Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu aibwaga Jamhuri sakata la mashahidi fiche

Muktasari:

  • Mahakama imekubaliana na hoja moja kati ya tano za Lissu kuhusu muundo wa kizimba hicho, huku ikizikataa hoja nyingine nne na kuamuru kesi iendelee.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeelekeza kufumuliwa na kurekebishwa kwa kizimba maalumu cha ushahidi kilichopangwa kutumiwa na mashahidi wa Jamhuri waliopewa ulinzi katika kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu.

Mahakama hiyo imetoa maelekezo hayo leo, Jumatano, Februari 11, 2026 katika uamuzi wake uliotokana na pingamizi la Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuhusiana na muundo wa kizimba hicho, matumizi yake na uhalali wa mashahidi hao kupewa ulinzi huo.

Kati ya hoja tano za pingamizi hilo alizowasilisha Lissu, mahakama imekubaliana na hoja moja, yaani muundo wa kizimba hicho, huku ikizikataa sababu na hoja zake nyingine nne ikisema hazina mashiko.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kikinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana...”

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, pamoja na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Novemba 12, 2025, Lissu aliweka pingamizi dhidi ya shahidi wa nne wa Jamhuri, ambaye ni miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri waliopewa ulinzi.

Mashahidi hao ni raia wa kawaida (wasio askari) ambao Mahakama Kuu iliamuru wapewe ulinzi kufuatia maombi ya Jamhuri kwa madai kuwa wamekuwa wakitishiwa usalama wao.

Mahakama hiyo, katika uamuzi uliotolewa na Jaji Hussein Mtembwa Agosti 4, 2025, ilielekeza majina ya mashahidi hao yasitajwe, wala anuani za makazi yao au taarifa zitakazowafanya watambulike wao, familia zao au watu wao wa karibu.

Pia ilizuia kusambazwa kwa maelezo yao au nyaraka zozote zinazowahusu zinazoweza kusababisha wakatambulika bila idhini ya mahakama, huku pia ikielekeza kutumia majina bandia wakati wote wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Jamhuri ilipeleka mahakamani hapo maombi ya ulinzi wa mashahidi hao chini ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za Mwaka 2025, zilizotungwa na Jaji Mkuu kwa mujibu wa kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Hata hivyo, siku hiyo Lissu alimpinga shahidi huyo aliyetambulishwa kwa jina la P11, akipinga kutumia kizimba maalumu ambamo haonekani, huku pia akipinga uhalali wake pamoja na mashahidi wengine wa aina hiyo kuwa mashahidi waliopewa ulinzi huo.


Hoja za pingamizi, mahakama ilivyoziamua

Mosi, Lissu alidai kizimba cha ushahidi hakiendani na maelekezo ya kanuni ya 3 ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi.

Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa kanuni hiyo, kizimba kinatakiwa kuiwezesha mahakama, jaji au hakimu kumuona shahidi, lakini akadai katika kizimba kilichotengenezwa hata majaji hawawezi kumuona shahidi huyo.

Pia alidai Jamhuri, katika maombi yake ya ulinzi wa mashahidi, haikuomba matumizi ya kizimba maalumu na mahakama haikuelekeza hivyo.

Akiamua hoja hiyo, Jaji Ndunguru amekubaliana na hoja ya Lissu kuwa kizimba hicho hakikidhi matakwa ya kanuni ya 3.

Amesema hata kama si kwa matakwa ya kuibua pingamizi hilo, mahakama hiyo, kwa kukiona jinsi kilivyo, ingeweza kuliona hilo kwamba hakikidhi matakwa ya kanuni.

“Kwa kuzingatia namna kilivyojengwa kizimba hiki, hakikidhi matakwa kwani mahakama haiwezi kumuona shahidi, jambo linalofanya ishindwe kutathmini tabia ya shahidi,” amesema Jaji Ndunguru.

Amesema ingawa mshtakiwa alidai hakipaswi kutumika, mahakama inakubaliana na Jamhuri kuwa kizimba maalumu kinapaswa kutumika kwa mashahidi waliopewa ulinzi.

“Hivyo mahakama inaelekeza kizimba hiki kirekebishwe ili kikidhi kanuni ya 3, kwamba shahidi anapokuwa katika kizimba hicho mahakama imuone.”

Katika hoja ya pili, Lissu alidai shahidi huyo na wengine hawajapewa ulinzi kwa kuwa hawakubainishwa katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani.

Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 5(1) ya kanuni hizo, mahakama inaweza kutoa amri ya ulinzi iwapo itaridhika kuwa mtu aliyebainishwa katika maombi ni shahidi katika shauri husika na maisha yake au usalama wake uko hatarini.

Alidai mtu aliyebainishwa ni yule aliyetajwa, lakini akadai kuwa katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani, katika viapo vyote viwili vilivyoungwa mkono maombi hayo, hakuna hata kimoja kilichotaja jina la shahidi, wala waliokuwa wanawatishia na hata aina ya vitisho.

Hata hivyo, mahakama imeikataa hoja hiyo ikisema kanuni imesema tu kuwa anayeombewa ulinzi atabainishwa kwenye maombi.

Jaji Ndunguru amesema kanuni hiyo haitamki moja kwa moja kuwa wanatakiwa kutajwa majina.

Amefafanua kuwa mahakama imepitia amri ya ulinzi huo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alibainisha kuwa wanaoombewa ulinzi ni mashahidi ambao ni raia, na amri hiyo ilitolewa kwa mashahidi hao tu.

Katika hoja ya tatu, Lissu alidai katika amri ya ulinzi wa mashahidi hao, mahakama haikuamuru matumizi ya kizimba maalum na kwamba hata upande wa mashtaka hawakuwa wameliomba.

Mahakama imesema imeangalia katika maombi ya ulinzi wa mashahidi, yanabainisha walindwe wakati wa mwenendo kabidhi na wakati wa usikilizwaji, na kwamba mahakama iamuru kutokuwekwa wazi kwa taarifa za utambuzi wa mashahidi hao.

Jaji Ndunguru amesema mahakama imejiuliza kama amri ya ulinzi imeshatolewa, walindwe vipi?

Amesema katika mazingira hayo mahakama imeona kuwa uwepo wa kizimba hauwezi kuepukika kwa sababu shahidi anakuja mahakamani, lazima kuwepo namna ya kumlinda, na kama mahakama ilivyosema, imeelekeza kurekebishwa kwa kizimba hicho ili mahakama iweze kumuona.

Amesema pia kanuni hizo, zilivyotengenezwa na Jaji Mkuu, zimezingatia kuwepo kwa kizimba kama namna ya ulinzi wa mashahidi hao.

“Kanuni ya 8 inasema mahakama inaweza kurekebisha namna ya ulinzi kulingana na mazingira; ndiyo maana mahakama imesema kizimba hicho kiendelee kutumika kwa namna ilivyoelekezwa kwenye kanuni ili mahakama iweze kumuona,” amesisitiza Jaji Ndunguru.

Lissu, katika hoja ya nne, alidai kuwa matumizi ya kizimba maalumu yanaathiri haki yake ya kusikilizwa kwa usawa, kwani hataweza kumhoji maswali ya dodoso, akidai kuwa ni kinyume na kanuni ya 6(2) na 5(f) ya kanuni hizo.

Mahakama katika uamuzi wake imesema ilitafakari kwa makini hoja hiyo, lakini ilishindwa kuona namna gani mshtakiwa atashindwa kumhoji shahidi huyo kwa kuwa ndani ya kizimba.

Tano, Lissu alidai Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Namba 2), Namba 7 ya Mwaka 2018, iliyoanzisha kifungu cha 194 cha CPA kinachozungumzia ulinzi wa mashahidi, haijawahi kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Alidai kifungu cha 14 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria kinasema ili sheria ianze kutumika lazima iwe imechapishwa kwenye Gazeti la Serikali na kwamba itaonekana katika tovuti na maktaba za ofisi mbalimbali za Serikali, lakini huko kote haipo.

Vilevile, alidai kuwa kanuni hizo haziwezi kutumika katika kesi yake kwani zilitungwa na kuanza kutumika Julai 11, 2025, wakati tayari kesi yake hiyo ilikuwa imeshaanza tangu Aprili 10, 2025.

Katika hoja hiyo, mahakama imesema kuwa ingawa Jamhuri ilijibu kuwa sheria za kiutaratibu zinaweza kutumika hata kwa kurudi nyuma, imekubaliana na mshtakiwa kuwa ni pale tu ambapo haitakiuka haki za mshtakiwa.

Amesema mahakama ilikwenda mbali kuangalia kama kweli kanuni hizo zilitungwa baada ya kesi hiyo kuanza.

Jaji Ndunguru amefafanua kuwa kanuni hizo zimetungwa na Jaji Mkuu mwaka 2025 chini ya kifungu cha 194(3) cha CPA, lakini sheria ya ulinzi wa mashahidi ilikuwepo tangu mwaka 2018.

“Kwa hiyo, hatuwezi kusema kuwa sheria hiyo haikuwepo wakati kesi yake inaanza Aprili 2025, pia sheria haiwezi kukosa kufanya kazi kwa sababu kanuni hazipo,” amesema Jaji Ndunguru na kusisitiza:

“Hivyo hata kama kanuni zisingekuwepo, sheria kifungu cha (3) kimeweka wazi namna ulinzi wa mashahidi unavyofanyika, labda kama kifungu kingesema hakitafanya kazi mpaka kanuni zitungwe. Hivyo kifungu hiki kimekuwepo hata kabla ya kesi hii.

Kuhusu sheria ya marekebisho ya sheria hiyo kutotangazwa, Jaji Ndunguru amesema kuwa Jamhuri walitoa nakala ya Gazeti la Serikali lenye tangazo la sheria hiyo jana wakati wakijibu hoja za Lissu.

“Kwa hiyo, mahakama inaona ni pingamizi la kwanza tu ambalo limekubaliwa kwa kiasi hicho, na mengine manne yamekataliwa. Hivyo kesi itaendelea kusikilizwa kwa kuzingatia kanuni ya 3 baada ya kufanya marekebisho kuhakikisha kuwa shahidi anayekuja mahakamani mahakama inamuona.”

Mahakama imeelekeza kesi hiyo iendelee kusikilizwa kesho, Alhamisi, huku ikiamuru Jamhuri ipeleke mashahidi wa aina zote walio chini ya ulinzi na wasio chini ya ulinzi ili, kama marekebisho ya kizimba cha mashahidi wenye ulinzi yatakuwa hayajakamilika, waendelee na mashahidi wasio chini ya ulinzi.