Luka Modric ang'ara na uzee wake

Friday February 19 2021
michezopic
By Mwandishi Wetu

Madrid, Hispania (AFP). Mchezaji bora wa Real Madrid kwa miezi mitatu iliyopita ana umri wa miaka 35 na mkataba wake unaisha katikati ya mwaka huu.

Pengine Luka Modric ndiye amekuwa mchezaji bora msimu huu kwa Real Madrid, pamoja na kuchaguliwa na mashabiki wa klabu hiyo kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba, Desemba na Januari. Anaweza pia kuwa wa Februari.

Hakuna mwingine katika kikosi cha Zinedine Zidane anayemzidi kwa umri na bado ni wachezaji wanne tu waliocheza kwa dakika nyingi zaidi ya Modric msimu wa mwaka 2020/21, mmojawapo akiwa kipa Thibaut Courtois.

Modric ni mmoja wa wachezaji wawili wanaoongoza kwa ufungaji katika klabu hiyo na wa tano kwa kutoa pasi za magoli, licha ya kwamba kwa tathmini yake anaona mchango wake hauwezi kuakisiwa na vipimo hivyo.

Mlinganishe Modric, kwa mfano, na Frenkie de Jong wa Barcelona, kiungo mwingine mchezeshaji, ambaye ni mdogo kwa tofauti ya miaka 12 na ambaye amekuwa na msimu mzuri.

Modric ametembea na mpira zaidi ya De Jong, kuchezewa rafu zaidi, pasi zake zimezuiwa zaidi, kupiga kiki nyingi zaidi golini, na kufunga idadi sawa ya mabao na Mholanzi huyo.

Advertisement

"Nina nia kama hiyo ya kucheza, kupigania nafasi yangu, na nataka hasa kuonyesha kuwa umri si tatizo," alisema Modric katika mkutano na waandishi wa habari mwezi uliopita.

"Kitu muhimu ni jinsi unavyocheza uwanjani na natumaini naweza kuendelea na kiwango hiki kwa miaka mingi."

Mkataba wa Modric unaisha mwishoni mwa mwezi Juni na wakati mwezi Desemba kulikuwa na taarifa zinazodai kuwa mkataba wa mwaka mmoja umekubaliwa, miezi mitatu baadaye hakuna taarifa rasmi.

Labda kuna mengi ya kufanya, hasa kwa Real Madrid, ambayo hali yake ya kifedha inamaanisha hakuna senti hata moja itabaki.

"Itakuwa kitu kizuri sana kumalizia soka langu katika klabu ya jiji hili zuri," Modric aliiambia AFP mwezi Desemba. "Lakini si uamuzi wangu. Ni wa Real Madrid, uamuzi ni wao."

Kama mkataba wake ukiachwa uishe, hakutakuwa na uhaba wa timu zinazomtaka, zikiwemo kubwa za Ulaya.

Lakini, wakati Sergio Ramos akielekea kupona majeraha, kitendo cha Madrid kusita kuongeza mkataba wake si suala la kifedha, bali ni kutuma ujumbe wa kile inachosema kuhusu kutotaka kuingia enzi mpya iking'ang'ania nyota wa enzi iliyopita.

Pamoja na yote, inakuwaje wakati wachezaji wenye umri mkubwa wanapokuwa bado ni bora kuliko wapya? Ni wakati gani mchezaji mwenye umri mkubwa anaonekana ni bora?

Luis Suarez aliondolewa na Barcelona katikati ya mwaka jana, si kwa sababu hakuwa akifanya vizuri -- alifunga mabao 21 msimu uliopita -- lakini kwa sababu klabu ilitaka kuanza ukurasa mpya.

Kwa sasa Suarez anaongoza kwa mabao katika La Liga, akiwa ameiwezesha Atletico Madrid kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi sita.

Msimamo wa Zidane kutumia wazoefu ulimsaidia kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa misimu mitatu mfululizo, lakini angalau kwa miezi michache sasa umemletea matatizo. Wakati matokeo yanapokuwa mabaya, amekuwa akikosolewa kwa kutotaka kutengeneza timu ya baadaye.

"Mwaka ujao watatakiwa kufanya mambo, labda kufanya mabadiliko," Zidane alisema mwezi uliopita. "Lakini mwaka huu tuna haki ya kupigana. Tuache tupigane."

Modric amekuwa mchezaji anayefanya vizuri katika kiungo kinachoundwa na wachezaji watatu na ambacho kinaweza kuwa chenye mizania nzuri barani Ulaya. Si Toni Kroos wala Casemiro anayeonekana anahitaji kubadilishwa.

Kwa muda mfupi, Fede Valverde alifanikiwa kujipenyeza kwa watatu hao lakini amepotea. Isco hayumo. Martin Odegaard alipelekwa Real Sociedad kwa mkopo, kwa wazo kwamba anaweza kuwa kinara wa kizazi kipya. Badala yake, Odegaard alichezeshwa kwa nadra na akaamua kujiunga na Arsenal kwa mkopo mwezi uliopita.

Wakati Odegaard akikaa benchi, alimshuhudia Modric akiongoza, akijipenyeza kwenye mianya, akipokonya mipira na kusambaza kutoka nyuma. Alimuona Modric akiikimbiza timu ya Real Madrid licha ya umri wake mkubwa, na Zidane anaona pia.

Hata kwa msimu huu wa mechi zilizobanana na unaochosha, Modric amepangwa kuanza mechi 20 kati ya 23 za Madrid, ikiwa ni kumbukumbu ya msimu uliopita.

"(Modric) Ni wa aina yake," alisema Zidane mwezi Desemba.

Jumamosi (kesho) Real Madrid inacheza na Real Valladolid, ikitegemea kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Atletico, ambao watakuwa nyumbani wakiikaribisha Levante. Barcelona, katika nafasi ya tatu, itakuwa mwenyeji wa Cadiz Jumapili.

Advertisement