Kwanini mikoba ni hatari kwa afya

Monday July 19 2021
mikoba pc

Umewahi kujiuliza huwa unaweka mahali gani mkoba wako na je, kuna usalama wa kutosha kwa afya yako?

Kawaida watu wengi huweka mikoba juu ya meza, viti, madawati ya baa, hotelini, vibaraza vya vyooni, wanachoangalia ni mahali pasafi.

Wataalamu wa afya kutoka taasisi ya kisayansi ya Advanced Biomedical Research walifanya utafiti uliochapishwa katika majarida mbalimbali ya afya, ulionyesha kuwa mikoba ni gari la kubeba vimelea vya magonjwa kutoka eneo moja kwenda lingine.

Lengo la utafiti lilikuwa kujua kati ya mikoba ya wanawake na wanaume ipi inabeba vimela vya maradhi, baada ya uliofanywa awali uliohusisha mikoba ya wanawake kuonyesha inabeba vimelea vya maradhi.

mikoba 2

Hata hivyo, utafiti huo bado ulionyesha mikoba ya wanawake inaongoza kwa kubeba bakteria wengi kutokana na mahali inapowekwa.

Advertisement

“Mara nyingi wanawake huweka mikoba yao katika mazingira yaliyojaa bakteria kama vile meza za jikoni, henka za mikoba, kaunta za choo na kaunta za hoteli, huku wengine wakiweka kwenye makapu ya nguo chafu,” alisema Shaghayegh Haghjooy Javanmard, ambaye alihariri na kuandaa utafiti huo.

Javanmard ambaye pia ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Isfahan University of Medical Sciences, alisema mbali na hilo, pia wanawake huhifadhi vitu vingi vikiwamo vya urembo ambavyo hushikwa na wengi.

Alisema tofauti na wanaume ambao mbali ya kuweka katika kaunta za hoteli, baa na mara chache chooni, huitumia kuhifadhi nyaraka, funguo na sarafu, vitu ambavyo ni rahisi kubeba vimelea vya magonjwa.

Utafiti huo ulifanywa kwa kushirikisha mikoba 145 kutoka kwa wanawake 80 na wanaume 65 na bakteria waliangaliwa wingi wao kwa kutumia vipimo maalumu vya maabara.

Jumla ya mikoba 138, sawa na asilimia 95.2 ilikutwa na bakteria, kati ya hiyo 49.4 ilikuwa nao wa aina moja na 50.7 ilikuwa nao aina mchanganyiko. Mikoba bandia ilikutwa na vimelea wengi wa bakteria kuliko ile iliyotayarishwa na waandaaji halisi kwa maana ya zile kampuni maalumu kwa ajili ya mikoba.


mikoba 3

Tofauti kati ya viwango vya ukuaji wa bakteria kutoka kwa mikoba ya wanawake na ya wanaume iligundulika kuwa ya kitakwimu asilimia 57.2 na 44.7.

Utafiti huo ulihitimisha kwa kushauri kuwapo kwa uangalizi wa matumizi ya mikoba kwa sababu ina nafasi kubwa ya kuambukiza magonjwa kwa kubeba vimelea kutoka eneo moja kwenda lingine kwa urahisi, huku wahusika wakiikumbatia.

Pia ilieleza vifaa kama simu, sarafu, rununu, vifaa vya kuchezea michezo ya kwenye runinga, kibodi na kompyuta zake na vifaa vya matibabu pia vina nafasi kubwa ya kubeba vimelea vya magonjwa, hivyo wanaovitumia wavitunze kwa uangalifu mkubwa.

“Unajua kitu kama kompyuta mpakato, unaweza kuiweka popote kwa muda ili ufanye shughuli nyingine, kumbe ulipoweka pana vimelea wa magonjwa, kisha unaweka kwenye mkoba unaokwenda kuutundika nyumbani na kuwa ni gari la kuvisambaza”alisema Hamid Nasri, aliyeshiriki kufanya utafiti huo.

Advertisement