Kwa nini mashahidi 11 kesi ya kina Mbowe hawakuonekana?

Muktasari:

Wakati kesho Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitarajiwa kuamua kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu ama la katika tuhuma za ugaidi zinazowakabili, wataalamu wa masuala ya sheria wamezungumziakutotokea kwa mashahidi 11 wa upande wa mashtaka kutoa usahidi wao katika kesi hiyo.

Dar es Salaam. Wakati kesho Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitarajiwa kuamua kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu ama la katika tuhuma za ugaidi zinazowakabili, wataalamu wa masuala ya sheria wamezungumziakutotokea kwa mashahidi 11 wa upande wa mashtaka kutoa usahidi wao katika kesi hiyo.

Pamoja na mambo mengine wataalamu hao wamesema upande wa mashtaka haulazimiki kuwaita mashahidi wote inaowaorodhesha bali huwa na uwezo wa kuamua nani aitwe na nani asiitwe kutoa ushahidi kulingana na tathmini ya ushahidi uliokwishatolewa.

Ufafanuzi huo umekuja kufuatia mjadala mkali unaoendelea mitandaoni kutokana na uamuzi wa Serikali kufunga ushahidi wake juzi ikiwa imewaita mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imewaorodhesha awali kwamba, wangefika mahakamani hapo kueleza wanachokijua kuhusu tuhuma zinazoendelea kusikilizwa.

Pamoja na mambo mengine, wadau wanaoifuatilia kesi hiyo wanasema Serikali imelazimika kufunga ushahidi baada ya kuwaita mashahidi 13 badala ya 24.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili jana walieleza kuwa baadhi ya mashahidi wanaokuwa wametajwa na upande wowote kwenye kesi, kutokuitwa mahakamani ni jambo la kawaida kwa kuwa kesi haithibitishwi kwa wingi wa mashahidi bali kwa ubora wa ushahidi uliowasilishwa.

Wakili wa Kujitegemea, Timon Vitalis alisema shahidi hawezi kugoma kwenda mahakamani kutoa ushahidi na ikitokea hivyo basi upande wa mashtaka unaweza kuomba hati ya kumkamata na kumfikisha mahakamani shahidi huyo kwa nguvu.

“Shahidi yeyote anakuwa compellable (anaweza kulazimishwa) ukiacha mke au mume, yaani kama shahidi ni mke au mume wa mshtakiwa. Shahidi huyo halazimiki kwenda kutoa ushahidi dhidi ya mume wake au mkewe. Mashahidi wengine waliobaki ni compellable,” alisema Wakili Vitalis na kuongeza kuwa:

“Kwa hiyo hakuna shahidi anaweza kugoma kwa sababu anakwenda kwa wito wa mahakama kutoa ushahidi, kwa kupelekewa summons (hati ya wito wa kufika mahakamani). Asipotii summons inatolewa hati ya kumkamata ili kumlazimisha kufika mahakamani.”

Wakili Vitalis alifafanua zaidi kuwa mashahidi wa upande wa Jamhuri wanakuwa tayari wameandika maelezo yao kuhusu kesi husika hata upande wa utetezi ambao mashahidi wake wanakuwa hawajaandika maelezo lakini, wanaweza kuiomba mahakama ikatoa wito kwa shahidi yeyote.

Alisisitiza kuwa shahidi wa upande wowote ikithibitika alipelekewa wito wa kwenda mahakamani lakini hakutokea basi inatolewa hati ya kumkamata kwa kutokutii wito wa mahakama.

“Kwa hiyo suala la kutoa ushahidi mahakamani ni agizo, unatii amri ya mahakama. Huwezi ukasema eti amekugomea, anakuwa anaigomea mahakama kwa sababu wito ule ni wa mahakama,” alisema Vitalis.

Kuhusu idadi ya mashahidi, Wakili Vitalis alisema Jamhuri ina uwezo wa kuachana na baadhi ya mashahidi iliopanga kuwatumia hata kuruhusu upande wa utetezi kuwatumia kama utapenda kufanya hivyo katika kesi husika inayoendelea mahakamani.

“Jamhuri ina uwezo wa ku- abandon, kuwa mashahidi wengine tuliokuwa tumepanga kuwatumia tunaachana nao. Na mara nyingi kwa mwendesha mashtaka ambaye yuko makini hawezi kuishia kusema tu kuwa ninawa-abandon, atasema kuwa ninawa-offer (ninawatoa) kwa upande wa utetezi wakipenda kuwatumia wawatumie,” alisema.

Alifafanua zaidi kuwa sababu ya kufanya hivyo ni kuepuka kuifanya mahakama ione kuna jambo linalopangwa kufichwa.

“Kumbuka maelezo yao tayari mahakama inakuwa inayo kwa sababu kuna wakati inaweza kuonekana kutokuletwa kwa shahidi aliyetajwa kunalenga kuficha jambo fulani, huenda unaamini akija kuongea ataongea vitu ambavyo vitakwenda kinyume cha kile unachotaka kukithibitisha.

“Sasa ili kuwa salama unasema ninawa-offer kwa sababu hakuna kinachozuia initially (awali) shahidi ambaye alikuwa amekusudiwa kuitwa na upande wa mashtaka, kutumiwa na upande wa utetezi.”

Naye wakili wa kujitegemea, Nahodha Bendera alisema mwanasheria yeyote anapoona mashahidi aliowaita wamekidhi haja ya kesi anayoishughulikia basi hana haja ya kuita mashahidi wengine kuja kuendelea kurudia kilichosemwa na waliotangulia.

“Kwa hiyo Serikali inaposema hawa wametosha ina maana imaridhika na ushahidi walioutoa ambao imejiridhisha kuwa umetosha kukidhi kuthibitisha tuhuma zilizopo. Lakini, hiyo ya kusema kwamba wamewagomea hakuna hilo,” alisema wakili Bendera na kuongeza:

“Mtu yeyote akipewa summons ya kufika mahakamani lazima aende lakini kama mwendesha mashtaka ameona hamna haja ya kuwapa summons basi hajawaita. Kwa hiyo watu wajue ule uhuru alio nao mwendesha mashtaka ya kuleta mashahidi anaoona wanaweza wakasaidia upande wa kesi yake.”

Hoja hizo za mawakili Vitalis na Bendera ziliungwa mkono pia na wakili Juma Nassoro, ambaye pia alisema kuwa mwendesha mashtaka ndiye anajua aina ya ushahidi anaioutaka na kwamba hana haja ya kujaza mashahidi pale ambapo anakuwa ameridhika na ushahidi wake aliokwishautoa.

Wakili Nassoro alisisitiza kuwa wakati mwingine kuna mashahidi ushahidi wao unakuwa unafanana na kwamba katika hali ni busara kwa mwendesha mashtaka kuamua kuachana nao.


Kesi nyingine

Hii si kesi ya kwanza kwa upande wa mashtaka kupunguza idadi ya mashahidi tofauti na waliotajwa awali kwamba wangefika kortini.

Baadhi ya kesi kubwa ambazo Serikali ilipungunza kwa kiwango kikubwa mashahidi wake ni ile ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mehenge mkoani Morogoro.

Ni kesi iliyokuwa ikiwakabili maofisa na askari polisi 13 akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe.

Katika kesi hiyo Serikali iliorodhesha mashahidi 85 lakini ilifunga ushahidi baada ya mashahidi 39 tu kufika mahakamani kueleza wanachokijua kuhusu mauaji hayo.

Kesi nyingine ni ya utoroshaji wa makontena kutoka bandari kavu bila kulipiwa kodi iliyokuwa ikiwakabili maofisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), watumishi wa Bandari kavu ya Azam na wafanyabiashara iliyokuwa na mashahidi zaidi ya 80 lakini Serikali iliwatumia mashahidi 38 tu.

Kwenye kesi ya Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza), Adamu Hassan Kasekwa almaarufu kama Adamoo (wa pili) na Mohamed Abdillah Ling’wenya (wa tatu).

Bwire, Kasekwa na Ling’wenya walikuwa askari wa (JWTZ) wa kikosi maalumu, maarufu kama kikosi cha makomandoo.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Joachim Tiganga katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.