikali kuona jinsi ya kuchukua hatua kwa ajili ya kupambana na hali hii iliyopo,” alisema Mweyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo.


Wasemacho viongozi wa dini

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini nchini, Askofu William Mwamalanga anasema ugumu wa maisha ndiyo chanzo kikubwa cha vijana wengi kutopendelea kuoa siku za hivi karibuni.

Askofu Mwamalanga anasema tatizo hilo la watu wengi kutokuwa kwenye ndoa lipo sana katika nchi zinazoendelea kwakuwa kila mtu yupo ‘bize’ na kutafuta maisha na wepesi wa kupata aina ya maisha anayoyatamani.

“Ugumu wa maisha ndiyo sababu ya changamoto hiyo ndiyo maana utaona kuna wengine kwa ugumu huo huo wa maisha wanakubali kulelewa au kuwa ‘chawa’ ili kukidhi matamanio yao ya kiuchumi,” anasema Mwamalanga na kuongeza kuwa jamii kwa ujumla inapaswa kuchukua hatua ya kushughulikia alichokiita ni udumavu wa akili.

Mwamalanga anasema kilichoelezwa katika utafiti wa NPS kinaendana na hali halisi iliyopo katika nyumba za ibada akisema mwamko wa vijana kuoa uko chini jambo ambalo Serikali na taasisi za kidini zinapaswa kulichukulia kwa uzito. Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa anasema katika nyumba za ibada wanaiona hiyo changamoto ambayo uhalisia wake ni kama ilivyoelezwa na ripoti hiyo na chanzo cha tatizo hilo ni jamii kuiona zinaa kama jambo rahisi.

“Mtu sasa hivi anaona hata akishikwa na hamu anaweza akaimaliza hana ile ya kujiuliza nimekaa muda mrefu bila kukutana na mwanamke/mwanaume kwakuwa anauwezo wa kupata kile anachokihitaji,” anasema Sheikh Mussa.

Anaongeza sababu nyingine ni changamoto za kiuchumi akisema vijana wengi wakipiga hesabu za gharama za kuoana na kipato chao wanaona hawawezi kuzimudu hivyo wanaamua kuachana nbazo lakini pia kuna changamoto ya kidini.

“Kwenye dini changamoto iliyopo ni kuwa watu hawaoni ndoa kama sehemu ya ibada wanaona kama jambo la starehe na endapo watu wataona ndoa katika mtazamo wa kiibada basi wanaliendea jambo hilo bila kusita,” anaeleza.


Mtaalamu wa ndoa

Mtaalamu wa masuala ya ndoa, Sadaka Gandi ameainisha sababu 12 zinazowasukuma wanandoa wengi hasa wachanga kushindwa kuendelea kuishi pamoja.

Gandi ambaye pia ni mwanasaikolojia anasema kila mtu ana sababu ya msingi linapokuja suala la wanandoa kutengana au kutalikiana, akieleza inawezekana mmoja kuliona suala ni zito kwake lakini mwingine akaliona la kawaida linaloweza kuvumilika.

Anasema vijana wengi wameingia kwenye ndoa kwa mashinikizo kama vile ya umri kusogea hasa anapoona wenzake wameoa au wameolewa na wana watoto.

“Ndoa inahitaji uwekezaji hasa wa hisia. Lakini walio wengi hawafanyi hilo kwani waliingia kwa matarajio kuwa akiolewa atapata hiki na kile. Mwingine anavyomuona rafiki yake baada ya kuolewa ana gari nzuri anadhani akiolewa naye itakua hivyo mwishowe alichokifuata hakioni.”anaeleza.

Gandi ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na afya anataja kukosekana kwa hisia baina ya wanandoa kuwa ni sababu mojawapo inayochangia migogoro ikiwemo vitendo vya ukatili baina ya wanandoa.

“Na hili niseme wanapokosa hisia mara nyingi wazazi huwa wanakuwa wabinafsi wanajifikiria wao wenyewe bila kujali kwamba muunganiko wetu tulipata watoto na hili niwasihi wale ambao wanashindwa kujibeba katika uhusiano yaani wewe kila kitu unasubiri ufanyiwe na mtu mwingine,” anasema.

Kukosekana kwa maisha ya Kimungu ni moja ya sababu anayoitaja Gandi kwamba imechangia wanandoa wengi kuachana na wengine kuogopa kuingia kwenye ndoa.

“Kuna kitu kinaitwa kujishtukia hasa kwa wanaume. Mtoto wa kiume anafika mahali kwa kuwa anashindwa kujisimamia au kusimamia maisha ya familia, anajiona kama amepoteza uanaume wake na hili ni baya,”anasema.

Gandi anaenda mbali na kueleza kuwa kitendo cha wasichana kuwezeshwa kielimu na kiuchumi, hali hiyo imechangia walio wengi kuingia kwenye ndoa wakiwa wanajimudu kimapato na wengine wasitake kuolewa kabisa.

“Pale ambapo mtoto wa kike aliwezeshwa tangu mdogo kila kitu anatajwa msichana, imewafanya vijana wengi wa kiume kukua wakiwa hawajui chochote waliachwa nyuma, hawa watu wawili wanapokutana na ikiwa huyu mwanaume akawa hajitambui , basi tatizo tayari,” anasisitiza.