Maalim Seif: Magufuli akutane na wapinzani wote kujadili uchaguzi huru na haki - VIDEO

Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wahariri na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, alipotembelea kampuni hiyo jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mshauri mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amemshauri Rais wa Tanzania, John Magufuli  kukutana na viongozi wa vyama vyote vya upinzani kujadili kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kuwa huru na haki.

Dar es Salaam. Mshauri mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amemshauri Rais wa Tanzania, John Magufuli  kukutana na viongozi wa vyama vyote vya upinzani kujadili kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kuwa huru na haki.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 4, 2020 katika ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa licha ya mazungumzo ya jana ya  Magufuli na baadhi ya viongozi wa upinzani  akiwemo yeye, bado yanahitajika  mazungumzo yatakayowahusisha wapinzani wote.

Jana katika kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kuibua matumaini mapya ya maridhiano, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa vyama vya upinzani Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kuhimiza haja ya kudumisha amani, usalama na upendo.

Viongozi waliokutana na Rais kwa nyakati tofauti ni Maalim Seif,  Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Hata hivyo, haikueleweka mara moja kama kukutana huko kutakuwa na mwendelezo wa vikao vingine vya viongozi wengine wa upinzani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alipoulizwa kwa simu alisema suala hilo ni siri ya ratiba za rais. “Siwezi kusema kama kutakuwa na mikutano mingine au hapana. Hilo litategemea uamuzi wa rais na hao wanaotafuta kuon-ana naye au ambao anataka kukutana nao,” amesema Msigwa.

Lakini katika mahojiano leo na Mwananchi Maalim amesema, “ nafikiri rais anatakiwa akutane na vyama vya upinzani na wajadili suala la tume huru patakuwa na hoja za upande wao na wapinzani nao wana hoja zao, majibu yatakayotolewa yatafika mahali mtasikiliza na kuridhika.”

“Nadhani hilo rais angelifanya. Wakurugenzi (wa uchaguzi) ni sehemu ya sekretarieti ya tume (ya Taifa ya Uchaguzi) na wote wale ni makada wa CCM. Na ikiwa wameshaambiwa kwamba lazima waiangalie CCM ndio imewafikisha hapo.”

Ameongeza, “itakuwa jambo la ajabu kuwatangaza wapinzani. Nchi hii wengi wa watu wanategemea riziki kutoka serikali, wapo wanaojiajiri wenyewe ila wa serikalini kila mmoja ana hofu asipoteze kitumbua chake.”

“Rais aitishe kikao cha viongozi wa vyama kwa pamoja na baada ya hapo mnaweza kuzungumza mnaendeleaje baada ya hapo. Hatua ya kwanza angekutana na vyama.”

Katibu huyo wa zamani wa CUF amesema, “siwezi kusema asilimia 100 kuwapa uhakika wa kikao cha jana kwa sababu haya mamlaka na madaraka hayapo mikononi mwangu yapo kwa Magufuli.”

“Sasa hivi wakati umefika inawezekana hakuna kisichowezekana, Zanzibar tuliposema maridhiano muda ulikuwa mfupi lakini iliwezekana. Mapendekezo ya tume ya Jaji Warioba (Joseph-aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba)  yapo pale na yanasema nini kuhusu tume huru, kwanza fanyeni hayo.”

Maalim amesema, “Zanzibar ingekuwa tuna watu waadilifu ingekuwa nafuu, tume (ya uchaguzi Zanzibar -ZEC) inaajiri yenyewe kuanzia wilaya hadi majimbo, ila kutangaza matokeo ni kujaribu kuonyesha sheria imefuatwa ila wanaoteuliwa ni wa mlengo wa huko. ZEC wangetafuta watu wanaoaminika ingekuwa nafuu   kuliko bara.”

Amesema ingekuwa muda unatosha katiba ya nchi ingebadilishwa huku akikumbusha kusimama kwa mchakato wa katiba mpya mwaka 2014 kupisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Mchakato huo uliishia katika kura ya maoni.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi. Mahojiano na Maalim Seif yapo moja kwa moja kupitia MCL Digital