Haya hapa mapendekezo maboresho sheria za demokrasia

Mkurugenzi MKuu wa LHRC, Anna Henga. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  nchini (LHRC), kimefanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya kuboresha miswaada ya sheria zilizowasilishwa bungeni ziku chache zilizopita, ikiwamo kuondoa uhalali wa watumishi wa umma kusimamia chaguzi na ushindi wa kiti cha urais uwe zaidi ya asiliamia 50.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimefanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya kuboresha miswaada ya sheria zilizowasilishwa bungeni ziku chache zilizopita ikiwamo watumishi wa umma kutosimamia uchaguzi.

Novemba 10, mwaka huu Serikali iliwasilisha kwa mara ya kwanza muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria  za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2023.

Hata hivyo, akizungumza na wanahabari leo Novemba 21, 2023 jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema kwa ujumla miswaada hiyo iondoe uhalali wa watumishi wa umma kusimamia chaguzi.

Amefafanua kuwa  mshindi wa kiti cha urais atangazwe baada ya kupata kura zaidi ya asilimia 50  ili kumjengea uhalali wa kuchaguliwa na idadi kubwa ya wananchi anaowaongoza.

Pia amesema Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutokuwa na uhalali wa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwepo chombo cha usimamizi wa migogoro katika vyama vya siasa.

Mbali na hilo, LHRC inapendekeza uwepo wa midahalo ya wagombea urais ili kuwasikiliza kwa pamoja kabla ya kuingia kwenye kampeni.

Kuhusu uhalali wa watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Anna amesema badala ya kutumia wakurugenzi wa halmashauri, Serikali itangaze maombi ili kila mwenye sifa aombe.

“Wakishaomba, uchambuzi ufanyike kuwachuja ili kuwabaini watakaokuwa na uhalali wa kusimamia chaguzi, kwa sababu inawezekana sio rahisi kupata wenye sifa kwa  kuwaona kwa macho,”amesema Anna.

Kuhusu uamuzi wa Serikali kuwasilisha muswada unaokinzana na uamuzi wa Mahakama wa kutotumia wakurugenzi katika chaguzi hizo, Anna amesema wanasubiri mpaka sheria zitakapokamilisha.

“Tunasubiri sheria ikipitishwa ndio tunakwenda kuipinga mahakamani, kwa sasa huwezi kupinga muswada,”amesema.