Kutoka 'ombaomba' hadi kumiliki bajaji
Mkazi wa Jiji la Tanga, Mariam Siafu, mwenye ulemavu, akikagua moja ya bajaji zinazomilikiwa na kikundi chao cha Mother Disabled Group. Kikundi hicho kwa sasa kinamiliki bajaji nne zinazowawezesha wanachama kujipatia kipato na kujiendeleza kiuchumi. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Walioonekana kutegemea misaada leo ni waajiri na wafanyabiashara. Kupitia mikopo ya asilimia mbili ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, watu wenye ulemavu wamebadili maisha yao, wanamiliki bajaji, wameajiri madereva na sasa wana ndoto ya kumiliki daladala.
Tanga. Miaka michache iliyopita, Mariamu Siafu alikuwa miongoni mwa watu wenye ulemavu waliokuwa wakipambana kujikimu kwa shughuli ndogondogo za kila siku. Leo, maisha yake yamebadilika. Anamiliki bajaji, ameajiri madereva na sasa ana ndoto ya kupanua biashara kwa kumiliki daladala.
Mabadiliko hayo, anasema, yamewezekana kupitia mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa watu wenye ulemavu, fursa ambayo kwake imekuwa chachu ya kujitegemea kiuchumi na kurejesha heshima yake katika jamii.
Mariamu, mkazi wa Kata ya Chumbageni jijini Tanga, anasema safari ya mafanikio ilianza mwaka 2022 baada ya yeye na mwenzake mwenye ulemavu kuamua kutafuta suluhisho la changamoto za maisha badala ya kusubiri misaada.
“Nilikaa na mwenzangu tukakubaliana kuomba mkopo wa asilimia mbili ili tubadilishe maisha yetu. Tuliona ndiyo njia pekee ya kujikomboa kiuchumi,” anasema.
Kupitia mkopo wa kwanza wa Sh17 milioni walioupata mwaka huo, walinunua bajaji mbili na kufanikiwa kurejesha fedha zote ndani ya kipindi cha miaka miwili. Baada ya kuonyesha uaminifu katika marejesho, waliomba tena mkopo na kupatiwa Sh22 milioni, zilizowawezesha kununua bajaji nyingine.
Zainab Athuman, mkazi wa Kata ya Chumbageni, Jiji la Tanga na mmoja wa wanufaika wa mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa watu wenye ulemavu, akisaidiwa na dereva wa bajaji ya kikundi chao mara baada ya kukutana kwa ajili ya kukusanya mapato ya wiki. Picha na Mbonea Herman.
“Leo tunaendelea kurejesha mkopo wetu kama kawaida na biashara zinaendelea vizuri. Hii imetupa matumaini ya kufikia malengo makubwa zaidi,” anasema.
Kwa Mariamu, mtu mwenye ulemavu hapaswi kuendelea kutegemea msaada wa familia au jamii ikiwa fursa za kujikwamua zinapatikana.
Anasema wakati baadhi ya familia zina uwezo wa kuwasaidia ndugu zao wenye ulemavu, nyingine hazina uwezo huo, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kutumia fursa zilizopo kujijengea maisha bora.
“Unaweza kuwa na watoto wanaokutegemea. Huwezi kuendelea kusubiri kusaidiwa wakati Serikali imeweka mikopo isiyo na riba. Ukiamua kuitumia vizuri, unaweza kubadili maisha yako,” anasema.
Hata hivyo, anaamini bado kuna haja ya kuongeza kiwango cha fedha kinachotengwa kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu utaratibu wa kupata mikopo hiyo.
Kwa mujibu wake, baadhi ya walengwa hushindwa kujitokeza kwa kuhofia urasimu, ilhali changamoto kubwa ni kutokuzingatia masharti na elimu inayotolewa kuhusu usimamizi wa mikopo.
“Kama mtu anafuata taratibu na anarejesha kwa wakati, hakuna ugumu wa kupata mkopo mwingine. Elimu ndiyo muhimu zaidi,” anasema.
Mariamu anasema mafanikio ya kikundi chao cha Mother Disabled Group yamechangiwa pia na ushirikiano mzuri kati yao na maafisa maendeleo wa kata, ambao wamekuwa wakitoa ushauri na kufuatilia maendeleo ya biashara zao.
Anasema hata wanapokumbana na changamoto katika marejesho, wamekuwa wakishirikiana na maafisa hao kutafuta suluhisho badala ya kukwepa wajibu wao.
Zainab Athuman, mkazi wa Kata ya Chumbageni, Jiji la Tanga na mmoja wa wanufaika wa mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa watu wenye ulemavu, akisaidiwa na dereva wa bajaji ya kikundi chao mara baada ya kukutana kwa ajili ya kukusanya mapato ya wiki. Picha na Mbonea Herman.
Licha ya mafanikio hayo, Mariamu anasema bado watu wengi wenye ulemavu wanaendelea kuombaomba kutokana na kukosa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo.
Anasema baadhi yao hutumiwa kama chanzo cha mapato na watu wengine wasiokuwa na ulemavu, hali inayowafanya waendelee kuishi katika utegemezi badala ya kujitegemea.
“Wapo wanaotumiwa kama kitega uchumi. Fedha wanazokusanya huishia mikononi mwa watu wengine badala ya kuwasaidia kubadili maisha yao. Ndiyo maana elimu kuhusu mikopo ni muhimu,” anasema.
Kwa sasa, anasema maisha yao yamebadilika kwa kiwango kikubwa na wameanza kuheshimika tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Zamani tuliitwa ombaomba, leo tunaitwa mabosi. Tunatembea kifua mbele kwa sababu tuna biashara zetu na tunachangia maendeleo kama wananchi wengine,” anasema.
Malengo yao sasa ni kupanua biashara, kujenga nyumba na baadaye kuwekeza katika usafiri wa daladala.
“Tunataka kujenga nyumba zetu na kuacha kupanga. Tukifanikiwa, hatua inayofuata ni kumiliki daladala,” anasema.
Hata hivyo, anakiri kuwa biashara hiyo haikosi changamoto, hususan katika suala la marejesho ya mikopo kutokana na mabadiliko ya mapato ya madereva wanaowaajiri.
“Changamoto zipo, lakini tunajitahidi kuhakikisha tunalipa kwa wakati. Tunajua tusiporejesha, wengine hawatapewa nafasi ya kunufaika na mikopo hii,” anasema.
Mariamu anaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha watu wenye ulemavu kupitia mikopo hiyo na kuwataka walengwa wengine kuitumia kama daraja la kujikwamua kiuchumi.
Naye Zainab Athuman, ambaye pia ni mkazi wa Chumbageni na mnufaika wa mkopo huo, anasema safari yao ilianza baada ya kupata ushauri kutoka kwa aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, marehemu Kimaya.
Leo, kikundi chao kinamiliki bajaji nne na kinaendelea kupanua biashara.
“Kilichotufikisha hapa ni kujiamini. Tuliondoa hofu ya kushindwa na tukatumia fursa tuliyopewa. Tunawahimiza wengine wajitokeze kwa sababu mikopo hii inaweza kubadili maisha,” anasema.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga, Simon Mdende anasema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kujitegemea kiuchumi.
Anasema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Jiji la Tanga ilitoa jumla ya Sh5.13 bilioni kwa makundi hayo. Kati ya fedha hizo, vikundi 171 vya wanawake vilinufaika na Sh1.97 bilioni, vikundi 113 vya vijana vilipata Sh2.93 bilioni, huku vikundi 27 vya watu wenye ulemavu vikipewa zaidi ya Sh223 milioni.
Kwa Mdende, takwimu hizo zinaonyesha dhamira ya Serikali ya kuviwezesha makundi maalumu kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kuboresha maisha yao.
Kwa Mariamu na Zainab, mikopo hiyo haikuwa mtaji wa biashara pekee. Imekuwa daraja la kurejesha heshima, kuondoa utegemezi na kuthibitisha kuwa watu wenye ulemavu wakipewa fursa na kuaminiwa wanaweza kuwa waajiri, wawekezaji na wachangiaji muhimu wa uchumi wa taifa.