Kwa nini likizo muhimu kwa wanafunzi
Muktasari:
- Zimepita siku mbili tangu shule za sekondari na msingi nchini zifungwe, tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma kuwa wanafunzi hupata likizo Juni.
Zimepita siku mbili tangu shule za sekondari na msingi nchini zifungwe, tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma kuwa wanafunzi hupata likizo Juni.
Hata hivyo, baada ya Serikali kutangaza tarehe hizo za kufunga shule ili kazi ya Sensa ya Watu na Makazi ifanyike vyema, kuliibuka mjadala baada ya Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (Tamongosco), kutaka madarasa ya wanafunzi wakiwamo wa bweni, watakaofanya mtihani wa Taifa waruhusiwe kuendelea na masomo, kwa maana hiyo, wasipate likizo.
Awali, kabla ya likizo, Kamishna wa elimu nchini, Dk Lyabwene Mtahabwa aliwataka wamiliki wa shule hizo kuhakikisha wanafuata mwongozo wa mihula ambao Serikali ilishautuma mapema kwa kila shule za msingi na sekondari na wadhibiti ubora wa elimu nchini.
Hata hivyo, baada ya maombi ya wanachama kutaka wanafunzi waendelee na masoma, Mwenyekiti wa Tamongosco, Axwesso Mao alisema Ofisa Elimu Kiongozi aliagiza shule zikifungwa Julai 28 mwaka huu, wanafunzi wote waende nyumbani kwa likizo na hakuna ruhusa ya kubakiza wanafunzi wa madarasa ya mitihani shuleni.
“Kwa hiyo ndugu zangu, hayo ndiyo majibu ya maombi yenu, kwamba maombi yamekataliwa, nimejitahidi kumshawishi kamishna kutoa ahueni, lakini amekataa,” alisema Mao.
Kutokana na hilo, Mwananchi ilifanya mahojiano na Kamishna huyo wa elimu na baadhi ya wanasaikolojia ili kujua sababu ya Serikali kusisitiza likizo.
Dk Mtahabwa anasema ifike mahali wazazi na walimu wawahurumie watoto waweze kupumzika na kujumuika na familia zao kwa kuwa baadhi wamekuwa wakiwafundisha watoto kupita kiasi kwa malengo tu wapate ‘A’ bila kujua namna gani wanawaathiri kimakuzi.
“Serikali ilipopanga ratiba za kufunga shule na kupeleka mwongozo na nyaraka kwenye shule, haikukosea, kuna sababu zake kimakuzi, afya ya mtoto na kisaikolojia, kijamii na kihisia; hivyo naomba wazazi na wamiliki wa shule kuwa na desturi ya kuheshimu miongozo hiyo,” anasema Dk Mtahabwa.
Pia, anasema jingine lililochangia likizo ya Juni mwaka huu kusogezwa hadi mwishoni mwa Julai ni katika kuheshimu shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi inayoenda kutekelezwa kuanzia Agosti 23.
Wazazi, wanafunzi wafunguka
Baadhi ya wazazi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu likizo kwa wanafunzi wenye mitihani ya Taifa, wakisema ni bora watoto wabaki shule kwa kuwa wakiwa nyumbani kuna usimamizi mdogo wa walezi na wazazi kuhakikisha wanajisomea.
“Maisha ya wazazi wengi ni wale wa kutoka asubuhi kurudi usiku katika kutafuta, hivyo kwa kipindi chote mtoto anakuwa mwenyewe, huwezi kujua kasoma au la, na anaweza kukudanganya anasoma akikuona umerudi, hii ndiyo moja ya sababu pia tunaamua kuwapeleka shule za bweni, hivyo ni bora wabaki shule,” anasema Gervas Mmasi.
Mzazi mwingine, Prisca anasema afadhali mtoto wake apumzike, kwa kuwa amekuwa akiamka asubuhi saa 11:00 kila siku kwenda shule kutokana na kuwa na mitihani ya saa 12 kabla ya kuanza ratiba ya masomo ya darasani na hutoka saa 12:00 jioni, kwa hiyo kutokana na ratiba hiyo ni wazi mtoto wake atakuwa amechoka.
Agripina Tesha anasema wazazi wasikubali watoto watumike kama mitaji ya kuzinufaisha shule, kwa kuwa kusoma sana sio kwamba ni kigezo cha kufaulu na kubainisha kuwa baadhi ya shule hizo zinawatumia watoto kuwakaririsha ili wapate A, malengo yao yakiwa ni kupata wanafunzi wa kujiunga.
Wanasaikolojia
Mshauri Nasihi wa Saikolojia kutoka Taasisi ya Health Tanzania, Bosco Bosco anasema kuna madhara ya mtoto kutokwenda likizo, hasa wa bweni kwa kuwa wanashindwa kutengeneza ukaribu na wazazi, jambo ambalo baadaye linaweza kusababisha asione umuhimu wao, hasa anapokuwa mkubwa kwa kuwa hakupata mapenzi yao.
Anasema pia watoto wanaweza kupata ugonjwa aliouta ‘homesicking’, jambo linaloweza kumsababishia kuumwa kichwa mara kwa mara na anapokwenda kupimwa hakutwi na ugonjwa wowote.
“Pia wakati mwingine mtoto hujikuta mikono ikimuuma hadi kufika hatua ya kushindwa kuandika, kuharisha na kutapika nayo ni magonjwa yanayoweza kutokea, kutokana na kukosa huko likizo,” anasema Bosco.
Mshauri huyo anasema mtoto anaweza kudumaa katika eneo moja la kusoma tu na kujikuta anashindwa kuonyesha kipaji chake kingine, hivyo anapoingia uraiani na kushindwa kupata kile alichosomea anashindwa kuchagua upande wa pili wa maisha.
Hata hivyo, Bosco anasema watoto wa aina hiyo ndio wanashindwa kuja kuwa wazazi bora wa kulea familia kwa kuwa yeye alikuwa hasaidiwi.
Mwanasaikolojia Antony Mhando, anasema endapo mtoto anapata muda wa likizo humsaidia katika afya ya akili kwa kuwa hukutana na mambo mapya yatakayoweza kuifanya akili yake kuwa imara na bora zaidi.
“Kama mwanafunzi hatokuwa na muda wa kupumzika kwa masomo, anaweza akawa na wakati mgumu sana kufanya vitu vyake binafsi,” anasema Mhando.
Pia, anasema afya ya akili haiwezi kujulikana kwa haraka, hivyo ni vizuri wanafunzi wapewe likizo ya masomo itakayowasaidia kuimarisha afya hiyo.
Mwanasaikolojia Charles Nduku anasema kusoma kwa muda mrefu huweza kutengeneza msongo wa mawazo, hivyo mwanafunzi kupewa likizo humsaidia kupumzisha akili.
“Kujiandaa sana huweza kutengeneza woga kuwa kitu anachokutana nacho ni kikubwa, hivyo ni vizuri kupumzika,” anasema mwanasaikolojia Nduku.
Ratiba za mitihani
Kwa mujibu wa Baraza la Mtihani Nchini Tanzania (Nacte), mtihani wa darasa la saba utafanyika Oktoba 5 na 6 na wa kidato cha nne ni Oktoba 26 na 27.
Wakati mtihani wa kidato cha pili utafanyika Oktoba 31 hadi Novemba 10, huku ule wa kidato cha nne ukitarajiwa kufanyika Novemba 14 hadi Desemba 1.
Mihula ya kufunga hii hapa
Kwa muhula wa kwanza 2022, shule zimefungwa Julai 28 na zitafunguliwa Septemba 5 mwaka huu, robo muhula wa pili, zitafungwa Septemba 30 na zitafunguliwa Oktoba 10, wakati likizo ya muhula wa pili, shule zitafungwa Desemba 8 na zitafunguliwa Januari.