Linyama wa ‘Ndugu abiria’ ashinda kesi, kulipwa Sh150 milioni

Muktasari:

  • Kampuni ya udalali ya Dexter Insurance kumlipa dereva wa Kampuni ya New Force, Waubani Linyama maarufu kwa jina la 'Ndugu abiria', fidia ya Sh150 milioni kwa kosa la kutumia picha yake kibiashara bila idhini yake.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imeiamuru Kampuni ya udalali ya Dexter Insurance kumlipa dereva wa Kampuni ya New Force, Waubani Linyama maarufu kwa jina la 'Ndugu abiria', fidia ya Sh150 milioni kwa kosa la kutumia picha yake kibiashara bila idhini yake.

Pia mahakama hiyo leo Agosti 10, imetoa zuio la kudumu dhidi ya kampuni ya udalali ya Dexter Insuarance kutoendelea kutumia picha ya Linyama kwenye matangazo yao ya biashara.

Linyama akiwakilishwa na wakili wake, Ferdinand Makore alifungua kesi katika mahakama hiyo akiomba kampuni hiyo ya bima imlipe fidia ya Sh200 milioni kwa kuituma picha ya mdai huyo kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kujipatia faida au biashara.

Amedai kuwa kampuni hiyo iliandika kwenye ukurasa wake wa Instragram ujumbe uliosema, “Tangazo Tangazo ndugu abiria msiwe na wasiwasi basi letu lina bima ya Dexter Insuarance.”

Dereva wa kampuni ya magari ya New Force, Waubani Linyama maarufu kama Ndugu abiria (kushoto) akiwa na wakili wake, Ferdinand Makore baada ya kutoka kwenye chumba cha Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Picha na Pamela Chilongola

Alisema kwa tangazo hilo kampuni hiyo ilimgombanisha na mwajiri wake yaani kampuni ya New Force kwa kumwaminisha kuwa aliingia mkataba na kampuni nyingine.

Akitoa uamuzi huo Hakimu Mkazi, Erick Rwehumbiza amesema katika shauri lililofunguliwa na Linyama aliomba alipwe fidia ya Sh 200 milioni na kampuni hiyo ya udalali kwa kutumiwa picha yake kufanya biashara.

"Ktendo cha kampuni hiyo kutumia picha ya mdai kutangaza biashara na kupata faida ameingilia faragha bila ya ridhaa yake," amesema Rwehumbiza.

Amesema kutokana na hilo mahakama hii imeamuru kampuni hiyo kumlipa Linyama fidia ya  Sh150 milioni kwa kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii kwenye ukurasa wa Instagram  Kwa lengo la kufanyia biashara na kupata faida.

Rwehumbiza amesema pia mahakama hiyo imeamuru kampuni hiyo kila siku inatakiwa kutoa asilimia saba kama riba ya kimahakama siku maamuzi yalipotolewa kuanzia Agosti 10, 2022 hadi mdai atakapolipwa na kampuni hiyo gharama ya Sh150 milioni.

"Mdai anatakiwa arudishiwe gharama alizotumia kwenye kesi hii," amesema Rwehumbiza.

Hakimu huyo amesema, Linyama alyeleta madai yake hayo Julai 16, 2021, ni mwajiriwa wa kampuni ya mabasi ya New Force na picha hiyo iliyosambaa mitandaoni alipigwa mwaka 2019 akiwa anaendesha gari akitokea Sumbawanga kuja Dar es Salaam.

Alipigwa akiwa Mafinga akizungumza kupitia kipaza sauti (microphone) akiwaelezea abiria kuwa atapumzika ili abiria wapate chakula.

"Wakati huo dereva msaidizi, Farahan Kondole alimpiga picha Kwa makubaliano lakini hiyo picha iliwafikia kampuni ya Dexter Insurance wakitumia kwa matangazo yao bila ylya kuhusisha na ikasababisha usumbufu Kwa mwajili wake," alisema Rwehumbiza.