Maaskofu Katoliki wakemea utekaji, wataka viongozi wawajibike
Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limelaani matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini na kuvitaka vyombo vya dola kutimiza wajibu wake ipasavyo, ili kurudisha heshima ya Tanzania iliyozoeleka ya kuwa ni kisiwa cha amani.
Mbali na hilo, maaskofu hao wamesema viongozi waliopo kwenye nafasi za kusimamia matukio hayo yasitendeke kama: “Hawakuwajibika kwa kadri ya nafasi zao wawajibishwe.”
Huo ni ujumbe TEC uliotolewa leo Jumapili, Septemba 15, 2024 katika Kilele cha Kongamano la tano la Ekaristi Takatifu la Kanisa Katoliki, linalofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Akisoma ujumbe huo, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa amesema kauli mbiu ya kongamano hilo ni ‘Udugu huponya ulimwengu, sisi sote ni ndugu.’ Amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa inasifika kama kisiwa cha amani licha ya tofauti za kidini, kikabila na kiitikadi bado umoja ulitawala, lakini kwa hali ilivyo sasa inakwenda tofauti.
“Matukio yaliyotokea karibuni ya watu kutekwa na hata kuuawa, tunajiuliza nini kimetokea, Taifa letu limekosea wapi je, uongozi na mamlaka husika na vyombo vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hadi kushindwa kudhibiti hali hii?
“Sisi maaskofu hatuamini kama makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu ya ulinzi na usalama. Hivyo tunaviomba vyombo kutimiza wajibu wake ili kurudisha heshima yetu ya misingi ya udugu na amani,” amesema Nzingilwa ambaye pia ni Askofu Jimbo la Mpanda.
“Tunaungana na watu, taasisi, jumuiya za kimataifa kulaani na kukemea vitendo hivi vya kihalifu na utekaji, tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka ili wale wote waliohusika na matukio hayo wafikishwe mbele ya sheria,” amesema na kuongeza:
“Na ambao hawakuwajibika kwa kadri ya nafasi zao wawajibishwe. Uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu, mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake mwenyewe. Maisha na utu wa mtu lazima viheshimiwe na kulindwa kwa nguvu zote.”