Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ebola tishio DRC, wagonjwa waongezeka kwa kasi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus jana amefanya ziara katika Mkoa wa Ituri, ambao umeathirika zaidi na mlipuko huo, ili kujionea mwenendo wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Muktasari:

  • Wiki mbili baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza mlipuko huo, zaidi ya wagonjwa 1,000 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola wameripotiwa nchini humo na watu wasiopungua 246 kufariki dunia.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Sekta ya Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) likitarajia kukutana leo Juni 1 na 2, 2026 kujadili hatua za kikanda za kukabiliana na Ebola, imeelezwa kuwa maambukizi ya ugonjwa huo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yanaongezeka kwa kasi na kufikia kiwango cha kutia hofu.

Shirika la kimataifa la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) limesema wiki mbili baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza mlipuko huo, zaidi ya wagonjwa 1,000 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola wameripotiwa nchini humo huku watu wasiopungua 246 wakifariki dunia.

Kwa mujibu wa MSF, mamia ya sampuli za wagonjwa bado hazijafanyiwa uchunguzi wa maabara, jambo linalofanya iwe vigumu kufahamu ukubwa halisi wa tatizo.

Naibu Mkurugenzi wa MSF, Dk Alan Gonzalez amesema hali ya sasa inatia wasiwasi kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa katika kipindi kifupi tangu mlipuko huo kutangazwa rasmi.

“Hatukuwahi kushuhudia mlipuko wa Ebola wenye idadi kubwa ya visa kwa muda mfupi kiasi hiki tangu kutangazwa kwake,” amesema Gonzalez.

Ameeleza timu za afya zilizopo maeneo yaliyoathirika zinashuhudia juhudi za kudhibiti ugonjwa huo zikishindwa kwenda sambamba na kasi ya maambukizi.

Aidha, changamoto za usafiri, kufungwa kwa baadhi ya mipaka na viwanja vya ndege pamoja na hali ya usalama katika maeneo ya mashariki mwa DRC zimeendelea kuchelewesha utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus, amefanya ziara katika Mkoa wa Ituri, ambao umeathirika zaidi na mlipuko huo, ili kujionea mwenendo wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kutathimini changamoto zilizopo.

Akiwa katika mji wa Bunia, Dk Tedros amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kudhibiti maambukizi. Amesema wananchi wanaelewa vyema mazingira yao na wanaweza kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la tatizo hilo.

Pia ametoa tahadhari kuhusu mila za mazishi zinazohusisha kugusa miili ya marehemu, akisema tabia hiyo inaweza kuongeza kasi ya maambukizi.

“Ni muhimu kuheshimu na kuomboleza waliopoteza maisha, lakini lazima tuepuke vitendo vinavyoweza kusababisha maambukizi zaidi na kuongeza idadi ya vifo,” amesema.

Ebola huenezwa kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, ikiwamo damu, mate, jasho, mkojo, matapishi na kuhara. Ugonjwa huo pia unaweza kuambukizwa kwa kugusa vitu vilivyochafuliwa na majimaji hayo.

Katika mji wa Bunia, shughuli za kila siku zinaendelea kama kawaida, ingawa hatua za tahadhari zimeimarishwa. Katika uwanja wa ndege wa mji huo, wasafiri wanatakiwa kunawa mikono kabla ya kuingia au kutoka, huku ujumbe wa elimu ya afya ukitangazwa kupitia redio, televisheni na mabango katika lugha mbalimbali za wenyeji pamoja na Kifaransa.

Maabara ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba ya Baiolojia iliyopo Bunia sasa imeanza kutoa majibu ya vipimo ndani ya saa 24, hatua inayotarajiwa kusaidia kubaini wagonjwa mapema na kuanza matibabu kwa wakati.

Wakati huohuo, Uganda imethibitisha wagonjwa tisa wa Ebola na kifo kimoja, huku mamlaka za afya nchini Brazil zikichunguza mgonjwa mmoja anayeshukiwa kuwa na maambukizi hayo baada ya kurejea kutoka DRC.

Mlipuko wa sasa unasababishwa na aina adimu ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo hadi sasa haina chanjo iliyothibitishwa kufanya kazi, huku ikisababisha vifo vya takribani theluthi moja ya walioambukizwa.