Maaskofu walia uchaguzi huru

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo.

Moshi. Siku tatu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, maaskofu wa makanisa ya Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Angalikana Tanzania na lile la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) wameibua changamoto 12 zinazolitesa Taifa kwa sasa, huku suala la uchaguzi wa huru na haki likitawala.

Mambo hayo 12 yamo katika salamu za Pasaka 2024, ambazo maaskofu hao wamezituma kwa waumini wao na Taifa, wakitaka yafanyiwe tafakuri wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya ufufuko wa Yesu Kristo.

Katika salamu hizo, Askofu Fredrick Shoo wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini amezungumzia uchaguzi ujao, akitaka usiwe tu huru na haki, bali uaminike mbele ya macho ya jamii.

Kwa upande wake, Dk Dickson Chilongani, askofu wa Kanisa la Angalikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), yeye alienda mbali na kutaka Watanzania kuwaamini wanawake kuwa wanaweza na kuwapa nafasi katika uchaguzi huo.

Mwingine aliyezungumzia uchaguzi ni Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula ambaye aliwataka watawala wanaosimamia michakato ya uchaguzi wa serikali za mitaa, watende haki na uchaguzi ufanyike kwa haki na amani.

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwakani, huku Watanzania wakiwa na kumbukumbu ya kilichojitokeza katika uchaguzi wa 2019 na 2020, ambao madai ya kutokuwa huru wala haki yalitawala maeneo mengi nchini.


Mengi yanayolitesa Taifa

Mbali na uchaguzi, salamu hizo zimebeba ujumbe pia kuhusu kuporomoka kwa maadili, ubinafsi uliokithiri, kukosa uaminifu na hofu ya Mungu, ulevi wa pombe uliokithiri, hususan kwa vijana, matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya rushwa na kupuuza uwezo wa mwanamke kiuongozi.

Pamoja na hayo, ujumbe huo pia unakemea matumizi mabaya ya madaraka, haki kununuliwa, upendeleo na ubaguzi, amani na mabadiliko ya tabianchi.


Salamu za Askofu Shoo

Katika salamu zake, Askofu Shoo ambaye ni mkuu mstaafu wa KKKT, ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa za maendeleo na ujenzi wa demokrasia anayoionyesha tangu aingie madarakani.

Sambamba na pongezi hizo, Askofu Shoo anasema “hata hivyo tunazidi kutoa wito kwa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuheshimu maoni ya wananchi, hususan kuhusu marekebisho ya Katiba na sheria za uchaguzi na ya vyama vya siasa ya mwaka 2019.”

“Tunataka kuwa na uchaguzi huru na wa haki katika kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani. Wananchi tuwachague viongozi waadilifu, waaminifu na wenye hofu ya Mungu, na tukatae kuhongwa,” anasema askofu Shoo katika salamu zake.

“Pasaka ni sikukuu muhimu kwa Wakristo. Tunaadhimisha kufa na kufufuka kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yesu alikuja ili "wote wawe na uzima tele. Uzima tele ni kiashiria cha jamii yenye afya ya kimwili, kiakili na kiroho,” anaeleza na kuongeza:

“Leo kuna vilio vingi katika jamii yetu, hakuna uzima tele. Kuporomoka kwa maadili, ubinafsi uliokithiri, kukosa uaminifu na hofu ya Mungu ndio chanzo cha maovu na maumivu mengi tunayoshuhudia leo katika familia, kanisa na jamii.

“Panahitajika mabadiliko ya tabia. Ndoa nyingi zimevurugika, vijana wanaangamia kwa ulevi wa pombe kali na madawa ya kulevya, malezi bora ya watoto ni changamoto. Tunahitaji kujenga familia imara ili kuwa na ustawi endelevu,” anasisitiza.

Askofu Shoo alitoa wito kwa viongozi wa dini na wanakanisa kumrudia Mungu kwa toba ili kujirekebisha na kuishi maisha yenye mfano bora kwa watoto na vijana, huku akisema mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa uzima wa dunia nzima.

Kwa upande wake, Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera alisema Agano Jipya na la Kale katika Biblia yanakubaliana “damu ni alama ya ukombozi na upatanisho, damu isiyo na hatia isipokomboa basi inakuwa na laana.”

“Damu ya Bwana Yesu Kristo ilikomboa na kutupatanisha na Mungu. Kwa kuwa haikuwa na hatia, walioimwaga wanaalikwa kupatana na Mungu ili kuepuka laana. Wanaoendelea kuimwaga damu isiyo na hatia wanaalikwa kutubu,” anasema katika salamu hizo.

“Mienendo yetu isiyofaa kama rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ukatili dhidi ya watoto, ukatili dhidi ya mazingira, udini, uitikadi, biashara ya kuuza na kununua haki na dhuluma dhidi ya Taifa letu vinatokana na roho za mafarakano.”

Askofu Bagonza anaendelea kuandika “kila eneo katika taifa letu kuna uvundo wa mafarakano. Mihimili karibu yote, yaani Bunge, Serikali na mhimili wa Mahakama kumejaa mafarakano na kuishi kwa tahadhari kubwa na hofu ya kuwindana.”

“Ndani ya taasisi za dini kuna moshi wa chuki kuliko harufu ya upendo. Mwathirika mkuu ni mpendwa wetu ‘haki’. Hatuwezi kutenda haki wala kusimamia haki ikiwa maamuzi yetu yamejaa hila, chuki, ubinafsi, rushwa na visasi”.

Askofu Bagonza anasema baadhi ya maamuzi yanaongozwa na itikadi, dini na makundi masilahi, hivyo kwa kuwa Kristo amefufuka, basi anawasihi wapatanishwe na warudi katika meza ya mapatano na kupatanishwa.

Katika hatua nyingine, Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Stephen Munga pia alitoa salamu zake akiegemea maneno ya Biblia 1Wakorintho 15:22 “Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu vililetwa na mtu.”

Anasema maneno hayo ya Mtume Paulo ni jumlisho zuri na fundisho la msingi linaloshikilia imani ya Wakristo na tumaini la kuishi duniani na kufufuka katika wafu.

“Ndani yetu tunazo nguvu za mauti na ndani yetu tunaweza kujitwalia nguvu za uzima. Badiliko kutoka utu wa mauti hadi kupata utu wa uzima hufanyika kwa njia ya kumwamini Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka,” alisema askofu Munga.

“Imani hiyo siyo kwa ajili ya maisha ya kiroho tu, bali ni msingi wa hata maisha yetu ya kila siku. Tunaishi kwenye ulimwengu wenye mvutano kati ya nguvu za mauti na nguvu za uzima. Tumeumbwa kuzishinda nguvu za mauti za ulimwengu.

“Katika ubinadamu wetu tumevikwa uwezo wa kuzishinda nguvu za mauti kama uonevu, njaa, rushwa, dhuluma, ukiukwaji wa haki, vita, ugomvi, unyanyasaji na ukandamizaji,” anasema Askofu Munga na kufafanua:

“Tendo hili la kufa na kufufuka kwa Yesu ndilo lifanyayo mabadiliko hayo makubwa. Kwa hiyo Pasaka ni tendo la mabadiliko na mapinduzi katika ulimwengu. Naomba Mungu ili kila mmoja wetu akawe balozi mwaminifu wa mabadiliko hayo makubwa.”


Wenye uwezo wajitokeze

Akifafanua salamu zake, Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula anasema mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa ambao nafasi yao ni muhimu sana katika jamii.

Akijenga hoja hiyo, anasema “miaka mitano iliyopita, Watanzania hawakupata fursa ya kuchagua kwa uhuru viongozi wanaowataka. Ili tusaidie nchi itawalike vizuri kuanzia chini, ili kutatue matatizo ya wananchi, kwanza watu wenye uwezo wajitokeze kugombea hizo nafasi.

“Lakini pia wapigakura wajiandae kisaikolojia kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka, lakini pia watawala wanaosimamia michakato ya uchaguzi wa serikali za mitaa, watende haki na uchaguzi ufanyike kwa haki na amani,” anasema Askofu.

Suala la uchaguzi pia limegusiwa na Askofu Dickson Chilongani wa DCT, ambaye anawataka Watanzania katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa wawaamini wanawake kwamba wanaweza kama Yesu Kristo alivyowaamini wanawake.

“Ukisoma somo la Marko wanawake ndio wako mstari wa mbele sana katika kufika kaburini alikozikwa Yesu. Kwenye uchaguzi tuwaamini wanawake kuwa wanaweza kama walivyojitokeza katika tukio la ufufuo wa Yesu. Yesu anawaamini kuwa wanaweza.

“Ndiyo maana katika ufufuo wanafunuliwa wao kwanza ndio wanajua, halafu wanaenda kuwaambia wanaume. Uchaguzi ujao tuwaamini wanawake kwamba wanaweza, lakini pia tuwe na moyo wa kusameheana kama Yesu alivyomsamehe Petro, badala ya kuwekeana visasi,” anaeleza.


Kuvumiliana jambo muhimu

Askofu Mkuu wa KKAM, Oscar Ulotu katika salamu zake, anawataka Wakirsto na Watanzania kuvumiliana, kusameheana na kuombeana, huku wakikumbuka kazi kubwa ya msalaba aliyoifanya Yesu Kristo.

“Tusherehekee sikukuu ya Pasaka kwa amani na utulivu tukikumbuka kazi kubwa ya msalaba aliyoifanya Yesu Kristo pale msalabani. Hakika tumenunuliwa kwa damu ya thamani kuu, hivyo ni wajibu wetu sote kujifunza kwake,” anasema.

“Hayo ni pamoja na kuwa wavumilivu, kuwasamehe wengine kama yeye alivyotusamehe, kuombeana na kutiana moyo, ubaguzi na magomvi miongoni mwetu viondoke na amani ya Kristo itawale mioyoni mwetu,” anasisitiza.

“Watanzania wote tumepewa jukumu moja tu la kuiombea nchi yetu amani na kuwaombea viongozi wetu siku zote ili watuongoze kwa haki na haki ikitamalaki na amani nayo itatamalaki nchini,” anaeleza Askofu Ulotu.