Kitendawili shahidi kesi ya kina Mbowe leo

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimiana na baadhi ya wafuasi wa chama hicho wakati akiingia mahakamani na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi. Picha na Sunday George

Muktasari:

Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu leo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa huku kukiwa bado kuna kitendawili kuhusu ni shahidi gani atapanda kizimbani kutoa ushahidi.

Dar es Salaam. Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu leo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa huku kukiwa bado kuna kitendawili kuhusu ni shahidi gani atapanda kizimbani kutoa ushahidi.

Kitendawili hicho cha shahidi atakayepanda kizimbani leo kinatokana na hali ya afya ya shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Tumaini Swila ambaye alishindwa kuendelea na ushahidi wake baada ya kujisikia vibaya kiafya.

Inspekta Swila alishindwa kuendelea na ushahidi Alhamisi iliyopita wakati akihojiwa na wakili wa Mbowe, Peter Kibatala kuhusiana na ushahidi wake wa msingi alioutoa wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka.

Kutokana na maombi ya upande wa mashtaka, Jaji Joachim Tiganga anayesikikliza kesi hiyo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, aliiahirisha mpaka kesho yake, (Ijumaa).

Hata hivyo siku hiyo pia shahidi huyo hakufika mahakamani, hivyo mahakama ikalazimika kuahirisha kesi hiyo hadi leo, kwa ajili ya shahidi huyo kuendelea na ushahidi wake kama hali ya afya itakuwa imeimarika au kuendelea na shahidi mwingine.


Hali ilivyokuwa

Alhamisi wiki iliyopita, Inspekta Swila alipanda kizimbani kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wake wa nyongeza yaani kuhojiwa na upande wa utetezi, ikiwa ni siku ya nne ya ushahidi wake, na siku ya tatu ya kuhojiwa na mawakili wa utetezi.

Baada ya kupanda kizimbani kabla ya kuanza kuhojiwa, Inspekta Swila aliieleza mahakama hiyo kuwa jana yake hali yake afya hauikuwa nzuri, lakini akasema ataendelea kutoa ushahidi wake.

Lakini baada ya kuhojiwa kwa takribani saa mbili, Inspekta Swila akaieleza mahakama kuwa asingeweza kuendelea kwa kuwa alikuwa akijisikia vibaya. Hivyo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando aliiomba mahakama itoe ahirisho hadi kesho yake.

Wakili Kibatala alipinga maelezo ya shahidi na maombi ya ahirisho, akidai kuwa shahidi anataka kukwepa kujibu maswali yake.

Hata hivyo, aliiomba mahakama kama maombi ya ahirisho hilo yatakubaliwa, mahakama imuamuru shahidi awasilishe uthibitisho wa kidaktari kuhusu hali ya afya yake.

Jaji Tiganga alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka kuwa suala la afya ya mtu ni nyeti na kwamba katika utamaduni wa kimahakama ni moja ya sababu muhimu za ahirisho la kesi, akaahirisha kesi hiyo mpaka kesho yake (Ijumaa).

Pia Jaji Tiganga alikubaliana na hoja ya wakili Kibatala akaamuru shahidi kuwasilisha uthibitisho wa kitabibu kuhusu afya yake, hasa maelezo ya kuthibitisha kuwa anaumwa au kuwa amepata matibabu.

Ijumaa shahidi huyo hakufika mahakamani, badala yake Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliieleza mahakama kuwa afya yake bado haijatengamaa na kwamba ameshauriwa na daktari apate mapumziko zaidi.

Hivyo aliomba mahakama itoe ahirisho mpaka leo akiahidi kuwa shahidi huyo afya yake itakuwa bado haijatengamaa, wataendelea na shahidi mwingine kwa mujibu wa sheria, huku akiiarifu mahakama kuwa kuna nakala kivuli ya matibabu na kwamba nakala halisi ataiwasilisha shahidi mwenyewe.