Lema ajitosa sakata la mawaziri kudaiwa kuhusika kumtukana Rais

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ameonyesha kushangazwa na kauli Paul Makonda kuwa wapo baadhi ya mawaziri wanaomtukana Rais Samia Suluhu Hassan.

Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ameonyesha kushangazwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwa wapo baadhi ya mawaziri wanahusika kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan mtandaoni.

Makonda ameitoa hiyo leo huko Monduli mkoani Arusha katika kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine ambapo alidai anawafahamu baadhi ya watu wanaotuma watu kumchafua Rais Samia mitandaoni na kwamba baadhi yao  ni mawaziri.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika viwanja vya Manyema, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, leo, Ijumaa April 12, 2024, Lema amewataka wananchi kumpa Rais pole kwa kuwa anatukanwa na mawaziri aliowapa kazi.

“Makonda kasema leo anawajua mawaziri wanaohusika kumtukana Rais Samia mbele ya mawaziri, mbele ya waziri mkuu, mbele ya makamu wa Rais, na mbele ya amiri jeshi mkuu wa nchi na viongozi wote na amewapa mpaka Jumatatu wasipoacha atawataja... Kama Rais anatukanwa na mkuu wa mkoa anajua, maana yake nchi hii haina kiongozi wa juu ndiyo sababu lazima tutafute utawala wa nchi hii,” amesema Lema na kuongeza;

“Tumpe pole mama Samia, anatukanwa na mawazri aliowapa kazi, Makonda kasema, siyo mimi…huyu mama alifanya mimi nikarudi Tanzania, nilikuwa nimetoroka, leo kuna mawaziri wanamtukana, nitalia mie.”

Akizungumza kwenye mkutano huo, Boniphace Mwambukusi, amesema mwaka 2024 na 2025 ni mwaka wa ukombozi na kuwataka wananchi kukataa vitisho na kupambana kwa ajili ya nchi yao.

“Kwa nini tunahitaji Katiba mpya, tunahitaji katiba mpya kwa sababu ni wajibu wetu, ni haki yetu kuwaamrisha vingozi kutekeleza matakwa yetu, kwani katiba siyo mkataba ni amri ya wananchi ya namna wanavyotaka Taifa lao liendeshwe,” amesema na kuongeza;


“Hapa tulipo tunakwenda mwaka 2024 na mwaka 2025 ni mwaka wa vita ya ukombozi, tukifanya makosa, mkifanya makosa kuruhusu wababaishaji na vitisho kurudi madarakani tutalia kilio na kusaga meno hakuna wa kutufuta machozi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Jimbo la Moshi Mjini, Raymond Mboya amewataka wananchi kukiamini chama hicho na kuwapa nafasi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025, ili kurudi kupigania maendeleo.


“Nilikuwa Meya wa Manispaa ya Moshi kwa miaka mitano, tuliongoza kwa usafi, leo Moshi inanuka kwa uchafu kila kona, ndugu zangu wananchi, tupeni nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, ili turudi kuipambania Moshi yetu na kuirudisha mahali pake kiusafi na kimaendeleo,” amesema Mboya.