Upande wa mashtaka wafunga ushahidi kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu umesema umemaliza ushahidi baada ya shahidi wa 13 kumaliza ushahidi wake.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu umesema umemaliza ushahidi baada ya shahidi wa 13 kumaliza ushahidi wake.


Leo Jumanne Februari 15, 2022 shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila amemaliza kutoa ushahidi baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.


Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert Kidando aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba mahakama ione kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.


“Baada ya ushahidi wa shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu 41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande wetu tunafunga kesi hii” amesema Wakili Kidando.


Hata hivyo, baada ya kutoa ombe hilo, upande wa utetezi kupitia Wakili Peter Kibatala umeomba kupewa nafasi ya kufanya mawasiliano ya mdomo pamoja na kupewa mwenendoi wa kesi.


“Baada ya upande wa mashtaka kufunga kupitia kifungu hicho cha 41 tunaomba mahakama hii itupe nafasi ya kufanya mawasilisho ya mwisho Lakini pia tuna maombi mawili ombi la kwanza Mahakama itupe mwenendo wa kesi lakini pili tupewe nafasi ya kufanya mawasilisho ya mwisho oral” amesema Kibatala.


Akijibu hoja hizo, Jaji Joachim Tiganga aliomba kupewa dakika kumi wajadiliane kabla ya kutoa uamuzi.


“Hadi leo PS wangu (msaidizi) ameshachapa kurasa 1,400 nikichanganya za jana na leo zinaweza kufika 1,600 nilikuwa nafikiria hapa nadhani nipatiwe dakika kumi tukajadiliane” amesema Jaji Tiganga