Maandamano ya Chadema kuhitimishwa Arusha
Muktasari:
Leo Jumatatu, Februari 26, 2024, msimamizi wa maandamano hayo kanda ya kaskazini, Salum Mwalimu amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwamo kibali cha uwanja wa reli wanapokutania na vibali vya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Arusha. Maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyoanza Januari 24 mwaka huu Dar es Salaam yanahitimishwa kesho Jumanne, Februari 27, 2024 jijini Arusha.
Lengo la maandamano hayo yaliofanyika Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya yaliyopewa jina la ‘vuguvugu la haki ya Watanzania’ ni kuishinikiza Serikali kushughulikia tatizo la gharama za maisha.
Pia, kuitaka Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kwenye miswada ya uchaguzi iliyokuwa imepelekwa bungeni Novemba 10 mwaka jana na kujadiliwa katika mkutano wa bungeni kisha kupitishwa na sasa inasubiriwa kusainiwa na Rais kuwa sheria.
Maandamano hayo yalianzia jijini Dar es Salaam kwa waandamanaji wakiongozwa na viongozi wao wakuu, Freeman Mbowe (mwenyekiti), Tundu Lissu (makamu mwenyekiti-bara), John Mnyika (katibu mkuu) na wajumbe wa kamati kuu kuandamana kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), zilizopo Ubungo, kufikisha ujumbe wao huo.
Maandamano kama hayo yalifanyika jijini Mwanza Februari 15 mwaka huu kwa kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kumalizikia Viwanja vya Furahisha kulipofanyika mkutano wa hadhara.
Wamefanya hivyo jijini Mbeya, Februari 20 na kuhitimishwa Viwanja vya Rwanda Nzovwe ambapo hata hivyo, mkutano haukufanyika kwa kuwa mvua ilikuwa kubwa na kesho watahitimisha kwa maandamano yakiongozwa na Mbowe, Lissu na Mnyika.
Maandamano hayo yatafanyika katika Barabara Kuu tatu za kuingia mjini Arusha ikiwamo Barabara ya Arusha-Moshi, Arusha- Dodoma na Arusha – Simanjiro yote yataishia Uwanja vya Reli utakapofanyika mkutano wa hadhara.
Leo Jumatatu, Februari 26, 2024, msimamizi wa maandamano hayo kanda ya kaskazini, Salum Mwalimu amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwamo kibali cha uwanja wa reli wanapokutania na vibali vya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha.
“Tumeshalipia uwanja wa reli tutakapokutania na kufanya mkutano na Jeshi la Polisi wametupa kibali hivyo hakuna cha kuhofia wananchi wote wajitokeze kupaza sauti zetu za pamoja kupinga udhalimu huu na manyanyaso ya,” amesema Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar
Amesema zaidi ya viongozi wa juu wa Chadema 17 watakuwepo akiwamo Mbowe, Tundu Lissu na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kaskazini Godbless Lema.
Mwalimu amezitaja njia watakazopita ni kwa wananchi wa mji wa Moshi na Tanga wataungana na wananchi wa Arusha waishio Maji ya Chai, Usa na Tengeru katika eneo la Ngulelo na maandamano yataanza saa mbili asubuhi.
“Msafara huo utakuja moja kwa moja kufuata barabara hiyo ya Arusha –Moshi hadi Sanawari, Mianzini na watakunja kona kuelekea viwanja vya Sheikh Amri Abeid na kupita hadi Barabara ya Soko Kuu kabla ya kuelekea mnara wa mwenge na mzunguko wa mnara wa saa na kuishia viwanja wa reli kupitia barabara ya Fire,” amesema Mwalimu.
Kwa wakazi wa Singida, Kondoa na wilaya za Karatu na Monduli, Mwalimu amesema wataungana na wananchi wengine kutoka Kisongo, Ngaramtoni, Kwa Mrombo na Majengo katika makao makuu ya Tanapa na wataandamana kufuata Barabara ya ‘Eso Mataa’ hadi Soko la Kilombero na kukata kona kuelekea viwanja vya reli.
Amesema kwa wananchi wanaotoka Muriet, Mkonoo, Nadosoito, Intel, Patel na Sokon One watakutana kwenye kijiwe cha Bajaji eneo la ‘Uswahilini’ na kupandisha hadi Sinoni kisha kufuata uelekeo wa Uwanja wa Reli.
“Maandamano yote yataanza saa mbili asubuhi, hivyo wananchi mjitahidi kudamka kuonyesha kweli tuna jambo tunataka lifanyiwe marekebisho na Serikali,” amesema Mwalimu.
Katika hatua nyingine, Mwalimu amesema kutokana na Serikali kutangaza leo kuaga miili ya watu 25 waliopoteza maisha katika ajali ya magari Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, watajipanga mapema namna ya kuwezesha wananchi walioko kwenye maandamano kutoa mkono wa pole.
“Kwa sababu Serikali imetangaza kuaga miili ya wapendwa wetu kesho katika viwanja wa vya Sheikh Amri Abeid basi na sisi tutajipanga kuhakikisha tunapita hapo kwa umoja wetu kutoa mkono wa pole kwa wafiwa na kisha tutaendelea na shughuli yetu ya madai ya msingi,” amesema Mwalimu
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema heshima hizo za mwisho zitatolewa uwanjani hapo na Serikali watagharamia mazishi na majeneza kwa watakaohitaji na zaidi watatoa Sh1 milioni kwa kila mwili.
“Heshima hizi hazilengi kuingilia shughuli za maandamano maana tunajua wako kisheria, lakini lazima pia shughuli zingine ziendelee hasa hizi za kuwapa heshima wenzetu walipoteza maisha,” amesema Mongella.
Watu hao walifariki dunia katika ajali ya magari manne baada ya lori kufeli breki na kusababisha vifo hivyo vikiwemo vya raia wa kigeni eneo la Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Kiongozi wa ‘Sauti ya Watanzania’ Dk Wilbrod Slaa amesema maandamano hayo hayalengi kumpindua mtu yeyote wala Serikali bali kuwasilisha hoja kwa sauti moja ya umma ili kushinikiza kuboreshwa kwa masilahi ya Taifa.
“Wananchi msiogope kujitokeza kuandamana na kupandisha mabango yenye jumbe za kusema yale mnayohisi mnaonewa kwa sababu hayalengi kumpindua mtu bali wala Serikali yetu bali waamke kutekeleza yale ambayo yanapigiwa kelele kila kukicha,” amesema Slaa.
Wakili Boniface Mwabukusi amesema maandamano hayo wanataka yalete mabadiliko katika utendaji kazi wa Serikali iliyoko madarakani.
“Tunaandamana mapema kuwaonya kwenye chaguzi zijazo wasije wakarudia waliyoyafanya kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, tunaandamana kuiamsha Serikali usingizi waliolala la kushindwa kuzalisha wataalamu wenye kushindania fursa za ajira kimataifa badala yake tunauza fursa kwa wageni kwenye sekta zote zinazoweza kufanywa na wazawa,” amesema Mwabukusi.