Kina Mbowe wadai hawajala 'lunch' miezi mitano

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimiana na baadhi ya wafuasi wa chama hicho wakati akiingia mahakamani na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi. Picha na Sunday George

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi wamedai kuwa hawajawahi kula chakula cha mchana wakiwa mahakamani hapo kwa zaidi ya miazi mitano huku wakiiomba Mahakama kutoa muongozo wa suala hilo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi wamedai kuwa hawajawahi kula chakula cha mchana wakiwa mahakamani hapo kwa zaidi ya miazi mitano huku wakiiomba Mahakama kutoa muongozo wa suala hilo.

Akiwakilisha washtakiwa wenzake, Mbowe ametoa lalamiko hilo leo Jumatatu Februari 14, 2022 mchana muda mfupi baada ya Mahakama kurejea ambapo ilikuwa imesimama kwa dakika 45 kwaajili ya mapumziko.

Mbowe amedai kuwa tangu wameanza kuhudhuria mahakamani hapo miezi mitano iliyopita hawajawahi kupewa chakula cha mchana na kudai ndugu hawatakiwi kuwaletea badala yake wanaambiwa wanatakiwa watoke nacho gerezani.

Mbowe alinyosha mkono mahakamani hapo na kutoa lalamiko akisema “Mheshiimiwa Jaji kwa kipindi cha miezi mitano tumenyimwa haki ya kula, Tunapoenda break wenzetu wamekuwa wanakula lakini sisi hatuli, tunaomba ulitolee maelezo angalau tuwe tunapewa chakula na ndugu zetu kama wanavyofanya gerezani

“Tumekuwa tukiambiwa kama ni kula tuwe tunatoka na chakula gerezani kama unavyojua kule hakuna friji” amedai Mbowe

Baada ya Mbowe kutoa malalamiko hayo, Jaji Joachim Tiganga anayesikikliza kesi hiyo ya ugaidi aliwaita mawakili wa pande zote kwenda kujadili suala hilo ofisini kwake na baada ya muda mfupi Mahakama ikarejea na Jaji Tiganga kumpa nafasi Mbowe ya kuzungumza tena.

“Muda iliyopita mshtakiwa wa nne alileta hoja tukaenda kujadiliana na pande zote zinazohusika na suala hilo limeshughulikiwa basi kwa aliyeleta hoja kama ana lolote la kusema” Amesema Jaji Tiganga kabla ya Mbowe kuzungumza

Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo alinyanyuka na kusema “Mheshimiwa Jaji nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja ingawa nje ya utaratibu, lilikuwa ni jambo la muda mrefu ingawa sikuwashirikisha mawakili lakini tuliona ni njia rahisi ya kufikisha ujumbe ili kuweza kushughulikiwa” ameeleza Mbowe nakuongeza

“Nishukuru kwa namna lilivyoshughulikiwa wewe pamoja na uongozi wa Mahakama basi wakati linaendelea kushughulikiwa na kupatiwa ufumbizi wa kudumu basi tuendelee na shauri hili.

Ingawa tuna njaa lakini bado tuna nguvu ya kuendelea na kesi basi niombe radhi kwa wale niliowakwaza” amesema.

Baada ya Mbowe kueleza hayo, Jaji Tiganga alimruhusu wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala kuendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka.

Leo, shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila ameendelea kuhojiwa na upande wa utetezi.

Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa mpaka keso Jumanne ambapo Wakili Kibatala ataendelea kumhoji shahidi huyo wa 13 wa upande wa mashtaka.


Soma hapa kujua kilichojiri mahakamani hapo leo


Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo ameshaingia mahakamani na kesi imeanza, baada ya utambulisho wa mawakili wa pande zote.

Wakili Peter Kibatala anaanza kumhoji shahidi wa 13 Inspekta Tumaini Swila baada ya Jaji kumkumbusha shahidi kuwa bado yuko chini ya kiapo

Kwanza wakili Kibatala anaomba kielelezo cha nne na cha tano vya upande wa mashtaka kisha anauliza


Wakili: Shahidi unakumbuka mara mwisho zoezi letu lilisimama kwa sababu za kiafya?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Bila shaka uliitoa kauli hiyo ukiwa chini ya kiapo?


Shahidi: Ni Sahihi


Wakili: Una daktari mahsusi au unahudumiwa tu unapokwenda?


Shahidi: Ninahudumiwa na madaktari wawili tofauti


Wakili: Unaweza kuwataja?


Shahidi: Mmoja anaitwa Mohamed


Wakili: wa pili?

Shahidi: Sikumbuki


Wakili: Ukiacha huyo Dk Mohamed jina la daktati wa pili humfahamu hata jina moja?


Shahidi: Simkunbuki


Wakili; Ni hali ya kawaida daktari ambaye amekuhudumia miaka miwili usimkumbuke?


Shahidi: Ni hali ya kawaida


Wakili: Ulilazwa au ulipumzishwa?


Shahidi: Nilipumzishwa


Wakili: Huko nyumbani kuna daktari ambaye alikuwa anakuja kukuhudumia?


Shahidi: Hapana


Wakili: Sawa, tutashughulika na mambo hayo baadaye maana kama nilivyokwambia tuliwaandikia (hiyo hospitali) na watatujibu.


Wakili: Hivi Jeshi la Polisi mnafanya kazi kwa pamoja au kila mtu kivyake?


Shahidi: Kwa pamoja


Wakili: Uliwahi kumuuliza DCI kama alimuuliza RPC wa Mtwara akamhoji baba yake Ling'wenya?


Shahidi: Hapana


Wakili: Unakubaliana na mimi maelezo ya washtakiwa ni moja ya source namna ambayo hela zilitoka na kutumika?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Tukianza na Urio fedha ambazo aliwapatia Ling'wenya na Kasekwa aliwapatia kwa matumizi gani?


Shahidi: Kwa matumizi ya kwenda kukutana na Freeman Mbowe


Wakili: Ni sawa na kusema walitumia kwa nauli?


Shahidi: Ni sawa


Wakili: Ni sahihi fedha hii waliyopewa kwa ajili ya nauli wameielezea wenyewe kwenye maelezo yao?


Shahidi: Ndio


Wakili: Ni sahihi pia kwamba fedha hizo zimezungumzwa katika maelezo ya Luteni Urio ambayo uliyaandika wewe?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Unakumbuka Luteni Urio alisema aliwapa kina Ling'wenya shilingi ngapi?


Shahidi: Lakini moja na tisini na tano kisha laki moja na tisini na tisa


Wakili: Hizi laki moja na tisini na tano zinaonekana katika maelezo yao?


Shahidi: Ndio zinaonekana


Wakili: Na wewe kama mpelelezi makini ambaye unapeleleza kesi hii nzito uliziona?


Shahidi: Ndio


Wakili: Unakumbuka katika maelezo yake Kasekwa anasema baadhi ya fedha alizopewa alikwenda kununua nguo likiwemo shati la mauamaua ambalo alilivaa siku anahojiwa?


Shahidi: Nakumbuka maneno kununua shati.

Wakili: Hilo shati la maua ambalo alinunua kwa fedha aliyopewa na Mbowe linahusiana vipi na ugaidi?

Shahidi: Vinahusiana kwa sababu alinunua kwa fedha ambazo alipewa na Mbowe?


Wakili: Shahidi naomba ushike maelezo ya Adamu Kasekwa, Tafuta eneo la Luteni Urio alitupa nauli elfu 87.

Wakili: Nataka kujua nauli waliyopewa kwa ajili ya kwenda Moshi ilikuwa ni shilingi ngapi na kama walipewa mmojammoja au walipewa kwa pamoja.


Wakili: Kwa hiyo kila mtu alipewa elfu 87 kwenda Moshi?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Hayo maelezo uliona yana upunguf au ni sahihi?


Shahidi: Sikuona upungufu


Wakili: Kwa hiyo kwa maelezo hayo jumla walipewa shilingi ngapi wote wawili?


Shahidi: Sh174,000


Wakili: Tafuta katika maelezo hayo hela iliyobaki katika laki Sh199,000, elfu 25,000 kama utaiona


Shahidi: Haijaelezwa


Wakili: Wewe kama mpelelezi uliielezea vipi hiyo tofauti?


Shahidi: Alishahojiwa, hakukuwa na umuhimu


Wakili: Kwa hiyo hiyo Sh25,000 kwenye maelezo ya Kasekwa tunaipata wapi ili hesabu ya Sh199,000 iliyoko kwenye hati ya mashtaka itimie?


Shahidi: Haionekani kwenye maelezo ya Kasekwa

Wakili: Uliwahi kufundishwa katika kozi za upelelezi kuwa maelezo ya mshtakiwa lazima yaeleze kila kitu?


Shahidi: Si kweli kwamba lazima maelezo yote yaandikwe


Wakili: Kwa hiyo wewe tofuati ya Sh25000 ni immaterial?


Shahidi: Haina umuhimu


Wakili: Sasa shahidi fungua maelezo ya Ling'wenya na tafuta sehemu baada ya mazungumzo ya Luteni Denis Urio, mpaka pale ambapo ni Shilingi ngapi walizopatiwa


Wakili: Unakubaliana na mimi kwa maelezo hayo baadhi ya fedha hizo alinunua nguo?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ling'wenya anasema walinunua nguo ili waonekane nadhifu?


Shahidi: Sahihi


Wakili: Ni sahihi Urio aliwapa Sh190,000?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Kwa maelezo ya Luteni Urio alitumiwa Sh199,000 na Ling'wenya anasema walipewa Sh190,000 hizo figure zinafanana au zinatofautiana?


Shahidi: Zinafanana


Wakili: Na kwa maelezo ya Kasekwa ambayo walikuwa pamoja na walikamatwa pamoja hizi zinafanana au zinatofautiana?


Shahidi: Zinafanana.


Wakili: Sh199,000 kutoa Sh190,000 inabaki ngapi?


Shahidi: Elfu tisa


Wakili: Kwenye maelezo ya Ling'wenya hiyo elfu tisa imefafanuliwa wapi?


Shahidi: Haijafafanuliwa


Wakili: Hiyo tofauti ya elfu tisa uliifanyiaje kazi?


Shahidi: Sikuona tofauti maana wote wanakiri kupewa pesa na Urio


Wakili: Soma maelezo ya washtakiwa wote wawili halafu eleza hiyo Sh195,000 kwenye maelezo ya Urio, wanaizungumziaje? Tukisema kwamba hawajazungumzia tutakuwa tumekosea shahidi?


Shahidi: Watuhumiwa hawajazungumzia, lakini Urio ameizungumzia


Wakili: Simzunguzii Urio maana huyo ni mtoa taarifa na hawa ni washtakiwa, nauliza kwenye maelezo ya mshtakiwa wa pili na wa tatu, ipo? wanakiri kuipokea kama refund ya nauli?


Shahidi: Kwenye maelezo ya washtakiwa hawajaeleza


Wakili: Na wewe unaona ni hali ya kawaida?


Shahidi: Ni hali ya kawaida


Wakili: Na kwa sabau ni hali ya kawaida hukuchukua hatua yoyote?


Shahidi: Nilichukua


Wakili: Hatua gani?


Shahidi: Niliangalia maelezo ya Urio ambayo ni ya uhakika na yalipelekea watuhumiwa kukamatwa.


Wakili: Na maelezo ya washtakiwa?


Shahidi: Nayo ni ya uhakika kwa kadri wao walivyoeleza.

Wakili: Kipi ulianza kukiona kati ya maelezo ya Urio na ya washtakiwa?


Shahidi: Maelezo ya washtakiwa


Wakili: Ambao hawazungumzii hiyo Sh195,000.


Shahidi: Nilikuwa sijayasoma


Wakili: Uliposoma maelezo ya Urio na ya washtakiwa ulilinganisha?


Shahidi: Nililinganisha


Wakili: Na ukaona kila kitu kiko sawa?


Shahidi: Ndio


Wakili: Urio anasema alitumiwa Sh500,000, akatoa Sh300,000 akawapa hao vijana baadaye akatoa tena Sh195,000 akawapa wengine, inakuwa kiasi gani?


Shahidi: Sh495,000


Wakili: Elfu tano iko wapi?


Shahidi: Ni gharama za mtandao


Wakili: Hizo gharama za mtandao umetoa kwenye maelezo ya Urio?


Shahidi: Hapana aliniambia


Wakili: Kwenye maelezo yako umeizungumzia?


Shahidi: Hapana


Wakili: Uliwahi kuambiwa kuwa hata shahidi kutoka Airtel alizungumzia?


Shahidi: Sikuuliza


Waakili: Uko interested na hii kesi? Una umakini nayo?


Shahidi: Ndio


Wakili: Unafahamu gharama za mtandao zinatakiwa zionekane kwenye rekodi za Airtel?


Shahidi: Hilo sijui


Wakili: Ndio maana nakuuliza una umakini na hii kesi wewe kama mpelelezi wa kesi hii ya ugaidi?


Shahidi: Ndio


Wakili: Kwa upelelezi wako washtakiwa walipewa kiasi gani kwenda kumfuatilia Sabaya Moshi?


Shahidi: Katika upelelezi wangu sikuweza kuona fedha zaidi ya zile Sh669,000 lakini kwa maelezo ya washtakiwa walieleza kuwa zipo


Wakili: Lakini hizo ni za kufikirika hazipo kwenye hati ya mashtaka?


Shahidi: Ndio


Wakili: Unaona kwenye hati ya mashtaka zinatusaidia?


Shahidi: Ndio, zinasaidia


Wakili Kibatala anaomba kielelezo cha 15 mpaka 20


Wakili: Ulieleza kuwa katika hati ya ukamataji mali kwa Ling'wenya simu moja haikuwa na IMEI number kwani ilikuwa imefutika na ukatoa ushahidi namna ulivyoipata hiyo IMEI number?


Shahidi: Ndio


Wakili: Ulifanyaje?


Shahidi: Nilibonyeza #*106#


Wakili: Ulimtajia Jaji hiyo IMEI number?


Shahidi: Sikumtajia


Wakili: Hiyo uliyoipata uliwasiliana na ‘manufacturer’ au wakala wake nchini wa Tecno kujiridhisha hiyo uliyoipata ni sahihi?


Shahidi: Hapana


Wakili: Huo utaratibu ulimwambia Jaji kwamba ni ulifundishwa na ‘manufacturer’ kuwa kama IMEI number ikifutika unatumia utaratibu huo?


Shahidi: Hapana


Wakili: Unafahamu kwamba IMEI number ni DNA ya simu?


Shahidi: Nafahamu



Wakili: Shahidi wakati unafanya shughuli zako za upelelezi hizo IMEI number ulizozipata mwenyewe alisema chochote kuhusu IMEI number za simu zake?


Shahidi: Hakueleza


Wakili: Unafahamu ICCID number (ile DNA ya sim card)?


Shahidi: Ndio


Wakili: Kwenye maelezo yake Ling'wenya amezungumzia ICCID ya simu zake?


Shahidi:  Hajazungumzia.


Wakili: Gladys Fimbari (Shahidi kutoka Airtel) alizungumzia miamala ya simu ngapi?


Shahidi: Mbili


Wakili: Kwa hiyo Gladys Fimbari aliombwa miamala ya namba tatu yeye akajibu ya namba mbili akaacha moja, ni sahihi?


Shahidi: Sahihi


Wakili: Hiyo elfu 80 ambayo ilibadilishana kati ya Mbowe na namba hiyo ndio iliyoachwa?


Shahidi: Haikuachwa, miamala yake iko kwenye ripoti


Wakili: Nakuuliza kwenye covering letter, imetajwa haijatajwa? Huko kwenye miamala nitakupeleka.


Shahidi: Haijatajwa


Wakili: Sasa twende kwenye miamala wa tarehe 20/7/2020 hizo taarifa za miamala ulisoma na ukazielewa vizuri kama mpelelezi?


Shahidi: Nilisoma


Wakili: Kwa hiyo ni sahihi kukuuliza maswali kuhusu hiyo miamala.


Shahidi: Kwa kile nilichokielewa.


Wakili: Wewe ndio uliyeandika maelezo ya Mwanasheria wa Tigo, Frank Kapala?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ulimweleza Jaji ni juhudi gani ulichukua ku- reconcile tofauti ya mwaka wa jalada la (uchunguzi), katoka covering letter ya kuomba miamala Tigo (2020) na covering letter ya majibu kutoka tigo (2021)?


Shahidi: Sikumweleza


Wakili: Unajua implication ya tofauti hizo kisheria?


Shahidi: Sijui


Wakili: Nani author wa barua ya Tigo?


Shahidi: Imeandikwa na Mwanasheria


Wakili: Ulimweleza Jaji kwa nini barua haina jina la author lakini ukaenda kumhoji mtu anaitwa Frank Kapala wakati wewe hufanyi kazi Tigo?


Shahidi: Sikumwambia


Wakili: Tukisema kuwa ushahidi huu ni wa kutunga unasemaje?


Shahidi: Siyo sahihi.


Wakili: Hii ni covering letter kutoka Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, addressee ni nani?


Shahidi: Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai


Wakili: Ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hii, siyo?


Shahidi: Imendikwa kwa ofisi


Wakili: Hebu soma imeandikwa kwa Kurugenzi au Mkurugenzi?


Shahidi: Mkurugenzi


Wakili: Mkurugenzi ni ofisi?


Shahidi: Hapana


Wakili: Barua kutoka kwa DCI kwenda Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi?


Shahidi: Tarehe 13/8/2020


Wakili: Na barua ya majibu ni ya tarehe ngapi?


Shahidi: Tarehe 9/7/2021


Wakili: Ni baada ya muda gani?


Shahidi: Takribani miezi 11


Wakili: Waliwahi kukufafanulia kwa nini uchunguzi wa kesi nzito kama hii ulichukua muda mrefu kiasi hicho kufanya extraction tu?


Shahidi: Ndio

Wakili: Ni nini?


Shahidi: Walisema kwamba wana vielelezo vingi vya kufanyia uchunguzi.


Wakili: Unafahamu kwamba tarehe hizo ndio zilikuwa zinaelekea kwenye vuguvugu la Katiba mpya?


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Wakati mnawapelekea maombi haya ya uchunguzi mliwaeleza kuwa ni ya haraka au walifanya tu kama uchunguzi wa mtu na mpenzi wake waliotumiana meseji?


Shahidi: Walielezwa.


Wakili: Unafahamu washtakiwa Halid Athuman na Gabriel Mhina waliachiwa baada ya mwaka mzima?


Shahidi: Ndio


Wakili: Unafahamu ni athari gani walizozipata kwa kukaa gerezani kusubiri uchunguzi muda wote huo?


Shahidi: Sifahamu


Wakili: Maelezo kwamba Freeman Mbowe alituma hela nyingine kwa washtakiwa wenzake na kutoa maelekezo ya nini cha kufanya ulitoa wapi, kwenye ripoti au kwenye maelezo ya washtakiwa?


Shahidi: Kwenye ripoti


Wakili: Kwenye ripoti ni wapi onyesha palipoandikwa hivyo?


Shahidi: Kwenye ripoti hakuna maelezo hayo?


Wakili: Tunakubaliana hivyo na in fact kwenye ripoti anayeomba hela ni Urio, siyo?


Shahidi: Denis Leo Urio


Wakili: Ni sahihi kwamba kwenye Meseji uliyoisoma (naomba unitumie nauli ya kuwa-mobilize Morogoro) haioneshi lengo?


Shahidi: Hi meseji ni mojawapo ikiwa ni mwendelezo wa kile walichokiongea


Wakili: Nani aliyetaja kiasi?


Shahidi: Denis Leo Urio


Wakili: Kwa upelelezi wako nani aliyesema usiwe unatumia namba yako tumia ya wakala?


Shahidi: Denis Leo Urio


Wakili: Ulimhoji Luteni Denis Leo Urio, ulimhoji inakuwaje yeye aliyetumwa kumtoa gaidi pangoni anamwambia atumie namba ya wakala au wasaidizi wake?


Shahidi: Ndio, alieleza.


Wakili: Anamkabidhi shahidi maelezo ya Luteni Urio kisha anamuuliza ni wapi Urio amefafanua sababu ya kumtaka Mbowe asitumie namba yake bali ya wakala au wasaidizi wake?


Shahidi: Alifanya hivyo kwa lengo la kukusanya ushahidi ili kumuweka karibu asiweze kumtilia mashaka


Wakili: Hiyo ni tafsiri yako au maneno hayo yako katika maelezo ya Luteni Urio?


Wakili Kidando anasimama kupinga swali hilo akidai kuwa shahidi ameshalijibu na kama wakili Kibatala hafurahishwi na jibu basi aendelee na swalji lingine.


Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji kwa kuwa mwenzangu ana uhakika kuwa shahidi ameshajibu swali basi naomba anisomee jibu hilo ili nione naulizaje ili kupata information ninayoitaka.


Jaji: Anamfafanulia shahidi swali iwapo Luteni Urio kwenye maelezo yake kuna mahali ametoa ufafanuzi wazi kuwa lengo la kumtaka Mbowe asitumie namba yale badala yake atumie ya wakala au wasaidizi wake.


Shahidi: Kwenye maelezo maneno hayo hayapo lakini ndio kama nilivyoeleza kwamba ili kukusanya ushahidi.


Kibatala: Mheshimiwa Jaji naona ni saa saba kasoro dakika tatu, naomba kutoa hoja kuahirisha kwa muda.


Jaji: Naahirisha shauri hili kwa muda wa dakika 45. Tutarudi hapa saa 7:45.


Mahakama imerejea baada ya mapumziko mafupi, mawakili wa pande zote wako tayari kuendelea.


Mshtakiwa wa nne Freeman Mbowe amenyosha mkono


Mbowe: Mheshiimiwa Jaji kwa kipindi cha miezi mitano tumenyimwa haki ya kula.


Tunapoenda break wenzetu wamekuwa wanakula lakini sisi hatuli, tunaomba ulitlolee maelezo angalau tuwe tunapewa chakula na ndugu zetu kama wanavyofanya gerezani.


Tumekuwa tukiambiwa kama ni kula tuwe tunatoka na chakula gerezani kama unavyojua kule hakuna friji.


Jaji: Kibatala umekuwa unawakilisha nini kama watuhumiwa siku zote wamekuwa hawali.


Kibatala: Toka mwanzo hili tatizo nilishaliona na kuwasiliana na ofisa wa magereza na akahidi kulishughulikia.


Wakili Kidand: Mheshimiwa Jaji nadhani tungekutana na mawakili wenzetu tulijadili.


Jaji: Nawaalika mawakili wa pande zote ofisini kwangu.


Mshtakiwa wa nne Freeman Mbowe ameitwa ofisini kwa Jaji ambapo mawakili wa pande zote wapo wakiendelea kujadiliana.


Mahakama imerejea


Jaji: Muda iliyopita mshtakiwa wa nne alileta hoja tukaenda kujadiliana na pande zote zinazohusika na suala hilo limeshughulikiwa basi kwa aliyeleta hoja kama ana lolote la kusema.


Mbowe: Mheshimiwa Jaji nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja ingawa nje ya utaratibu.


Lilikuwa ni jambo la muda mrefu ingawa sikuwashirikisha mawakili lakini tuliona ni njia rahisi ya kufikisha ujumbe ili kuweza kushughulikiwa.


Nishukuru kwa namna lilivyoshughulikiwa wewe pamoja na uongozi wa Mahakama Kuu basi wakati linaendelea kushughulikiwa na kupatiwa ufumbizi wa kudumu basi tuendelee na shauri hili.


Ingawa tunanjaa lakini bado tuna nguvu ya kuendelea na kesi basi niombe radhi kwa wale niliowakwaza.



Wakili Kibatala anaendelea;

Wakili: Ni kweli kielelezo G ambacho ni simu uligundua kama ndani kulikuwa na laini ya Vodacom?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ni sahihi hii namba ndio laini ya Vodacom ambaye Urio aliitoa na kuweka kwenye simu nyingine ili muweze kuwasiliana


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ni sahihi hatuna nyaraka za simu tatu mlizokabidhiana na Luteni Urio iliyotolewa hapa Mahakamani kama kielelezo?


Shahidi: Sikutoa lakini niliieleza Mahakama


Wakili: Kwa kuwa una kielelezo ambacho ni maelezo ya Urio uliyaandika kuna popote katika hizo namba zimeandikwa


Shahidi: Hakuna

Wakili: Ni sahihi katika ripoti ya uchunguzi iliyoandaliwa na Inspekta Ndowo hakuna mahali imeonyesha mawasiliano ya Telegram ya Freeman Mbowe na hizo namba


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Kama mpelelezi ulifafanya chochote kwa Mheshimiwa Jaji kuhusiana na hizo namba


Shahidi: Sikufafanua


Wakili: Kwa ruhusa ya Mahakama naomba nikuonyeshe kielelezo namba 26


Wakili: Zile meseji umeziona kwa ujumla wake


Shahidi: Nimeziona


Wakili: Hiyo ripoti uliisoma na kuielewa


Shahidi: Niliielewa kiasi


Wakili: Unafahamu mtu aliyefanya uchunguzi wa instruction report kuhusiana na namba zilizokuwa zinawasiliana telegram

Shahidi: Sifahamu


Wakili: Hii namba ya Voda uliwahi kuwaandikia Voda ili tujue imesajiliwa kwa jina la nani


Shahidi: Sikuandika ila najua ulikuwa ya Denis Urio


Wakili: Na ulifahamu wapi


Shahidi: Ameitaja kwenye particular

Wakili: Ni sahihi hakuna sehemu yoyote hiyo namba imetajwa kwenye hayo maelezo


Shahidi: Imetajwa tu hapa juu huku ndani haijatajwa


Wakili: Ulimfafanulia Mheshimiwa Jaji


Shahidi: Sijamfafanuli


Wakili: Ulimweleza Jaji ulipata wapi mafunzo kuwa meseji za Telegram huwa zinabaki kwenye simu


Shahidi: Sijamueleza


Wakili: Simu zilizochukuliwa kwa Bwire ni sahihi zilikuwa kwenye himaya ya Kingai na Goodluck


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Tunakubaliana hujaleta karatasi ya hati za makabidhiano ya hizi simu za kina Bwire


Shahidi: Sijatoa


Wakili: Naomba nisomee hapa kwenye maelezo ya Hassan Kasekwa

Shahidi anasoma

Wakili: Unakubaliana na mimi kuna namba hapo hazipo


Shahidi: Rudia


Wakili: Hebu nisomee hizo namba.


Shahidi: 353736289120273


Wakili: Zinafanana?


Shahidi: Hazifanani lakini hazimaanishi sio yenyewe


Wakili: Ulitoa ufafanuzi wakati unaongozwa na Wakili


Shahidi: Sijatoa


Wakili: Angalia maelezo ya onyo ya Kasekwa ni wapi ana-identify PUK iliyoko kwenye simu yake


Shahidi: Hayapo lakini haimaanishi sio simu yenyewe


Wakili: Kwenye ripoti ya Inspekta Ndowo kuna mahali yamejirudia? Au ulitoa ufafanuzi kwanini zimetofautiana


Shahidi: Sijatoa


Wakili: Nakuonyesha ripoti ya umiliki wa silaha


Hii ripoti ni moja ya vitu ulivyofanyia kazi katika upelelezi wako


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Ulimwambia Jaji utofauti wa jalada uliopo kati ya jalada ulilofungua na la ripoti ya uchunguzi


Shahidi: Sikumwambia


Wakili: Wakati unawasiliana na wakamataji uliambiwa Adam Kasekwa alikamatwa Rau madukani majira ya saa ngapi


Shahidi: Sikumbuki


Wakili: Hebu angalia maelezo ya Adam Kasekwa alikamatwa muda gani


Shahidi: saa tano


Wakili: Wewe na Adam Kasekwa nani anajua muda wa ukamataji


Shahidi: Kimya


Wakili: Unajua Mohamed Ling'wenya na Adam Kasekwa walikamatwa pamoja


Shahidi: Nafahamu


Wakili: Angalia maelezo yao ya onyo umwambie Jaji walikamatwa sangapi


Shahidi: Saa saba mchana


Wakili: Kuna tofauti ya masaa mangapi?


Shahidi: Mawili


Wakili: Uliyafanyiaje kazi


Shahidi: Niliyafanyia kazi


Wakili: Ripoti ya maandishi unakumbuka uliizungumzia


Shahidi:  Ndio


Wakili: Anasema ulimpelekea makaratasi tisa na sio nane, ulimfafanulia Mheshimiwa Jaji


Shahid: Sikumfafanulia


Wakili: Unakumbuka wakati nakuuliza maswali kuhusu sayansi ya waandishi wa habari.


Wakili Chavula: Mheshimiwa Jaji sijui anatupeleka wapi hakuna mahali popote alipozungumzia waandishi wa habari.


Wakili Kibatala: Nanachokumbuka shahidi alisema alikusanya sampuli tisa lakini zilizopokelewa ni kumi na tano


Kama kitu walileta wenyewe na wakapinga ninayo haki ya kuuliza maswali.


Jaji: Unaweza kuuliza swali lolote bila kurefer kwenye ripoti, ripoti sijaipata haipo Mahakamani nitashindwa kurefer wakati naandika hukumu.

Kibatala: Kwa maelekezo hayo na kwa utaratibu wetu naomba kuishia hapa kwa kuwa bado nina maswali tuendelee kesho kwa muda utakaoona unafaa.


Wakili Kidando: Hatuna pingamizi


Jaji: Kufuatia maombi ya upande wa utetezi naahirisha shauri hili hadi kesho saa tatu asubuhi ambapo shahidi wa 13 ataendelea kutoa ushahidi na washtakiwa wataendelea kuwa chini ya magereza.