Kwikwi chanzo kifo cha mwandishi MCL

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Ugonjwa wa Kwikwi, kuharisha na kutapika umekatisha maisha ya Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi mkoani Lindi, Mwanja Ibadi.

Mtwara. Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi mkoani Lindi, Mwanja Ibadi kimetokana na ugonjwa wa kuharisha, kutapika na Kwikwi, imeeleza taarifa ya hospitali.

Ibadi alifariki dunia Mei 27, 2023 katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi alikokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza katika msiba huo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Lindi, Fatuma Maumba alisema wiki iliyopita Mwanja alilazwa katika hospitali ya Ngudu.

Amesema baadaye alihamishiwa Hospitali ya Nyangao na kuruhusiwa baada ya siku kadhaa, kabla ya hali yake kubadilika tena.

Baada ya hali hiyo, Fatuma alisema Mwanja alipelekwa tena katika Hospitali ya Nyangao na ndiko alikofariki.

"Tulikuwa tunawasiliana naye vizuri mara ya mwisho niliongea naye Ijumaa Mei 26, 2023 asubuhi saa mbili akaniambia anaendelea vizuri kutapika na kuharisha kumekata sio kama mara ya kwanza naweza kuruhusiwa leo au kesho" amesema Fatuma Maumba.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Lindi, Goodluck Mshairi alisema watamkumbuka Mwanja kwa ushirikiano na ushauri kwa waandishi wenziwe wa Mkoa wa Lindi.

Mwanja ameacha mke na watoto wanne.

Taarifa kamili za ratiba ya maziko zitajulikana mara baada ya kufika ndugu zake kutoka Wilayani Liwale.