Hatma ya kina Mbowe kujulikana Ijumaa

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (mwenye miwani) akiwa na watuhumiwa wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi, wakipelekwa katika chumba cha Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema Ijumaa Februari 18, 2022 itatoa uamuzi iwapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu au la katika kesi ya ugaidi inayowakabili.

Dar es Salaam.  Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema Ijumaa Februari 18, 2022 itatoa uamuzi iwapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu au la katika kesi ya ugaidi inayowakabili.

Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo amesema hayo leo Jumanne Februari 15, 2022 baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahaka kuwa wamefunga kesi hiyo kwa shahidi wa 13 kuhitimisha ushahidi wake.

Shahidi huyo wa 13 wa upande wa mashtaka ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila amemaliza kutoa ushahidi baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.

Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert Kidando aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba ione kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

“Baada ya ushahidi wa shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu 41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande wetu tunafunga kesi hii” amesema Wakili Kidando

Hata hivyo, baada ya upande wa mashtaka kutoa ombe hilo, upande wa utetezi kupitia Wakili Peter Kibatala umeomba kupewa nafasi ya kufanya mawasiliano ya mdomo pamoja na kupewa mwenendo wa kesi.

“Baada ya upande wa mashtaka kufunga kupitia kifungu hicho cha 41 tunaomba Mahakama hii itupe nafasi ya kufanya mawasilisho ya mwisho lakini pia tuna maombi mawili ombi la kwanza Mahakama itupe mwenendo wa kesi lakini pili tupewe nafasi ya kufanya mawasilisho ya mwisho oral” amesema Kibatala.

Kabla ya kujibu maombi hayo, Jaji Joachim Tiganga aliwaita mawakili wa pande zote kujadiliana kwa dakika kumi.

“Hadi leo PS wangu (msaidizi) ameshachapa kurasa 1,400 nikichanganya za jana na leo zinaweza kufika 1,600 nilikuwa nafikiria hapa nadhani nipatiwe dakika kumi tukajadiliane” amesema Jaji Tiganga

Baada ya muda mfupi Mahakama ilirejea na Jaji Tiganga akisema kuwa Mahakama hiyo itatoa uamuzi Ijumaa wa kuwa washtakiwa hao wana kesi ya kujibu au la.

“Baada ya kusikiliza na kupitia hoja za pande zote mbili na kuzingatia kifungu cha 41 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Mahakama hii itatoa uamuzi Februari 18, 2022 kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la saa nane mchana na washtakiwa mtaaendelea kubaki chini ya uangalizi wa Magereza” amesema Jaji Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.




Soma hapa kilichojiri mahakamani leo


Jaji Joachim Tiganga ameshaingia mahakamani na mawakili wa pande zote wameshajitambulisha.

 Jaji anamkumbusha shahidi kuwa bado yuko chini ya kiapo.

Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala anaanza kumuhojishahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila


Wakili Kibatala: Unafahamu katika repoti hiyo mlileta wenyewe mahakamani na mlisema mlipeleka sampuli 15 kutoka kwa Kasekwa


Shahidi: Sio kweli


Wakili: Hicho kidaftari mliambiwa kimeletwa hapa mahakamani kama kielelezo


Shahidi: Sikuambiwa


Wakili: Unafahamu majengo yana anuani


Shahidi: Nafahamu


Wakili: Makao Makuu ya Polisi Dodoma na ndogo nazo zina anuani


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ulisema kwamaba ulitembelea vituo mbalimbali vya mafuta


Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Vituo hivyo inasemekana ndio watuhumiwa walipanga kufanaya uhalifu


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ni vituo gani ulisema Morocco na vingine ni vipi


Shahidi: Puma Mivinjeni, Big born Kariakoo, Puma Sinza


Wakili: Ulimwambia Jaji viko ploti namba ngapi


Shahidi: Sikumwambia


Wakili: Kituo cha Puma Sinza ulimwambia Jaji kiko katika makutano ya barabara ipi?


Shahidi: Sikumwambia hakukuwa na umuhimu


Wakili: Big born Kariakoo ulimwambia Jaji Kiko barabara gani


Shahidi: Nilimwambia barabara ya Msimbazi


Wakili: Ulimwambia Jaji ni tarehe ngapi na muda gani ulitembelea vituo hivyo


Shahidi: Nilisema ni tarehe 14


Wakili: Na ni ushahidi wako ulitembelea vituo vyote siku moja


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Na kwenye maelezo yako umevifafanua hivyo vituo


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Kwahiyo nikiyaomba tutakuta huo ufafanuzi


Shahidi: Ndio


Wakili: Mheshimiwa Jaji nadhani nimejenga msingi wa kutosha naomba upande wa mashtka wanipe nakala halisi ya maelezo ya shahidi.


Wakili: Sasa shahidi yasome kwa nguvu kwa mujibu sheria.


Wakili: Unajua maana ya details


Shahidi: Fafanua


Wakili: Nikianza na kituo cha mafuta Puma Mivinjeni katika maelezo yako kuna mahali umetaja Kilwa Road


Shahidi: Hakuna lakini ndio maana nimekuja kutoa ushahidi hapa


Wakili: Kituo cha mafuta Big born kuna sehemu umetaja barabara ya Msimbazi


Wakili: Hakuna ndio maana nimekuja kutoa ushahidi hapa mahakamani haiwezekani kuandika kila kitu


Wakili: Kituo cha Sinza umefafanua kiko barabara gani


Shahidi: Sijafafanua


Wakili: We si shahidi ndio maana umekuja kutoa ushahidi hapa mahakamani

Shahidi: Ndio


Wakili: Una matatizo na maelezo yako Jaji akiyaona kama kielelezo cha utetezi


Shahidi: Hapana


Wakili: Mheshimiwa Jaji naomba yapokelewe kama kielelezo cha utetezi

Wakili Kidando: Hatuna pingamizi

Mahakama imepokea maelezo ya shahidi Tumaini Swila kama kielelezo cha tano cha upande wa utetezi.

Wakili: Wewe kama mpelelezi ulimaanisha Freeman Mbowe kama alikuwa hana nia ovu angeenda kumtafuta Halfan Bwire


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ni sheria ipi inamruhusu Freeman Mbowe kama mtu maaarufu alitakiwa kwenda kituoni kumtafuta


Shahidi: Hakuna


Wakili: Ni nani mlimpa taarifa ya kukamatwa na Halfan Bwire


Shahidi: Mke wake baada ya kwenda kupekuliwa nyumbani kwake


Wakili: Unajua Freeman Mbowe alituma mawakili kwenda kumuwakilisha Bwire


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Unafahamu wakati kesi inaendelea upande wa mashtaka walikuwa wakifahamisha kuwa upelelezi haujakamilika


Shahidi: Nafahamu


Wakili: Na wewe ndio uliiarifu mahakama washtakiwa watatu ushahidi ulikuwa hauwagusi ndio maana wakakachiwa


Shahidi: Ndio


Wakili: Freeman alikuwa anafuatiliwa na kuangaliwa kwa jicho la karibu


Shahidi: Ndio


Wakili: Kwa jicho la kiupelelezi mlikuwa mnafahamu Freeman Mbowe


Shahidi: Alichoniambia Ramadan Kingai kuwa Mbowe anafwatiliwa kwa karibu


Wakili: Unafahamu kipindi mnamtafuta Bwire alikuwa anaendelea na shughuli zake za kawaida


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Umeandika kwenye maelezo yako siku anakamatwa alikuwa ametoka wapi


Shahidi: Kazini kwake kwa Freeman Mbowe

Wakili: Mlikuwa mnafuatilia movement za Mbowe ndani na nje ya nchi zikoje


Shahidi: Nimesema sifahamu Kingai ndio alikuwa anafuatiliwa


Wakili: Unafahamu baada ya Uchaguzi Mkuu Mbowe na wenzake walikamatwa na faili lake lilikuwa Osterbay Polisi


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Unafahamu moja ya masharti ya dhamana alikuwa haruhusiwi kutoka nje ya nchi hadi apate kibali polisi


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Unafahamu kibali cha kutoka nje ya nchi kilitolewa na Jeshi la Polisi na hata aliporejea nchini hakukamatwa


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Uliwahi kuona taarifa kwenye faili la upelelezi likisema Freeman Mbowe amekimbia nchini


Shahidi: Sikuwahi kuona


Wakili: Washtakiwa wengine walioachiwa unafahamu walifanya nini hadi wakaunganishwa kwenye kesi hii


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Unasema waliachiwa baada ya mwaka mmoja


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Na Mbowe toka akamatwe hata mwaka haujaisha


Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Unafahamu Kissy Hotel ilipo


Shahidi: Kuna hapa Dar es Salaam na Moshi


Wakili: Ni ipi iliyopiga kengele kwenye shughuli zenu za upelelezi


Shahidi: Moshi


Wakili: Ulimwambia Jaji kama uliwahi kwenda kuitembelea


Shahidi: Hakukuwa na umuhimu

Wakili: Wakati unapokea simu kutoka maabara ya upelelezi uliwahi kufafanuliwa kwanini simu ilikuwa na chaji kwa kipindi cha miaka miwili


Shahidi: Hapana


Wakili: Wewe binafsi uliwahi kufahamu ni kwanini simu ilikuwa na chaji kwa takribani miaka kumi


Shahidi: Sifahamu zilikuwa zimefungwa


Wakili: Wakati unampigia Urio kuja kutoa maelezo unafahamu alikuwa wapi.


Shahidi: Morogoro


Wakili: Jeshi la Polisi lilimpa nauli


Shahidi: Sifahamu

Wakili: Unaweza kumwambia Jaji, Bwire alikiwa akalipue vituo vipi?


Shahidi: Vituo vyote kwa kuwa yeye ndio alikuwa na kidaftari chenye michoro


Wakili: Nionyeshe kwenye hayo maelezo ni wapi pameandikwa Bwire alikuwa alipue vituo vyote


Shahidi: Anasoma maelezo ya Adam Kasekwa


Wakili: Kwa mujibu wako hayo maelezo yanaonyesha Bwire alikuwa alipue vituo vya mafuta


Unapoataka kulipua wote wanalipua kwa wakati mmoja au kila mtu anafanya jukumu flani


Shahidi: Inategemea


Wakili: Kwa upelelezi wako katika mpango wa kulipua Adam Kasekwa alikuwa afanye kazi ipi


Shahidi: Katika hayo maelezo yao hawajeleza


Wakili: Katika maelezo hayo ulithibitisha mshtakiwa wa pili na watatu walishiriki mapokezi ya Tundu Lissu Airport


Shahidi: Nilithibitisha kupitia maelezo yao

Wakili: Baada ya kumpokea Lissu kati ya Julai 27 mpaka 31, waliendelea kufanya kitendo gani cha uhalifu!

Shahidi: Kwa maana amabyo unaitaka hakuna maelezo hayo.


Wakili: Sasa shahidi twende kwenye maelezo ya Ling'wenya, soma.

Shahidi anasoma maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Ling'wenya kisha wakili Kibatala anauliza:

Wakili: Uli-confirm kuwa katika majadiliano hayo walizungumza mambo ya siasa?


Shahidi: Katika maelezo yake ameeleza Ling'wenya lakini huyu mwingine hakusema.


Wakili: Wewe kama mpelelezi uli-confirm watu wa Mbowe (jimboni) wanapigwa na yeye mwenyewe anatukanwa?


Shahidi: Nilitumia maelezo


Wakili: Uliwahi ku-confirm Mbowe aliwahi kufikisha malalamiko yake kwa Rais kuhusu vitendo vya Sabaya?


Shahidi: Hapana


Wakili: Pia amesema malalamiko hayo aliwahi kuyafikisha kwa IGP kwa kuwa ni bosi wako uliwahi kumuuliza kuhusu malalamiko hayo?


Shahidi: Hapana.


Wakili: Ni sahihi kwa mujibu wa maelezo hayo kuna tarehe ambayo Ling'wenya haikumbuki walikutana na Mbowe Dar es Salaam na wikajadiliana kuhusu malipo yao kwa mwezi mshahara wa Sh1.3 milioni?


Shahidi: Kwa mujjbu wa maelezo ndivyo inayoonekana lakini haiondoi dhana


Wakili: Na ni sahii kwa mujibu wa maelezo hayo suala la mishahara Mbowe alilikabidhi kwa katibu wake, ni sahihi?


Shahidi: Rudia hapo


Wakili: Ngoja nisome (maelezo) kisha anarudia swali lake


Shahidi: Ambayo hayakutekelezwa (maelekezo ya mshahara)


Wakili: Ambaye hakutekeleza nani, Mbowe au katibu wake?


Shahidi: Ndivyo ilivyo kwenye maelezo


Jaji: Ameshakujibu hilo swali


Wakili: Ni sahihi siku hiyo walikwenda kumpokea Lissu?


Shahidi: Kwa mujibu wa maelezo


Wakili: Na kwamba walitokea kwa Mbowe?


Shahidi: Ni sahihi kwa mujibu wa maelezo


Wakili: Kwamba baada ya kumpokea Lissu walikwenda mpaka ofisi za Chadema?


Shahidi: Ni sahihi kwa mujibu wa maelezo


Wakili: Kwamba baada ya hapo walienda kwa Mbowe?


Shahidi: Ni sahihi kwa mujibu wa maelezo


Wakili: Unafamu shahidi kwamba suruali za khaki ambazo Ling'wenya anazizungumzia ni vazi rasmi wanachama?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Swali langu la mwisho kwako, Wewe kama mpelelezi kesi hii tangu ifunguliwe ilishakuwa na washtakiwa saba, ni sahihi?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Kwa ufahamu wako kama mpelelezi kuna mshtakiwa yeyote ambaye alishawahi kuhukumiwa kifungo?


Shahidi: Hakuna

Sasa upande wa mashtaka wanamhoji shahidi kutoa ufafanuzi wa hoja za maswali ya utetezi.


Mwendesha Mashtaka-Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando


Wakili: Shahidi umeulizwa kuhusu maelezo ya onyo ya Adamu Kasekwa, kuhusiana na suala la ulipuaji vituo vya mafuta, kuwa ni majukumu yapi mahsusi ya mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu kwa nini ulikuwa unasema hivyo, pitia kwanza hayo maelezo? Kwa nini ulisema Bwire ilikuwa alipue vituo vyote?


Shahidi: Kwanza amekamatwa na kidaftari cha michoro ya vituo vya mafuta. Naye alikuwa kwenye njama hizo za kulipua vituo vya mafuta. Hivyo nilikuwa namaanisha hivyo kwa maelezo haya.


Wakili: Poa uliulizwa jukumu mahsusi la Adamu Kasekwa ukasema hayajaelezwa lakini ilikuwa ni jukumu la pamoja kwa nini?


Shahidi: Kulingana na maelezo hayo Adamu Hassan Kasekwa alikuwa ni miongoni pamoja na watuhumiwa wengine kulingana na kidaftari alichokutwa nacho Halfan Bwire Hassan

Wakili: Pia kwenye maelezo ya Ling'wenya, uliulizwa kuhusiana na maongezi ya mshahra wa Sh1.3 milioni na kwamba maelekezo ya kukamilisha, kuna majukumu aliachiwa katibu wake (Mbowe), ukasema jambo hilo halikutekelezwa, hebu ifafanulie Mahakama.


Shahidi: Nilikuwa namaanisha kuwa haya makubaliano ya kuajiriwa hayakutekelezwa kwa hiyo hilo suala la kuajiriwa halikuwepo bali walitumika kama wahalifu na wao walikubali kushawishiwa nao wakaingia kwenye uhalifu.

Wakili: Pia katika kielelezo hochohicho cha 13 (maelezo ya onyo ya Ling'wenya) kuwa uli-confirm kama Freeman Mbowe alifikisha malalamiko yake kwa Rais na kwa IGP kuhusu Sabaya, kwa nini haukufuatilia?

Shahidi: Sikufuatilia kwa sababu mimi nilikuwa sihusiki na malalamiko hayo na sijui kama kweli aliripoti au la.


Wakili: Wakati unaulizwa zile simu tatu za Urio ulizozijaza tarehe 13 kama ulijaza fomu tarehe 13 mwezi wa 8 hukumuita tena Luteni Urio arudi wakati unajaza?


Shahidi: Sikuona umuhimu wa kumuita kwa sababu tulishakabidhiana na wakati wa kujaza fomu hizo yeye hawajibiki. Kwa hiyo nilizijaza na askari.


Wakili: Uliulizwa swali kuhusu Keeys Hotel ukasema ni Keey Hotel ya Moshi kutokana na ushahidi wa Kaaya na kama kuna hatua yoyote ya kiupelelezi ukasema hakukuwa na umuhimu, kwa sababu gani upisema hivyo?


Shahidi: Kwa sababu tayari Kaaya kwenye ushahidi wake mwenyewe alishasema walikutana hapo na Mbowe kisha wakaenda Aishi Hotel ambako walipeana namba za Sabaya.


Wakili Kibatala anapinga majibu hayo kuwa shahidi anakwenda mbali hata kwa majibu ya swali ambalo hawakumuuliza na kwamba wanaleta kitu kipya


Wakili Kidando anasisistiza kuwa wako sawa, lakini baada ya Kibatala kusisitiza kuwa ni jambo jipya Kidando anaamua kuondoa sehemu ya mwisho ya jibu la shahidi.


Wakili: Shahidi pia ulikuwa unaulizwa katika nafasi yako kama ulijua Mbowe alitaka kutoroka ukasema halikuwa jukumu lako kwa nini ulisema hivyo?


Shahidi: Nilisema hivyo kwa sababu taarifa za kufuatilia mwenendo wa Freeman Mbowe nilijulishwa na Afande Kingai, ila hakunijulisha kuwa nani anamfuatilia. Na niliposema sikuwa na taarifa za mtuhumiwa kutoroka ni kweli sikusikia.


Wakili: Mheshimiwa Jaji kwa sababu ni saa saba kasoro dakika mbili, tunaomba ahirisho fupi ili tuweze kuendelea baadaye.


Kibatala: Hatuna pingamizi


Jaji: Basi tunapata ahirisho kama dakika 45 tutarudi kuendelea.

Mahakama imerejea kwaajili ya upande wa mashtaka kuendelea kumuhoji shahidi.


Mawakili wa pande zote wako tayari kuendelea

Wakili wa Serikali Robert Kidando: Uliulizwa swali kuhusiana na details ikiwemo plot namba ukaseama sio muhimu ilikuwa unamaanisha nini?


Shahidi: Sio lazima kuweka details kwenye maelezo kwa kuwa ushahidi mwingne nimeutoa hapa mahakamani.

Wakili: Uliulizwa kuhusiana na mtu anaitwa Justin Kaaya kuhusu kushiriki vikao vya ugaidi na wewe ukaseama alishiriki bila kujua malengo, ulikuwa unamaanisha nini


Shahidi: Justin Kaaya alishiriki kikao bila kujua malengo yake wakati Freeman Mbowe anamuomba majina na sehemu anakopenda kuitembelea aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Wakili: Uliulizwa maswali kadhaa kuhusiana na taarifa aliyotoa Luteni Urio na washtakiwa kukamatwa, hebu ifafanulie Mahakama ni kwanini toka taarifa itolewe hadi washtakiwa wakakatwe palipita muda.


Shahidi: Nilikuwa namaanisha kwamaba taarifa ambazo Luteni Urio alituambia aliwaagiza mshtakiwa namba moja hadi tatu kumkusanyia taarifa kutoka kwa mshtakiwa namba nne lakini hawakufanya hivyo hadi alipofuatilia mwenyewe.


Wakili: Hebu ielezee Mahakama kwa nini Police fomu namba 145 inaonyesha Kituo cha Polisi Kati na Police Central.


Wakili John Malla: Mheshimiwa Jaji hiyo ni new fact itahitaji cross examination.


Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji hilo pingamizi halina mashiko.


Jaji: Jibu lilikuwa ni nini.


Anapotoa maelezo ni kitu kipya akileta maelezo inaweza kupelekea kukawa na cross examination.


Wakili Kidando: Hebu ifafanulie pale uliposema uchunguzi umekamilika ulikuwa unamaanisha nini kwa kuwa upelelezi wa shauri hili ulikamilika tangu tarehe 18/7/2021


Shahidi: Uchunguzi ulikamilika tarehe 18/7/2021 na ile taarifa niliyosema nimepokea kuhusu kukamilisha kwa upelelezi wiki iliyopita kuna baadhi ya uchunguzi wa vielelezo ulikamila katika maabara ya uchunguzi wa kisayansi.

Wakili: Uliulizwa maswali kadhaa hasa pale wakati wa upokeaji taarifa kutoka kwa Denis Urio na ukasema mtu aliyeipokea ni Afande DCI wakati huo Robert Boaz.

Ukaulizwa katika mazingira hayo DCI alitakiwa amuachie msaidizi wake ukasema sio kweli ulikuwa unamaanisha nini.


Shahidi: DCI hakutakiwa kumuachia msaidizi wake kwa kuwa taarifa ikitoka kwenye vyanzo vingine na kwenda kwa DCI ambaye ndio mwenye jukumu la kusimamia makosa ya jinai nchini.


Wakili: Uliulizwa pia ni lini DCI Robert Boaz aliandika maelezo na ukaulizwa kwanini kesi hii isichukuliwe ni ya kutunga hebu fafanua kwanini ulisema sio ya kutunga.


Shahidi: Sio ya kutunga kwa sababu kesi ilifunguliwa kwa kufuata utaratibu kwa kuwa jalada lilifunguliwa, washtakiwa wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Wakili: Ulionyeshwa kielelezo namba nne na tano ambacho ni risasi ukaonyeshwa kule nyuma namba ukasema hazina umuhimu hebu ieleze mahakama ulikuwa unamaanisha nini.


Shahidi: Risasi huwa zinafanana


Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji hii new fact.


Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji tunaomba kuliondoa hilo swali na kuendelea na swali lingine.

Wakili Kidando: Uliulizwa swali katika maelezo ya Denis Urio kama kuna mahali aliandika au alieleza kuwa alimwambia Mbowe usitumie namba yake binafsi au ya wasaidizi wake hebu fafanua maana yake.


Shahidi: Kumzuia asitumie namba yake ya simu ilikuwa ni kukusanya taarifa kutoka kwa mshtakiwa wa nne ili asione kuwa hayuko naye.


Wakili wa Serikali Pius Hilla naye anamhoji shahidi.


Wakili Hilla: Ifafanulie Mahakama ni kwa namna gani mtuhumiwa namba moja hadi tatu hawakuwa na ufahamu.


Shahidi: Mtuhumiwa namaba moja hadi tatu hawakuwa na ufahamu wa kupanga njama kwa kuwa walitumwa kukusanya taarifa lakini baada ya kukutana na mtuhumiwa namba nne wakakubali kushawishika na kuingia kwenye vitendo vya kihalifu na kupelekea kukamatwa.


Wakili: Unakumbuka pia Uliulizwa kuhusu uhamisho wako na ukaambiwa ni mkakati hebu fafanua.


Shahidi: Uhamisho wangu ulikuwa ni uhamisho wa kawaida wa kazi.


Wakili: Uliulizwa maswali kuhusiana na miamala na katika majibu yako ukasema sio lazima ku-tress kila senti kinachotakiwa mtu awe na knowledge ulikuwa unamaanisha nini


Shahidi: Mtumaji wa hizi fedha ambaye ni Mbowe aliweza kutuma hizo fedha na zikamfikia Luten Urio na yeye akazigawa.

Wakili Hilla: Mheshimiwa Jaji ni hayo tu.

Wakili Kidando: Mheshimiwa Jaji hatutakuwa na maswali tena kwa shahidi.


Jaji: Shahidi tunakushukuru kwa ushahidi.


Wakili Kidando: Baada ya ushahidi wa shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu 41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande wetu tunafunga kesi hii.

Jaji: Mahakama imekubaliana na maombi ya upande wa mashitaka kufunga kesi hii.


Wakili Kibatala: Baada ya upande wa mashtaka kufunga kupitia kifungu hicho cha 41 tunaomba mahakama hii itupe nafasi ya kufanya mawasilisho ya mwisho.


Lakini pia tuna maombi mawili ombi la kwanza Mahakama itupe mwenendo wa kesi lakini pili tupewe nafasi yakufanya mawasilisho ya mwisho oral.


Jaji: Kwanini unataka kufanya mawasilisho orally.


Kibatala: Tulikuwa tumeshajadiliana mwanzoni na kunafaida fulani fulani tutazipata.

Wakili Nashon Nkungu: Kwa niaba ya mshtakiwa wa kwanza: Tunaomba mawasilisho ya mwisho tuyafanye kwa njia ya mdomo na kupewa mwenendo wa kesi.

Wakili John Mally: Niunge mkono hoja za mawakili wenzangu na kuomba kufanya mawasilisho ya mwisho kama kuna kesi ya kujibu au la.

Wakili Fredrik Khiwelo: Kwa niaba ya mshtakiwa wa tatu: Niungane na wenzangu lakini pia na mimi ningeomba kupatiwa mwenendo wa kesi kwaajili ya kufanya mawasilisho ya mwisho kwa njia ya mdomo.

Wakili Kidando: Tukirejea kifungu cha 41 bado upande wa mashtaka tunaomba kufanya kwa nija ya maandishi

Shauri hili ukizingatia limeanza Septemba mwaka jana hatujajua itachukua muda gani kupata mwenendo wa kesi.

Jaji: Hadi leo PS wangu ameshachapa kurasa 1,400 nikichanganya za jana na leo zinaweza kufika 1,600 nilikuwa nafikiria hapa nadhani nipatiwe dakika kumi tukajadiliane.

Mahakama imerejea baada ya majadiliano na mawakili wa pande zote.

Jaji: Baada ya kusikiliza na kupitia hoja za pande zote mbili na kuzingatia kifungu cha 41 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Mahakama hii itatoa uamuzi Februari 18, 2022 kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la saa nane mchana na washtakiwa mtaaendelea kubaki chini ya uangalizi wa Magereza.