Lukuvi ‘kiulaaini’, Maghembe na Mwijage moto

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Wabunge walimwagia sifa wakati wa mjadala na kumtaka awape mafunzo mawaziri wenzake

Wakati mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiendelea jana, mawaziri waliomtangulia waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi kuwasilisha bajeti zao, akiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage walijikuta katika wakati mgumu.

Mawaziri hao walijikuta katika wakati mgumu wakati Bunge lilipoketi kama kamati ya matumizi ya Bunge zima, Profesa Maghembe na Mwijage, walikutana na moto wa wabunge kushika shilingi ya mshahara wa waziri wakihitaji majibu.

Wizara nyingine ambazo ziliibua mijadala yenye hisia na mvutano wakati wa kamati ni pamoja na ya ofisi ya Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na ile ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Lakini tangu kuwasilishwa kwa hotuba ya Lukuvi na wabunge kupata fursa ya kujadili hotuba hiyo, kulianza kuonekana dalili za wazi kwa bajeti hiyo kupita kilaini kutokana na pongezi za wabunge.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema utendaji wa kazi wa Lukuvi na Naibu wake, Angelina Mabula unapaswa kuwa mfano kwa mawaziri wengine wa Serikali, akisema hakika wanastahili pongezi.

“Na mimi nishauri mheshimiwa mwenyekiti. Hizi pongezi ambazo mheshimiwa Lukuvi anapewa na wengine nafikiri kama mawaziri wengine nao akajifunza kutoka kwa mheshimiwa Lukuvi,”alisema.

“Anapokea simu (Lukuvi) na naibu wake wanakusikiliza, wanakupa majibu, wanatembelea majimbo na kama jambo haliwezekani watakuambia hili haliwezekani kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai (Chadema), alisema angeonekana ni mchawi kama asingempongeza Waziri Lukuvi.

“Na mimi naomba nisiwe mchawi, nimpongeze sana mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu wake kwa kweli ni Wizara ambayo inafanya kazi bila itikadi za kisiasa na inasimamia wajibu wake,”alisema.