Landesa yataka makundi yote yashirikishwe kupanga matumizi ya ardhi

Baadhi ya wadau wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kikao Cha kupanga matumizi ya raslimali hiyo kwenye vijiji vya Ikongosi na Ikongosi Juu wilayani Mufindi
Muktasari:
Shirika la Kimataifa la Kutetea Umiliki wa Ardhi la Landesa limesema makundi yote kwenye jamii yanatakiwa kushirikishwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi bila ubaguzi.
Iringa. Shirika la Kimataifa la Kutetea Umiliki wa Ardhi la Landesa limesema makundi yote kwenye jamii yanatakiwa kushirikishwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi bila ubaguzi.
Makundi hayo ni pamoja na wanawake, watu wenye ulemavu, kaya maskini, wazee na vijana.
Mkurugenzi wa Landesa Tanzania, Profesa Monica Muhoja ametoa ushauri huo wakati wa kikao cha maandalizi ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vya Ikongosi na Ikongosi Juu, wilayani Mufindi.
Amesema ushirikishwaji wa makundi yote kwenye jamii unasaidia kupunguza migogoro kwa kutenda haki katika kila kundi.
“Kuna mila na desturi ambazo zinawanyima wanawake haki ya kushiriki kwenye mipango ya matumizi bora ya ardhi, nitoe wito kwa Serikali na taasisi ambazo zinapanga ni vizuri kushirikisha kila kundi,” amesema Profesa Muhoja.
Amesema wananchi wanatakiwa kujua thamani ya ardhi na kwamba kila rika linayo haki ya kumiliki raslimali hiyo.
Ofisa Ardhi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Leonard Jaka amesema upangaji wa ardhi kwenye vijiji hivyo unafadhiliwa kwa ushirikiano baina la Landesa na Shirika la Pelum Tanzania.
“Tayari mchakato umeanza na tumefanikiwa kuyashirikisha makundi yote muhimu,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Programe kutoka Pelum Tanzania, Angolile Rayson amesem upangaji wa matumizi bora ya ardhi njia muhimu katika kupambana na migogoro mingi ya ardhi.
Naye Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mwamini Mwakyaka amesema wakulima ni miongoni mwa makundi yanayokumbana na changamoto ya matumizi ya ardhi.
“Migogoro mingi ya ardhi huwa ni baina ya wakulima na wafugaji, wakulima ni wasikivu sana wanachohitaji ni kushirikishwa kwenye upangaji wa matumizi bora ya ardhi,” amesema Mwakyaka.