Lulu afunga ndoa na Majizo akimaliza kejeli

Wednesday February 17 2021
lulupic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu na mfanyabiashara Francis Ciza maarufu Majizo wameweka rekodi jana baada ya kufunga ndoa kwa siri tofauti na ilivyozoeleka kwa watu wenye majina kama wao.

Licha ya kuwapo kwa tetesi tangu juzi lakini ni watu wachache sana waliokuwa wanajua wapi ndoa hiyo itafungiwa na muda.

Ni mpaka mchana wa jana ndipo wengi wakaanza kujua kuwa ndoa hiyo itafungwa katika Kanisa la Mtakatifu Gasper la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

ulupicccmajizo

Majizo ambaye ni mkurugenzi wa televisheni ya TVE na Redio ya EFM amemuoa Lulu miaka miwili tangu alipomvalisha pete ya uchumba. Lulu alivalishwa pete hiyo miezi mitatu tangu alipotoka jela, Novemba 12 mwaka 2018.

Lulu anaingia kwenye ndoa huku akiendelea kuilinda hadhi yake ya usanii tofauti na ilivyo kwa baadhi ya manguli wenzake kama vile Wema Sepetu, Hamisa Mobeto, Aunt Ezekiel, Jaqueline Wolper na Kajala Masanja. Pamoja na misukosuko aliyopitia miaka ya hivi karibuni, mvuto wa Lulu haujapotea kwa mashabiki wake.

Advertisement

Ustaa katika umri mdogo

Katika safari yake ya maisha mpaka familia, Lulu amepitia misukosuko lukuki. Lulu alianza kujulikana akiwa na umri mdogo alipoanza kuigiza hivyo amekua na ustaa wake uliomfanya wakati fulani ajitumbukize katika matukio ya ajabu ikiwamo kupiga picha za nusu utupu.

Katika mwendelezo wa matukio hayo, mwaka 2012 alijikuta katika mikono ya dola baada ya kuhusishwa na kumuua bila kukusudia msanii mwenzake wa filamu, Steven Kanumba aliyekuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.

Lulu alituhumiwa kumuua Kanumba Aprili 7 mwaka 2012 huko Sinza Vatican jijini Dar es Salaam. Kesi yake ilisikilizwa mpaka Novemba 2017 alipohukumiwa kifungo cha miaka miwili jela lakini Mei 2018 akabadilishiwa adhabu na kutumikia kifungo cha nje.

Katika utekelezaji wa adhabu hiyo, Lulu alikuwa akifanya usafi katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam mpaka Novemba 12 alipoimaliza.

Ajitofautisha na wengine

Mara tu baada ya kumaliza kifungo, Lulu alibadilika kimaisha, akitamka na kuimba nyimbo za injili mara kadhaa na kupunguza marafiki wa kujirusha naye maeneo mbalimbali kama ilivyokuwa kabla hajahukumiwa kifungo jela.

Hata alipohudhuria shughuli zilizowahusisha wasanii wakubwa wa kariba yake, mara nyingi Lulu alionekana kuwa mtulivu tofauti na awali ambapo akiwa mahali ilikuwa lazima ijulikane.

Utulivu huo ulimwezesha kuhimili tuhuma za mara kwa mara kutoka kwa Florah Mtegoa, mama mzazi wa marehemu Kanumba ambapo hivi karibuni alionyesha wazi kuwa hawezi kumsamehe kwa kuwa ndiye aliyemuua mtoto wake huku yeye akiendelea kuponda raha.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Lulu alisema asingependa kulizungumzia kwa kuwa mama Kanumba ni sawa na mama yake mzazi na siku zote mkubwa hakosei na anamheshimu sana.

Ahimili ya mitandaoni

Lulu alijua kujitofautisha na wasanii wengine ambao wamekuwa wakiishiwa ujasiri na ustahimilivu wa kero za watu wa mitandaoni hata walipokuwa wanamuuliza ataolewa lini.

Mmoja wa shabiki wake katika mtandao wa Instagram, Lowata Soningo aliuliza “hivi dogo uliolewaga na jamaa yetu au mliishiaga wapi?” na Lulu akamjibu “tupotupo tu, mbele hatuchezi wala nyuma hatutingishiki broo.”

Shabiki mwingine, Beda Ayman aliandika “uzee unakaribia shoga, fanya uolewe” na Lulu akajibu “Beda, kuolewa kwani ni anti-uzee?” akimaanisha kunazuia kuzeeka.

Hata Lulu alipoweka video fupi ikimwonyesha akiwa amekumbatiana na Majizo na shabiki mmoja akamuuliza “anakuoa lini?” alijibu kirahisi kabisa, “hana hata mpango, njoo mpige.”

Maswali ya kumdhihaki yalikuwa mengi na majibu yalikuwa ya kuchekesha badala ya kuudhi kama alivyokuwa anaulizwa.

Lulu na Majizo

Licha ya kuhusishwa kutoka kimapenzi na wanaume kadhaa, wafuatiliaji wa mambo wanasema Lulu na Majizo walikuwa na uhusiano kwa muda mrefu kabla ya kuamua kuuweka wazi mwaka 2018.

Lulu, mhitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma alikosomea rasilimali watu na utawala bora, hajawahi kuhusishwa na mwanaume mwingine kama ilivyo kwa wasanii wenzake ambao mara kadhaa husikika wakibadilisha wenza kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, Lulu anaingia kwenye ndoa hiyo Takatifu kwenda kujenga familia na Majizo mwenye watoto kadhaa wanaofahamika.

Ndoa ya wawili hawa imefanyika kimyakimya huku picha na habari zake zikirushwa kwanza na vyombo vinavyomilikiwa na Majizomwenyewe ambavyo ni ETV na EFM.Advertisement