Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpaka wa Holili wajipanga kukabili Ebola

Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mpaka huo ambao ni kati ya nchi jirani ya Kenya na Tanzania katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro umekuwa na mwingiliano kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazofanyika katika mpaka huo.

Rombo. Wakati mamlaka zikiendelea kuongeza umakini na kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini, hali katika mpaka wa Holili uliopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, imeelezwa kuwa shwari huku kukiwa hakuna taarifa za uwepo mshukiwa au mgonjwa wa ugonjwa huo mpaka sasa.

Akizungumzia hali ya mpaka huo leo Juni 4, 2026, Kaimu Ofisa Mfawidhi Afya kwenye mpaka wa Holili, Petro Mwani amesema hatua mbalimbali za tahadhari zinaendelea kuchukuliwa mpakani hapo ili kuzuia uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini.

Amesema wasafiri na wakazi wa maeneo ya mpaka huo wanahimizwa kuendelea kuzingatia miongozo ya afya inayotolewa na mamlaka husika.

Aidha, amesema kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea katika mataifa jirani, maofisa wa afya mpakani hapo wamechukua tahadhari zote muhimu, ikiwemo kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi ambao hukutana na wasafiri wa aina tofauti wanaovuka mpaka huo.

“Sisi kama maofisa afya mpaka wa Holili tumechukua tahadhari ikiwemo kutoa elimu kwa makundi kadhaa wakiwemo wafanyakazi ambao tunakutana na wasafiri mbalimbali,” amesema ofisa afya huyo.

Amesema: “Mpaka sasa tumetoa elimu kwa madereva, wanajamii wanaotuzunguka kwa ujumla. Hapa mpakani tunafanya ukaguzi wa wasafiri wote wanaotoka nchi ambazo zina mlipuko kama Uganda na DRC Congo, lakini tuna taratibu za kuwaripoti kwa ajili ya uchunguzi na kujua historia zao.”

Amesema, hatua nyingine walizochukua ni kuelimisha wasafiri na madereva namna ya kuchukua tahadhari na kutoa taarifa endapo watamuona muhisiwa wa ugonjwa huo, na wao kuchukua tahadhari kwa kutumia vitakasa mikono kwa maji tiririka.

"Mpaka upo shwari hatujapata mshukiwa yoyote wa Ebola na kama ikitokea kuna utaratibu maalumu wa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya taratibu zaidi,"amesema.

Wakizungumza baadhi ya wananchi ambao wamekuwa  wakitumia mpaka huo, wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ulinzi wa afya mpakani.

Mmoja wa wasafiri hao, Elia Wambui, raia wa Kenya, amesema utaratibu uliowekwa mpakani hapo ni mzuri na unatoa uhakika wa usalama kwa wasafiri.

“Utaratibu huu wa hapa mpakani ni mzuri na unaonekana kuwa salama. Serikali inapaswa kuendelea kuusimamia vizuri, hasa katika suala la kunawa mikono. Upande wetu hatuoni utaratibu wa aina hii kwa kiwango hiki,” amesema.

Naye, msafiri mwingine, Wanjiku Mtua ameipongeza Serikali kwa kuchukua tahadhari hiyo kwa umakini mkubwa katika mpaka huo ambao unapita mamia ya wananchi.

“Nimetokea Kenya na nimeona utaratibu uliowekwa hapa, hakika ni salama kwa wananchi. Tunashukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza hatua hizi za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala amesema Serikali imechukua tahadhari zote ikiwemo kuweka vifaa vya kisasa katika mpaka huo ili kujikinga na ugonjwa huo.

“Serikali imetuletea gari la wagonjwa na vifaa vya kisasa vya afya ambavyo vipo katika mipaka yetu ambavyo vinasaidia wataalamu wetu kutambua na kuzuia chochote kitakachoweza kujitokeza dhidi ya ugonjwa huu,” amesema Mwangwala.