Maambukizi mapya ya VVU yashuka nchini

Thursday May 19 2022
vvu pic
By Mwandishi Wetu

Morogoro. Maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU) yameshuka nchini kutoka watu 68,000  mwaka 2020 mpaka kufikia watu 54,000 kwa mwaka 2021.
Sambamba na maambukizi mapya, vifo vitokanavyo na Ukimwi navyo vimetajwa kushuka kutoka 32,000 mwaka 2020 na kufikia vifo 29,000.
Hayo yamesemwa leo Mei 19 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk Leonard Maboko wakati wa mkutano maalumu uliolenga kuangalia hali ya maambukizi nchini chini ya ufadhili wa shirika la Pact Tanzania.
Dk Maboko amesema licha ya maambukizi kupungua bado hatujaweza kufikia malengo ya kidunia kwani ili kudhibiti janga ni lazima idadi ya maambukizi mapya iwe chini ya vifo vitokanavyo na ukimwi.
“Takwimu mpya zinaonyesha maambukizi mapya na vifo vimepungua kwa sasa maambukizi mapya ni 54,000 na vifo ni 29,000, lakini bado tuna kazi kubwa. Maambukizi mapya yatakapokuwa chini ya vifo pale ndipo tunaweza kusema sasa tunafanikiwa kuanza kutokomeza ugonjwa huu,” amesema Maboko.
Amesema tayari kuna mwelekeo mzuri kama nchi kwakuwa maambukizi mapya yamekuwa yakipungua kwa miaka 10 sasa lakini bado kuna changamoto kwa vijana hasa maambukizi mapya.
 “Takwimu zinaonyesha katika maambukizi mapya kila mwaka asilimia 40 ya vijana wanapata maambukizi na kati yao vijana wa kike ni asilimia 80 kwa mwaka 2021 takwimu zimeonyesha vijana wanachangia kwa asilimia 28 ya maambukizi mapya na hawa ni wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 hali inayotupa changamoto,” amesema Dk Maboko.
Hata hivyo amesema bado kumekuwa na mwamko mdogo wa ufuatiliaji wa matibabu na kipima kwa wanaume.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi, amesema maambukizi ya virusi vya ukimwi hayasababishwi na damu pekee bali majimaji yatokayo mwilini huambukiza pia VVU
“Lakini pia katika upimaji hata majimaji ya kwenye fizi yanaweza kuonyesha viashiria vya uwepo wa vimelea vya virusi vya ukimwi ndiyo maana kwa sasa kuna vipimo ambavyo mtu anaweza kujipima mwenyewe,” amesema Dk Mwakyosi.
Amesema mtu anayepima na kuanza kutumia dawa mapema anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufubaza virusi.

Advertisement