Ma-DC Lindi wapewa siku 90 kutengeneza madawati 24,810

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Taleck amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kushirikiana na viongozi wa vijiji kuvuna mbao kwa ajili kutengeneza madawati 24,810 ndani ya miezi mitatu ili kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.  

Lindi.  Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Taleck amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kushirikiana na viongozi wa vijiji kuvuna mbao kwa ajili kutengeneza madawati 24,810 ndani ya miezi mitatu ili kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.

Agizo hilo amelitoa kwenye kikao cha wadau wa elimu baada ya ofisa elimu Mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo kusoma taarifa ya maendeleo ya elimu na changamoto zake katika mkoa huo.

Kayombo amesema kwenye idara ya elimu mkoa una mafanikio ya kuongezeka kwa ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa kila mwaka huku akitaja changamoto ya upungufu wa madawati 24,810 unaosababisha wanafunzi kukaa chini kwenye sakafu.

'Tunaomba kutengeneza mkakati maalumu wa utengenezaji madawati ili kuwaondoa watoto hawa wanaokaa chini” amesema Kayombo.

Mkuu wa Wilaya Nachingwea, Hashimu Komba amesema kuwa watawashirikisha wananchi ili shughuli hiyo ikamilike kwa wakati.

 Diwani kata ya Kibutuka wilaya Liwale, Faraji Mnyira ameshauri shughuli hiyo kufanyika kwa kwa umakini ili kuondoa tatizo la madawati kwa wanafunzi.