Kwa Wahehe sio mbwa tu, hata panya nao wanalika

Mkazi wa Kijiji cha Ndengisivili, wilayani Kilolo, Boas Kikoto akionyesha panya ambao alikuwa akiwaandaa kwa ajili ya kitoweo. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga.

Muktasari:

  • Japo sio rahisi Wahehe kukubali utani kwamba hula nyama ya mbwa, wakazi wa Kijiji cha Ndengisivili, wilayani Kilolo wamekiri kula panya kama njia ya kupambana na wanyama waharibifu.

Iringa. Wakazi wa Kijiji cha Ndengisivili wilayani Kilolo mkoani Iringa, wamesema ulaji wa panya umekuwa silaha kubwa katika kupambana na uharibifu wa mazao yao hasa mahindi shambani.

Wamesema mbali na kuokoa mazao, nyama ya panya ina madini muhimu kwenye mwili wa binadamu jambo lililowafanya waipende nyama hiyo.

Kati ya utani unaowatambulisha zaidi wakazi wa Mkoa wa Iringa ni ulaji wa nyama ya mbwa ambao, hata hivyo hawajawahi kuukubali.

Hata hivyo, Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) wametoa wito kwa Watanzania kula nyama ya panya kwa madai kuwa ina virutubisho adimu mwilini.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 10, 2024 wakati akiandaa panya kwa ajili ya kitoweo, mkazi wa Ndengisivili, Boas Kikoto amesema nyama ya panya ina madini muhimu kwenye mwili lakini pia unapunguza uharibifu wa mazao shambani.

"Hata madaktari wanashauri ulaji wa panya, wananchi wa kijiji hiki wakikamata panya kwenye mashamba yao wananiletea mtaalamu nachoma," amesema.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Belnas Chavala amesema sio kweli kwamba Wahehe wanakula mbwa kama wanavyotaniwa isipokuwa ni kweli baadhi yao hula panya.

"Sisi huku tunakula panya lakini sijawahi kuona tunakula mbwa, mbona makabila mengi tu yanakula panya sio Wahehe peke yetu," amesema Chavala.

Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga amesema ulaji wa panya kwenye eneo hilo ni asili yao.

"Ukishazaliwa huku unakuja ukiona watu wanakula panya, kwa hiyo iwe panya au sio panyaradi analiwa, wanakijiji wanakula," amesema.

Mhadhiri Mwandamizi wa SUA kutoka Idara ya Uzalishaji, Mirende Matiko katika habari ya Mwananchi ya Machi 11, 2021 alinukuliwa akisema nyama hiyo ina ladha nzuri na ni laini.

Kilolo ni moja kati ya wilaya tatu za Mkoa wa Iringa ikiwa na jimbo moja.