Tanzania ipo salama dhidi ya Ebola – Mwigulu
Waziri Mkuu Mwigulu Nchema akizungumza wakati akijibu maswali ya papo kwa papo Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Ebola ni ugonjwa hatari wa homa ya kuvuja damu unaosambazwa kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.
Dar/Mbeya. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Tanzania bado ipo salama dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 4, 2026 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mtwara, Asha Salum Motto, ambaye alitaka kujua jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na ugonjwa huo kutokana na mahusiano ya kibiashara na kijamii yaliyopo kati ya Tanzania na nchi jirani zilizoathirika.
“Mpaka sasa tuko salama, nchi yetu ipo salama. Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba bado hatujaripoti kisa chochote cha Ebola nchini,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema Tanzania si kisiwa na inaendelea kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu kupitia biashara, utalii na shughuli nyingine za kijamii, hali inayolazimu Serikali kuendelea kuwa makini katika kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya Ebola pamoja na kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani na vituo vya kuingilia wageni kutoka nje ya nchi.
Amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona dalili zinazofanana na Ebola badala ya kuficha hali zao za afya, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti maambukizi endapo kutatokea mgonjwa.
“Tuendelee kuchukua tahadhari, kuelimishana na kuwa tayari kufanyiwa uchunguzi pale inapohitajika. Ni muhimu kutokuficha dalili au taarifa zinazoweza kusaidia wataalamu wa afya kuchukua hatua kwa wakati,” amesema.
Dk Mwigulu amesema Wizara ya Afya chini ya Waziri wake Mohammed Mchengerwa, imeendelea kushirikiana na wataalamu wa afya kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huo katika nchi jirani na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu hali halisi ya tahadhari zilizopo nchini.
Kauli hiyo imekuja wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) na mamlaka za afya katika ukanda wa Afrika zikiongeza juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo unaoendelea kuripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Hadi kufikia Juni Mosi 2026, DRC ilikuwa imeripoti wagonjwa 121 waliothibitishwa na wagonjwa 1,077 wanaoshukiwa kuwa na Ugonjwa wa Virusi vya Ebola vya Bundibugyo, ikiwa ni pamoja na vifo 17 miongoni mwa wagonjwa waliothibitishwa na vifo 246 miongoni mwa wagonjwa wanaoshukiwa.
Uganda ilikuwa imeripoti wagonjwa 11 waliothibitishwa kukiwa na kifo kimoja kilichorekodiwa. Jumla ya watu 642 waliogusana na wagonjwa walikuwa wametambuliwa ambapo 638 kati yao walikuwa chini ya ufuatiliaji wa karibu, jambo linaloonyesha hatari zinazoendelea za maambukizi na haja ya kuimarisha uratibu wa mipakani.
Ebola ni ugonjwa hatari wa homa ya kuvuja damu unaosambazwa kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo. Dalili zake ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa, udhaifu mkubwa wa mwili, kutapika, kuharisha na wakati mwingine kutokwa damu.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko, kuboresha maabara na kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya dharura ya afya ya umma.
Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuendelea kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na kuepuka kusambaza taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kusababisha taharuki isiyo ya lazima.
Udhibiti waendelea mipakani
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara wilayani Kyela, Kenedy Msaula amesema wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika mpaka wa Kasumulu na vifaa kinga walivyoweka kwa wananchi.
“Sisi tunaofanya biashara za ndani na nje ndio tunasaidiwa kwakuwa wengi tunakuwa hatuna elimu yoyote na ugonjwa huu, hivyo tunapopewa ushauri lazima tuuzingatie haswa kwa nchi za jirani tunasikia maambukizi ni mengi.
“Kwa ujumla tunawashukuru na kuwapongeza wataalamu wetu kwa hatua stahiki wanazochukua kutukinga na ugonjwa huu, niombe wenzangu kutoa ushirikiano wanapoona utofauti ili wote tuwe salama” amesema Msaula.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabet Nyema amesema wanaendelea kuimarisha usalama kwa wananchi hasa katika maeneo ya mipakani ikiwamo Kasumulu wilayani Kyela mkoani humo.
Amesema wataalamu wa afya kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za usalama wakiwamo Uhamiaji, wanaendelea kuimarisha usalama kwa kufanya uchunguzi wa afya kwa wanaoingia na kutoka ndani na nje ya mkoa.
“Tunaendelea pia kutoa elimu kwa wananchi kunawa mikono, kupunguza mikusanyiko isiyo ya lazima, tunachunguza wananchi wanaotoka nje kwenye maeneo ya mipaka na uwanja wa ndege.”
“Wananchi waendelee kufuata miongozo wanazopewa na wataalamu, tuchukue hatua stahiki kuhakikisha kila mmoja wetu anakuwa salama, lakini hata sehemu za kulala wageni tumeimarisha usalama tukishirikiana na mamlaka nyingine ikiwamo Uhamiaji” amesema Dk Elizabeth.