Lusinde amshukia Mbowe sakata la uwekezaji bandari

Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (CCM)

Muktasari:

 Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (CCM) amewajibu baadhi ya watu wanaopinga makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wakuendeleza bandari nchini kupitia kampuni ya DP World.





Dodoma. Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (CCM) amewajibu baadhi ya watu wanaopinga makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wakuendeleza bandari nchini kupitia kampuni ya DP World.

Miongoni mwa waliokosoa makubaliano hayo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyeonya kuwa mkataba huo una viashiria vyote vya kuhatarisha usalama wa nchi, kiuchumi na kisiasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana Jumatano Juni 7, 2023 kupitia mitandao ya jamii alipokuwa akitoa msimamo wa chama hicho akiwa nchini Ujerumani, ambapo pia aliwataka wabunge kutopitisha azimio hilo hadi uwepo wa uelewa kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Juni 8, 2023 jijini Dodoma, Mbunge huyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), amesema kauli ya Mbowe ya kuhoji kwa nini makubaliano hayo hayahusishi bandari ya Zanzibar ni ya kibaguzi.

“Mbowe anayesema Rais na Waziri wanaotoka Zanzibar, ila bandari ni ya Dar es salaam. Hii inaweza ikaharibu Muungano, haya ni maneno yasiyo na uungwana, kwani anataka kutuaminisha ni kosa rais na waziri kutoka Zanzibar. Huo ni ubaguzi.

“Hivi Rais akitoka Kilimanjaro mipaka yake ya kutoa uamuzi ihusu milima tu? Vitu vingine visiguswe, asizungumze kuhusu korosho azungumzie Kilimanjaro tu? Haiwezekani?” anasema Mbunge huyo,” amesema.

Kuhusu madai ya kuwemo kwenye ziara ya wabunge waliosafirishwa kwenda nchini Dubai kwa ajili ya kujifunza, Mbunge huyo amesema: “Sio kweli mimi sikwenda Dubai huo ndio uzushi mimi nilikuwa namuuguza mke wangu alikuwa amelazwa India.”

Kuhusu mkataba huo kutokuwekwa wazi, Mbunge huyo amesema Serikali inafanya mambo yake kwa siri na haiwezi kila kitu kukiweka wazi.

“Hata tukifika chooni tunafunga mlango baadhi ya mambo ni lazima yawe ya siri,” amesema Mbunge huyo.

Mbali na Lusinde, leo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa ametolea ufafanuzi suala hilo akisema mkataba huo ni wa miezi 12 na baada ya hapo kutakuwa na mikataba ya utekelezaji.

Kwa upande mwingine, Spika wa Bunge Dk Tulia Akson anesena leo bungeni kuwa litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.