Lowassa atoa msimamo Richmond, aahidi meli iliyomshinda JK, Mkapa

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa akihutubia wananchi wa Bukoba Mjini kwenye mkutano wa kampeni mkoani Kagera jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Gymkhana mjini Bukoba na kuwataka Watanzania watakaoulizwa jambo lolote kuhusu Richmond wawajibu kwa kusema, “acha fitna na uongo namchagua Lowassa”.

Kagera. Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amewashukia wanamhusisha na sakata la Richmond na kusema, “Siwajibu ng’o” na kupeleka jukumu hilo kwa wananchi akiwataka wawajibu kwa kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 25, mwaka huu awe Rais wa Awamu ya Tano.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Gymkhana mjini Bukoba na kuwataka Watanzania watakaoulizwa jambo lolote kuhusu Richmond wawajibu kwa kusema, “acha fitna na uongo namchagua Lowassa”.

Si mara ya kwanza kwa waziri huyo mkuu wa zamani kukataa kuzungumzia sakata hilo, na inapotokea kulizungumzia amekuwa akieleza kuwa alijiuzulu kisiasa kuilinda Serikali ya CCM na kwamba ushiriki wake ulitokana na maagizo kutoka juu.

Jana, baada ya kukaribishwa jukwaani na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ili azungumze na wananchi, alianza kwa kumshukuru Sumaye jinsi alivyofafanua kiundani kuhusu Richmond na kuwaeleza wananchi kuwa hawezi kujibu chochote.

“Sumaye amesema vyema kuhusu Richmond. Niseme tu kuwa siogopi lolote na siwajibu ng’o na wala sina muda wa kuwajibu,” alisema Lowassa na kushangiliwa na wananchi.

Aliwataka wananchi kuwajibu katika sanduku la kupiga kura watu wanamhusisha na tuhuma hizo, kauli ambayo iliamsha shangwe na kumfanya mbunge huyo wa zamani wa Monduli kushindwa kuendelea na hotuba yake kwa dakika mbili, kutokana na wananchi kunyanyua mabango yenye ujumbe mbalimbali huku wakimshangilia.

Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu Richmond, Sumaye alisema Lowassa hausiki na aliamua kujiuzulu mwaka 2008 ili kumlinda Rais Jakaya Kikwete huku akieleza ufisadi uliotokea serikalini tangu wakati huo mpaka sasa.

Septemba 11, mwaka huu Lowassa alikataa kujibu swali aliloulizwa na mwananchi wa kijiji cha Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma lililomtaka aeleze kilichotokea kwenye sakata la Richmond akisema swali hilo “halina maana”.

Sumaye

Kwa upande wake Sumaye alisema nchi ina rasilimali nyingi lakini maendeleo yanakwenda taratibu, huku akitolea mfano jinsi nchi jirani za Kenya na Uganda zinavyopiga hatua kimaendeleo licha ya kukumbwa na machafuko ya kila aina.

“Serikali ya Ukawa haitawazuia wananchi kuuza mazao nje ya nchi, hata wananchi wa hapa Bukoba watauza kahawa Uganda. Sekta ya kilimo ndiyo chanzo cha Watanzania kuwa maskini kwa sababu haijasimamiwa ipasavyo.

“Tutajenga utaratibu wa kuwa na masoko mazuri ili wakulima wawe na uhakika wa masoko kabla ya kulima, hatutaki kubahatisha,” alisema Sumaye.

Kuhusu huduma za jamii, Sumaye alisema kupitia ilani ya Chadema na Ukawa huduma hizo zitaboreshwa na kufafanua kuwa Tanzania haiwezi kuboresha uchumi wakati huduma hizo hazipatikani.

“Huwezi kupata uchumi wakati wananchi wao wana afya mbaya, huduma za hospitali kwa watoto na wazee wanalipia, dawa hakuna, miundombinu ya afya mibovu. Hapo ni ndoto nchi kukua kiuchumi,” alisema Sumaye.

Sumaye alisema wananchi wakiamua kumchagua mtu wanayempenda hakuna wa kuwazuia, “Hivi hao (CCM) wanavyosema hakuna wa kuwatoa wao ni nani? Chama hiki kimejenga kiburi kwa kuamini kuwa kitachaguliwa tu na wananchi. Hawaingii tena madarakani safari hii maana wamewatelekeza wananchi kwa muda mrefu.”

Alisema kauli ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kusema ‘Tanzania ya Magufuli’, ni tusi kubwa kwa wananchi, huku akitolea mfano jinsi Lowassa asivyotumia kauli ya aina hiyo.