LHRC: Mabadiliko ya tabianchi mwiba haki za binadamu

Mkurugenzi Mtendaji, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga 

Muktasari:

  • Ripoti ya Mabadiliko ya Tabianchi kwenye Haki za Binadamu imebainisha kuwa afya, chakula, elimu, maji safi na salama, mazingira, faragha na familia kama haki zinazoathiriwa zaidi na mabadiliko hayo huku kundi la wanawake na watoto likitajwa kuathirika zaidi.

Dar es Salaam. Afya, chakula, elimu, maji safi na salama, mazingira, faragha na familia zimetajwa kama haki zinazoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, huku kundi la wanawake na watoto likitajwa kuathirika zaidi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) Anna Henga katika uzinduzi wa Ripoti ya Mabadiliko ya Tabianchi kwenye Haki za Binadamu uliofanyika leo Mei 18, jijini Dar es Salaam.

Henga amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kituo hicho katika kanda nne za nchi zikijumuisha maeneo ya mikoa ya Pwani, Dodoma, Manyara, Mwanza, Dar es alaam, Kagera na Mbeya, zimeonyesha kuwa wanawake na watoto wameathirika zaidi na mabadiliko hayo.

Hii inatokana na mtindo wa kuhama hama unaofanywa na baadhi ya familia ili kupata mahitaji hayo, jambo linalosababisha baadhi ya watoto kutopata haki ya ekimu, huku baadhi ya wazazi wakitelekeza familia kutokana na hamahama hiyo.

Kwa mujibu wa bosi huyo wa LHRC, haki za kiuchumi pia zimeendelea kuathiriwa na mabadiliko hayo hasa kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwani yamepelekea upatikanaji hafifu wa bidhaa za kilimo na uvuvi pamoja na uwepo wa magonjwa mbali mbali yanayoathiri mifugo.

Ameongeza kuwa ripoti hiyo pia imebainisha athari za kiutamaduni  zinazotokana na mabadiliko hayo ambapo amesema kuwa wananchi kuendelea kuhama maeneo yao ya asili kutokana na kukosekana kwa chakula, maji safi na salama; kunasababisha athari katika upande wa mila na desturi.

“Katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha kunakuwepo na ustawi wa vizazi vijavyo, LHRC inatoa rai kwa serikali, taasisi na jamii ya Watanzania kwa umoja wetu tuchukue hatua zitakazotuwezesha kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa ustawi wa vizazi vijavyo,” aliongeza.