Lowassa: Asiyenipenda CCM ahame

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, nyumbani kwake, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Asema hawezi kamwe kukihama, ajibu maswali kuhusu afya yake, kashfa ya Richmond, utajiri, ajira na hali ya kisiasa nchini

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.

Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.

Kuhama CCM

Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.

“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.

Kimya miaka saba

Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.

“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza, askofu mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu. Nilichagua kuwa kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza, ningezungumza ningeweza kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo ambayo hayapo.

“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake.... sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Wagombea wapime afya

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.

“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.

“Twendeni tukapime tuone nani mgonjwa. Tuonane kwenye uwanja wa mapambano katika mchakamchaka wa maendeleo, ninajua nitawashinda kwa mbali,” alisema.

Sakata la Richmond

Kuhusu sakata la Richmond, ambalo lilimfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alisema tatizo kubwa halikuwa kuhusu mitambo hiyo ya umeme ila uwaziri mkuu.

“Ajenda haikuwa kuhusu Richmond, ila uwaziri mkuu ndiyo maana niliwaachia. Tunajifunza  nini katika hilo, wakubwa wawili wa Marekani, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (Hillary) Clinton na Rais wake (Barack) Obama, wote wamekuja Tanzania na wamethibitisha kuwa ile mitambo ni mizuri. Lakini jingine tulilojifunza katika ubishi ule umeisababisha nchi hasara ya Dola 120 milioni,” alisema Lowassa.

“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni kutaka kuvunja mkataba wa Richmond nikaita wataalamu, nikawaelezea kuhusu habari za magazeti kuwa zinasema hawa jamaa (Richmond) hawana fedha, hebu angalieni, nikaita wataalamu na mwanasheria mkuu, nikawaambia kuna hii habari kuweni makini, pamoja na hayo nikaweka kwa maandishi kwa mwanasheria mkuu, pia kulikuwa na timu ya mashauriano ya Serikali iliyokuwa chini ya makatibu wakuu nao walikuwa na vikao vyao, ilikuwa inaongozwa na (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Gray Mgonja) nao wakakutana chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa uamuzi ambao sina haja ya kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola 120 milioni.

“Nilipotaka mkataba uvunjwe nilikuwa nimetoa uzoefu wangu kwani kabla ya kuwa waziri mkuu nilikuwa nimekuwa waziri wa maji na mifugo ambako nilivunja mkataba wa kampuni ya Kiingereza iliyokuwa imewekeza katika mradi wa maji Dar es Salaam ya City Water.

“Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa tukagundua hawa jamaa (City Water) ni matapeli…tulifanya kikao saa tisa alasiri, tukachukua kibali cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na tukamfukuza akaondoka siku hiyohiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa tisa alasiri ili asiende mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia muda huo ili asije kwenda kupata zuio.

Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”

Elimu au kilimo kwanza?

Akizungumzia kuhusu kupingana na kaulimbiu ya Serikali ya ‘Kilimo Kwanza’, Lowassa alisema ataendelea kushikilia msimamo huo kwa sababu elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya mwanadamu.

“Mimi sikubaliani na wenzangu wanajua, sikubaliani na kilimo kwanza, naamini ‘elimu kabla, kilimo kwanza baadaye’. Tukitaka nchi yetu ipige hatua ni lazima tuwekeze katika elimu... Nchi zote za mashariki ya mbali waliwekeza katika elimu, kuna shule za kata hazina walimu, lazima tuwekeze kwenye elimu ili tujikomboe,” alisisitiza.

Ajira kwa vijana

Kuhusu ajira kwa vijana, Lowassa alisema bado anaamini kuwa hilo ni bomu ambalo lisipopatiwa majibu litapasuka. “Wakati ule nilisema hilo, waziri mmoja akanishambulia akinipinga akisema takwimu zangu si sahihi na hakuna tatizo, lakini bado mimi naamini kuna tatizo kubwa.

“Machafuko ya Afrika Kaskazini yalitokana na vijana kukosa kazi, haiwezekani vijana wamalize chuo kikuu, kidato cha sita na vyuo vingine wakarudi mitaani kwa sababu hakuna kazi, hilo ni jambo gumu.

“Duniani kote wakati wa uchaguzi lazima wagombea waseme watatengeneza ajira ngapi, hata Obama alipogombea kwa mara ya pili alishinda kwa sababu alitengeneza ajira kwa vijana.

“Tunaweza kutumia gesi tuliyonayo kukopa fedha na kuanzisha ajira kwa vijana kwa kuwapa mashamba wakalima michikichi. Tuwekeze maeneo ambayo yataleta ajira kwa vijana. Ukiniamsha usingizini uniulize kipaumbele changu nitakwambia ajira, ajira, ajira,” alisema.

Urafiki na JK

Alipotakiwa kuzungumzia uhusiano wake na Rais Jakaya Kikwete, Lowassa alisema hadhani kama hiyo ni ajenda. “Sidhani kama hiyo ni ajenda, acheni maneno yasiyokuwa na maana, kila mtu ana marafiki, mbona hatuwaulizi, sidhani kama kuna tatizo.” alisema kwa kifupi.

Utajiri wake

Alipoulizwa ana utajiri kiasi gani na fedha anazochangia kwenye harambee makanisani na misikitini zinatoka wapi, Lowassa alisema anatamani angekuwa tajiri, lakini anachukia umaskini.

“Tatizo siku hizi kuna maneno mengi, kila nyumba nzuri wanasema ya Lowassa. Mimi nina nyumba chache na ng’ombe kati ya 800 na 1,000. Kwetu Umasaini unapokuwa kiongozi unapewa ng’ombe ili usipate taabu kwa ajili ya kuwakarimu wageni wanapokuja wala usiwe ombaomba au usichukue rushwa. Lakini kama kuna mtu mwenye shaka na utajiri wangu aende Sekretarieti ya Maadili kule ataona kila kitu,” alisema.

“Nachukia umaskini, napenda utajiri, natafuta uongozi wa nchi hii ili kuwasaidia Watanzania kuwa matajiri na si kukumbatia umaskini. Hii kudanganya watu kwamba nikiwa maskini ndiyo nafaa kuwa kiongozi ni ujinga ambao inabidi tuuache. Nataka watu wawe matajiri, tuache kuwabeza matajiri, matajiri wawe ni mfano kwa wengine, watu kama (Reginald) Mengi, (Said) Bakhressa na (Nazir) Karamagi wanatakiwa kuwa mfano kwa wengine, tungekuwa na watu kama hawa 20,000, nchi hii ingekuwa haikopi nje. Naukataa umaskini na nauchukia umaskini. Nakataa umaskini na ninataka watu wanihukumu kwa hilo,” alisema.

Kuhusu kushiriki harambee nyingi na anakopata fedha alisema: “Sina fedha ila nina marafiki wengi, nikipata mwaliko wa kuchangia nawatafuta marafiki zangu wanachanga. Mfano ‘juzi’ nilipomwakilisha Makamu wa Rais mjini Arusha, marafiki zangu walichangia Sh100 milioni, Makamu wa Rais alichangia Sh10 milioni na watu wa Arusha wakatoa Sh100 milioni. Hizo hazikuwa fedha zangu, ila ni watu walichangia. Nafurahia kufanya harambee, harambee zangu zinasaidia misikiti, makanisa na shule, hivi ni vitu vya maendeleo ya watu, nawashauri na wabunge wafanye hivyo kwenye majimbo yao. Hata shule za kata zilichangiwa kwa harambee, tusionee aibu ni jambo jema,” alisisitiza.

Tahadhari kwa CCM

Akijibu swali kuhusu tahadhari inayotakiwa kuchukuliwa na CCM mwaka huu, Lowassa alisema upinzani umeanza kupata nguvu, nguvu kubwa mijini na vijijini.

“Sisi ni chama dola tumefanya mambo mazuri, lakini tusibweteke wenzetu wanajiandaa vizuri na sisi tunapaswa kujiandaa vizuri. Vyama vingi vilivyoleta ukombozi sehemu nyingi vimeshaondolewa mfano UNIP, Kanu na mkishaondolewa hamrudi madarakani, meseji yangu kubwa kwa chama changu tusifanye mchezo, tusibweteke badala yake tufanye kazi kubwa zaidi.”

Kulipa kisasi

Alipoulizwa kama atalipa kisasi akishinda urais, Lowassa alisema hana mpango wa kulipa kisasi kwa sababu hana kisasi.

“Siamini katika kufukua makaburi, tufanye kazi. Mimi ni Mkristo naamini katika maandiko ya Bwana Yesu, alisema samehe saba mara sabini. Tuchape kazi.”

 Kukataliwa na Nyerere

Alipoulizwa kama kweli Mwalimu Julius Nyerere amewahi kumkataa alisema jambo hilo si la kweli. “Jambo hili si la kweli, sijawahi kukataliwa.”