LHRC yataka midahalo ya wagombea, diaspora na wafungwa kupiga kura

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaaam leo, Aprili 4, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezichambua sheria mpya za uchaguzi zilizosainiwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kikibainisha maeneo yanayopaswa kufanyiwa marekebisho.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetaka kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2024 ili kuweka takwa la ulazima wa kufanya midahalo ya wagombea katika ngazi zote.

 Pia, kimetaka Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi na wafungwa kushiriki katika upigaji kura, kuangalia suala la mgombea binafsi, matumizi ya teknolojia katika hatua zote za uchaguzi kuanzia uchukuaji fomu.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Aprili 4, 2024 na Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga wakati akiwasilisha kwa vyombo vya habari uchambuzi walioufanya kuhusu Sheria za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2024, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi 2024 na Sheria ya masuala ya vyama vya siasa na gharama zake.

Henga amesema pamoja na baadhi ya mambo chanya yaliyozingatiwa katika sheria hizo, bado wanatoa wito kwa Serikali kuangalia vitu vingine ikiwemo suala la kuwapo kwa midahalo kwa wagombea wa ngazi zote. 

“Midahalo itawezekana ikiwa yatafanyika marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2024 ili kuweka takwa la ulazima wa kufanya midalo ya wagomebea katika ngazi zote,” amesema Henga.

Amesema uwepo wa midahalo hiyo itasaidia watu kujua kwa urahisi nani anasimamia sera gani mbali na kampeni watakazozifanya.

Kuhusu hayo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Abbas Mwalimu amesema huenda kwa sasa midahalo isiwe na nguvu kutokana na kuwapo kwa mikutano ya vyama vya siasa na badala yake alivishauri vyama kujikita katika kufanya utafiti kujua maeneo ambayo wakija na hoja wanaweza kushindana na chama kilichopo madarakani.

“Wanapofanya utafiti na kubaini mambo mbalimbali basi wajitahidi kutoa matokeo yake kwa lugha nyepesi, ili wananchi waweze kuelewa zaidi pia vyama vijikite katika kujenga mitandao yake wananchi waelewe itikadi, falsafa na kujua chama kinasimamia nini,” amesema Mwalimu.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF, Mohamed Ngulangwa amesema ikiwa watu watakuwa huru kufanya kampeni na wananchi kuwa na uelewa mpana wa kusikiliza mikutano hiyo itatosha kufikisha sera kwa wananchi na kuondoa ulazima wa midahalo.

Wafungwa, Diaspora kupiga kura

Henga alipowasilisha matokeo ya uchambuzi huo pia walitaka ujumuishaji wa wapiga kura kugusa makundi yote kwanza kwa Serikali kutekeleza maamuzi ya Mahakama Kuu katika shauri la Tito Elia Magoti dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyowapa wafungwa haki ya kupiga kura.


“Tunaona kuwa makundi mbalimbali yametengwa ikiwemo wafungwa hivyo ni wakati wa kutekeleza hili,” amesema Henga.

Kwa wanaoishi nje ya nchi, Henga amesema ni wakati sasa wa serikali kutekeleza makubaliano yake na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria juu ya suala la Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) kupiga kura.

“Hili lina mashiko, lakini haikuwa tayari kulifanya suala hili kuwa la kisheria. Hivyo LHRC inaikumbusha Serikali kurejea makubaliano yake na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria,” amesema Henga.

Mkurugenzi wa Tanzania Diaspora, Kelvin Nyamori alipozungumza na Mwananchi Digital ameitaka Serikali kujipanga na kuangalia namna inavyoweza kuwapa fursa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika uchaguzi wa mkuu mwaka 2025.

“Katiba inasema ni haki ya mtu kuchagua au kuchaguliwa, tunashangaa kwanini haki hii inakwamishwa na kucheleweshwa, nafikiri Tume ingeanza kujipanga kwa kuanza kufanya usajili wa wapiga kura katika maeneo tofauti, ili kuwapa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa sababu hakuna kinachoshindikana,” amesema Nyamori.

Mgombea binafsi

Henga amesema suala la mgombea binafsi ni jambo lililoachwa katika sheria hizo licha ya kuwepo kwa uamuzi mbalimbali wa Mahakama za ndani na za kikanda zilitoa uamuzi wa kuwepo wa mgombea binafsi, lakini bado kumekuwepo na kusita kufanya maamuzi ya kurekebisha Katiba na sheria juu ya suala hilo.

Kwa mujibu wa vifungu vya 32, 55 na 60 vya sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabune na Madiwani 2024, moja ya sifa ya mtu kuchaguliwa katika nafasi hizo ni lazima awe ametokana na chama cha siasa. 

“Hii inathibitisha kutochukuliwa kwa maoni ya wadau tuliotaka uwepi wa mgombea binafsi, licha ya LHRC na wadau wengine kuendekeza mabadiliko madogo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 katika ibara za 67(0) (b) na 39(1) (c), ili kuruhusu uwepo wa mgombea binafsi, lakini bado Serikali haijafanyia kazi,” amesema Henga. 

Amesema uwepo wa mgombea binafsi utachochea ukuaji wa demokrasia na kuongeza wigo wa Watanzania kuwa na haki ya kuchaguliwa bila kulazimika kupitua mkondo wa vyama vya siasa. 

Mwaka 2011 mwanasiasa, Christopher Mtikila (sasa marehemu) akishirikiana na LHRC walishirikana kutetea suala la wagombea binafsi katika Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR).

 Katika mahakama hiyo, waombaji waliitaka mahakama itoe tamko kuwa Serikali ilikiuka Ibara ua 2 na ya 13 (1) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na watu kwa kufanya marekebisho ya Katiba yaliyozuia wagombea binafsi.

Pia waliitaka mamlaka itoe amri ya kuitaka Serikali ichukue hatua za kikatiba na kisheria kuhakikisha haki za binadamu zilizo chini ya Ibara ya 2 na ya 13 (1) ya Mkataba wa Afrika wa haki za Binadamu na Watu na zile za 3 na 25 za mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia (ICCPR) zinazotekelezwa.

Kwa mujibu wa Mtikila, Katiba ya Tanzania ilikiuka haki yake ya kuungana na wenzake kushirikia katika shughuli za utawala wa nchi kwa kuzuia wagombea binafsi kugombea urais, ubunge na nafasi za Serikali za mitaa.

Kufuatia suala hilo, Julai mwaka 2013 Mahakama ya AfCPHR iliilekeza Tanzania kuchukua hatua za kikatiba, kisheria na hatua nyingine zote muhimu ndani ya muda stahiki ‘kutibu’ ukiukwaji wa haki za binadamu kama ilivyoainishwa na iijulishe mahakama hiyo hatua zilizochukuliwa.

Matumizi ya teknolojia

Henga alisema LHRC na wadau wengine wa demokrasia walipendekeza matumizi ya teknolojia katika mchakato wa uchaguzi kwenye hatua zote yaani uandikishaji, uchukuaji na uwasilishaji wa fomu za uteuzi wa wagombea, upigaji kura na kutangazwa kwa matokeo.


“Kifungu cha 166 kinachoweka takwa la matumizi ya teknolojia kuwa hiari ambapo LHRC na wadau wengine tulipendekeza matumizi ya teknolojia kwa mujibu wa kifungu hicho kuwa lazima, lakini baada ya kupitia sheria tumebaini kifungu hiki kimebaki kama kilivyo,” amesema Henga.


Katika hilo, Mtaalamu wa Tehama na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Jabhera Matogoro amesema ikiwa jambo hilo litaafikiwa muda uliobaki unatosha kufanya maandalizi yote ya matumizi ya teknolojia katika uchaguzi mkuu ujao.


“Kikubwa kinachopaswa kufanyika ni kujenga imani kwa watumiaji, wajue kwanini zoezi hili linakwenda kufanyika kwa haraka, zoezi likiwa la uwazi jambo hilo linawezekana,” amesema Dk Matogoro.


Vyama vya siasa

Katika hoja zote zilizotolewa, Mwenyekiti wa Vyama vya Siasa, Ally Khatib amesema kilio chao kikubwa kilikuwa ni sheria tatu zilizosainiwa na sasa kilichobaki ni kuwekwa sawa uwanja wa siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

“Kilio chetu kimesikilizwa, kilichobaki ni kuweka sawa uwanja wasiasa kuhakikisha vyama vinapata ruzuku, ili kila mtu afanye kampeni kwa usawa, sisi ndiyo tunajua tulichokuwa tunataka, tunachokipigania imani yetu hayo mengine yatafanyiwa kazi wakati utakapofika,” amesema Khatib.