Lishe ina uhusiano na afya ya akili

Lishe ina uhusiano na afya ya akili

Muktasari:

  • Kila ifikapo Oktoba 10 dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Akili na kwa mantiki hiyo makala yetu ya wiki hii itaangazia suala zima la lishe na afya ya akili.

Kila ifikapo Oktoba 10 dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Akili na kwa mantiki hiyo makala yetu ya wiki hii itaangazia suala zima la lishe na afya ya akili.

Moja ya athari kubwa ya utapiamlo nchini ni janga la udumavu.

Watoto waliodumaa ni wale waliokosa lishe bora katika kipindi muhimu cha ukuaji wa ubongo wa mtoto hususani siku elfu moja za mwanzo za uhai wa mtoto, kuanzia kutungwa kwa mimba.

Hali hiyo hupelekea watoto hawa kuwa na uwezo mdogo wa kiakili na hivyo kushindwa kumudu masomo, kufundishika na wanapokuwa watu wazima kutokuwa na nguvu hivyo kushindwa kuzalisha kwa tija katika uchumi, kwa kuwa madhara ya udumavu hayarekebishiki.

Kwa mujibu wa takwimu za hizi karibuni kupitia Utafiti wa Hali ya Lishe nchini uliofanyika kwa kutumia Methodolojia ya SMART (Tanzania National Nutrition Survey – TNNS 2018), takribani watoto milioni 2.6 sawa na asilimia 31.8 ya watoto wote Tanzania wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa. Kwa lugha nyingine, watoto 3 kati ya 10 nchini Tanzania hivi sasa ni wadumavu.

Kwa mujibu wa takwimu za TNNS 2018, Mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa zaidi ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 na wenye udumavu ni Njombe asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9, Iringa asilimia 47.1, Songwe asilimia 43.3, Kigoma asilimia 42.3 na Ruvuma ina asilimia 41.0.

Ili tuhakikishe akili ya mwanadamu inakuwa vizuri na kufikia kiwango kinachostahili ni lazima jitihada zifanyike kuhakikisha tangu akiwa tumboni mwa mama yake hadi anazaliwa na kufikisha umri wa miaka miwili anapata lishe bora na hizi ndio zile siku elfu moja nilizosema hapo juu.

Lishe bora inayotakiwa hapa ni kula vyakula venye virutubisho vyote na hii inatakiwa kuanzia mwanamke akiwa mjamziko, mama anaponyonyesha hadi mtoto apoanza kula vyakula vya nyongeza hadi pale anapofikia miaka miwili. Kwa kurudia tu hiki ni kipindi nyeti sana maana ndipo ubongo unapojitengeneza.

Moja ya hatari kubwa ya kutotilia maanani kipindi hiki ni mtoto kuzaliwa na udumavu. Mbaya zaidi udumavu wa akili huwezi kuujua kwa macho ya kawaida ya mwanadamu bali unaweza kuona ishara ya athari zake kwa kutathmini maeneo mbalimbali. Kwa mfano, mtoto aliyedumaa hupoteza hadi pointi kumi za IQ (kipimo cha uwezo bora wa akili) na hii inawaathiri hadi wanapokuwa watu wazima, kwa sababu huwa katika kiwango cha theluthi moja cha kutoweza kuepukana na umasikini. Mbaya zaidi, hii inamaanisha kwamba watoto wetu wengi wanakabiliwa na changamoto za udumavu hawatafundishika.

Vile vile, uwezekano ni mkubwa wa watoto hawa kushindwa kumudu ushindani wa kuendana na kasi ya maendeleo katika dunia ya utandawazi na mapinduzi ya nne ya viwanda kutokana na uwezo mdogo wa kufikiri, kushindwa kuwa wabunifu na kutumia vizuri fursa za maendeleo ya teknolojia.

Ili kuhakikisha ukuaji wa ubongo wa watoto unakuwa kama ambavyo inastahili;



1. Mtoto akiwa chini ya umri wa miezi sita anatakiwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee yake. Kwa takwimu za TNNS 2018, bado asilimia 40 ya watoto wa umri huu hawanyonyeshwi ipasavyo.

2. Mtoto akishafika umri wa miezi sita hadi miaka miwili anapaswa kuanza kupata chakula cha nyongeza ili aweze kuendelea kukua vizuri. Takwimu za TNNS 2018, zinaonyesha takribani asilimia 69 ya watoto chini ya umri wa miaka miwili hawapati angalau kiwango cha wastani wa lishe kinachokubalika